MATUSI NA KEJELI ZA KAGAME ZAMDUWAZA RAIS KIKWETE.

Baada ya kushambuliwa kwa kejeli na Rwanda, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kueleza kushangazwa na kauli hizo na maneno yasiyofaa yanayotolewa na viongozi wa nchi hiyo dhidi yake na Tanzania.

Badala yake amesema Tanzania haina mgogoro wowote na nchi hiyo wala haiwezi kufanya vitendo vyovyote vibaya dhidi yake, nchi nyingine jirani au yoyote duniani, kwani migogoro haina tija wala maslahi kwa Watanzania.
Rais Kikwete alieleza mshangao huo jana katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi ya kuzungumza na taifa, na kusema kuwa yeye binafsi na serikali ya Tanzania haina ugomvi wala nia yoyote mbaya na Rwanda.
"Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. 
Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu," alisema na kuongeza:
"Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake.  
Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yoyote.   Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.  Waingereza wanasema 'two wrongs do not make a right'.
Alikiri kuwa katika kipindi cha miezi miwili uhusiano baina ya nchi hizo umekuwa ukipita katika kipindi kigumu na kwamba kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yake na nchi ni ushahidi wa hali hiyo.
"Napenda kuwasisitizia kuwa mimi na serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi nyingine yoyote duniani. 
Hatuna sababu ya kufanya hivyo, kwani mambo hayo hayana tija wala maslahi kwetu," alisema.
Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania na Wanyarwanda kuwa, Tanzania inapenda kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo uhusiano wake na nchi zingine jirani na kuongeza kuwa kama majirani kila mmoja anamhitaji mwenzake, hivyo lazima uwepo uhusiano mwema.
Kwa mujibu wa Rais, wakati Tanzania imekuwa ikijihusisha siku zote na kukuza na kujenga ujirani mwema, kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano kwa maslahi ya nchi zote mbili na kwamba hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania kabla na baada ya kutokea sintofahamu.
Alisema Rwanda na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri miaka mingi, zikishirikiana na kusaidiana katika mambo mengi kitaifa, katika kanda ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, Umoja wa Afrika na hata kimataifa, hata hivyo mtikisiko huo umekuja baada ya kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda kufanya mazungumzo na mahasimu wao. 
"Nilitoa ushauri ule kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.  Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo (DRC) na kwa Serikali ya Uganda.  
Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema chochote pale mkutanoni lakini baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia," alisema.
Rais Kikwete alisema anastaajabu jinsi Rwanda ilivyouchukulia ushauri wake na haufanani na wanayoyafanya, huku akisisitiza kuwa alifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi za miaka mingi katika ukanda huo.
Alisema ni kawaida kukutana katika mikutano na vikao mbalimbali kuzungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea na kwamba wakati waliyachukulia kuwa ni mambo yanayohusu wote, hivyo kupeana ushauri ni wajibu wa wote. 
"Mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia sana.  Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu.  Jambo la kushutumiwa na kutukanwa!  
Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa.  Muungwana hujibu:  "Siuafiki ushauri wako".  Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo," alisema.
Alisisitiza Tanzania inapenda kuendelea na uhusiano mzuri na Rwanda na kuongeza kuwa labda kama Rwanda ina jambo dhidi ya Tanzania, kwa kile alichosema kusikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yake na nchi. Hata hivyo, alisema hapendi kuyaamini hayo yanayosemwa moja kwa moja lakini pia kama nchi hawatayapuuza.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema kauli yake aliyoitoa katika Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa ilitafsiriwa vibaya na kwamba hakutaja mtu wala nchi yoyote bali alizungumzia wajibu wa majeshi na raia kulinda uhuru na mipaka ya nchi.
Rais Kikwete alisema hataruhusu mtu au nchi yoyote kupokonya wala kuichezea haki ya Watanzania hiyo na kusisitiza utayari wa nchi kulinda mipaka yake, huku akitoa mfano wa mashujaa waliofariki dunia kwa kulinda nchi kuwa ni fundisho kwa mtu yeyote anayetamani kumega kipande chochote cha ardhi ya nchi ya Tanzania.
Baada ya kutoa kauli hiyo baadhi ya vyombo vya habari vilitafsiri kauli hiyo kuwa amewasema Malawi na Rwanda kutokana na kuwepo sintofahamu na viongozi wa nchi hiyo. Malawi na Tanzania wanagombea mpaka wa Ziwa Nyasa.
Alisisitiza kauli yake ya awali aliyoitoa mkoani Kagera ya kuwapa siku 14 wale wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa, badala ya kusubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita.
Pia alizungumzia ziara za viongozi wa mataifa mbalimbali akiwemo Rais wa Marekani, Barack Obama ambapo alisema ziara ya kiongozi huyo imeimarisha uhusiano mzuri baina ya mataifa mbalimbali pamoja na kutoa fursa na miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Alisema katika ziara hiyo, Rais Obama pia alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ameielekeza Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kutengeneza mkakati utakaoonesha jinsi watakavyojipanga kufaidika na mpango huo.
Alitaja viongozi wengine ambao walifanya ziara  hapa nchini kuwa ni Rais Mstaafu wa Marekani, George W Bush, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na  Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra, ambapo ziara za viongozi hao wote zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada za Tanzania kujiletea maendeleo.
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. kwa hili hongera mkuu,watuhukumu kwa busara zetu tumezaliwa hivyo na hatuwezi kuruhusu watutie vidole machoni

    ReplyDelete
  2. Hongera Mhe JK Mrisho kwa kutoa msimamo wa taifa letu, ni kweli ugomvi haujengi bali uongeza ukubwa wa tatizo. Watanzania tumejaliwa kuwa na busara na hekima, acha tuzitumie ili wao waje kuhukumiwa na busara na hekima zetu. Hongera kwa msimamo huu kuwa wa taifa letu pendwa. Na hii inathibitisha usemi wa kiswahili kuwa "MUUNGWANA AKIVULIWA NGUO UCHUTAMA".

    ReplyDelete
  3. Ala! Kikwete wewe muungwana tena hekima zako zinaheshimika duniani kote, asiyetaka basi asiupokee . Huyu ndiye Rais mwenye hekima

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad