MKOJO WA BINADAMU NA MAAJABU YAKE DUNIANI

Huwezi kuamini unapoambiwa kuwa mkojo ni bidhaa yenye umuhimu mkubwa kwako na jamii

 Johannesburg, Afrika Kusini. Jiulize, je, umeenda haja ndogo leo asubuhi au la?

Kama jibu ni ndiyo, basi ujue umemwaga kiasi kikubwa cha nishati ambacho pengine kingeweza kuokoa kiasi cha  fedha za kulipia bili ya umeme nyumbani kwako. Pia, mkojo una manufaa zaidi kwako ambayo huenda hukuyajua.

Wanayansi na watafiti nchini Uingereza wamevumbua nguvu za mkojo katika kuzalisha nishati ambayo inaweza kuchaji simu kwa muda wa dakika 25 na pia kumwezesha mteja kutuma ujumbe na kuperuzi intaneti.

Watafiti hao  kutoka Chuo Kikuu cha Watafiti cha Bristol wakishirikiana na wenzao wa Maabara ya Robot wanasema kuwa nishati hiyo ya mkojo ni mapinduzi ambayo yatasaidia katika upungufu wa nishati wakati wowote badala ya kutegemea jua au upepo.

Timu ya watafiti hao iliweka mkojo  katika chombo maalumu ambao baada ya muda ulizalisha bakteria.

Bakteria hao baada ya  kuwa na njaa huzalisha nguvu za kielektroni na kuwa nishati. Elektroni hizo hudondoshwa katika kontena maalumu kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Mmoja wa  wahandisi aliyevumbua nguvu za mkojo, Dk Ioannis Ieropoulo  wa Chuo Kikuu cha West of England (UWE), Bristol anasema, mkojo ni bidhaa ambayo haiwezi kutupungukia tofauti na bidhaa nyingine kama maji, upepo au jua.

Wavumbuzi hao wanasema mkojo ni nishati inayopatikana wakati wowote hivyo hatua hiyo inasaidia kuwa na uhakika wa kutopungukiwa na nishati hata kwa watu wa vijijini.

Anaongeza kuwa madhumuni hya uvumbuzi huo ni kupata nishati inayopatikana wakati wowote, rahisi kuiunda na itakayowasaidia watu wengi wa matabaka mbalimbali.

“Tumevumbua na tumehakikisha kuwa inafanya kazi. Kilichobaki sasa ni kuangalia uwezekano wa mkojo kutumika katika matumizi ya nyumbani,” anasema mhandisi huyo.

Mpaka sasa betri iliyoundwa kwa nishati ya mkojo huo ina uwezo wa kuchaji simu itakayoweza kudumu kwa dakika 25, kutuma ujumbe na kupiga simu kwa sekunde 20.

Pia, utafiti uliwahi kufanywa na Profesa Frederick Mwanuzi wa Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam, Kitengo cha Mazingira na kubaini kuwa binadamu anazalisha kilo 50 za kinyesi na lita 400 mkojo   kwa mwaka.
Profesa Mwanuzi anaeleza kuwa mkojo na kinyesi vinaweza kutumika kuzalisha nishati kwa mamilioni ya Watanzania.
Profesa huyo anasema walifanya majaribio katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam na katika vyoo mbalimbali na kuzalisha umeme katika baadhi ya nyumba hizo.
Watafiti hao wa Uingereza kwa upande wao wanasema hii ni mara ya kwanza kwa mkojo kuonyesha uwezo wa kutoa nishati ya kuchaji betri na ni mapinduzi makubwa.
 Wanasayansi wanaamini kuwa teknolojia hiyo ina manufaa makubwa katika jamii kwani huenda ikatumika katika bafu na vyoo na kuzalisha nguvu ya umeme kwenye mabomba ya bafuni, taa na kuchaji simu.
 Hata hivyo mkojo hauna manufaa katika nishati pekee, bali wanasayansi mbalimbali wamewahi kuthibitisha kuwa mkojo unaweza pia kutumika katika tiba.
 Mkojo na tiba
Mkojo ni mchanganyiko wa asilimia 95 za maji na asilimia tano za madini yanayotoka baada ya mmeng’enyo wa chakula kufanyika mwilini. Madini hayo ni pamoja na urea, chloride, sodiamu, potassiamu na chuma.
Baada ya kula na mmeng’enyo kufanyika, maji pamoja na mabaki yaliyomeng’enywa husafirishwa katika kibofu cha mkojo.
Maji hayo ndiyo husaidia kufanya usafirishaji wa mabaki hayo hadi katika kibofu cha mkojo.
Nchini India, kwa mfano tiba ya mkojo inaitwa ‘shivambu’.  Jina hilo likimaanisha ‘dawa ya hekima’  ambayo ilitangazwa zaidi na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Morarji Desai ambaye alidiriki kuutangazia umma kuwa anakunywa mkojo wake wa asubuhi kila siku na hiyo ndiyo siri ya afya njema na maisha marefu.
 Hata hivyo, inaelezwa kuwa mkojo una utajiri wa protini na madini mengine ambayo huweza kutumika katika matibabu na pia ni miongoni mwa vichanganyo katika dawa nyingi, kwa mfano dawa za ureacini, urecholin na urowave.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad