HILI NDO JAMBAZI SUGU LA ATM DAR ES SALAAM LILILO NUSURIKA KUUWAWA


Dar es Salaam. Msako wa wezi wa kwenye Mashine za Kutolea Fedha (ATM), umeanza kuzaa matunda baada ya raia wa Bulgaria kukamatwa akiiba kwenye ATM ya Bank of Africa (BOA), Tawi la Afrikana, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za benki, mtuhumiwa huyo ambaye 
hakutajwa jina lake alikamatwa baada ya kamera maalumu zilizowekwa kwenye ATM za BOA, kumtambua kuwa ni mwizi sugu wa benki hiyo anayetafutwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12 asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kuwekewa mitambo maalumu ya kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa malalamiko na baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha.
Chanzo hicho cha habari kilidai kuwa baada ya kupelekewa malalamiko hayo, waliweka mitambo maalumu ya kuwawezesha walinzi wa maeneo ya ATM za BOA kumbaini mtu atakayetoa fedha kwa njia ya wizi.
“Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alianza mchezo huo kwa muda mrefu ambapo kwa kutumia kadi za ATM zisizojulikana idadi yake, alikuwa anakwenda kwenye ATM mbalimbali za benki hiyo na kutoa fedha hadi Sh10 milioni.
Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao walimkamata na kumfunga pingu.
“Huyu mtuhumiwa mwenye asili ya Kiarabu alifika na gari lake saa 12 asubuhi, aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati anaingia ndipo alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
“Ni kweli taarifa nimezipata, mtuhumiwa amekamatwa, bado hatujajua ni kiasi gani ambacho ameiba kwa kutumia mtandao, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Wambura.
Tukio kama hili lilishawahi kutokea mkoani Mwanza Februari 19 mwaka huu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na maofisa ya Benki ya NMB liliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad