TAHARUKI: NANI ALIMTEKA DR ULIMBOKA?
0
August 08, 2013
USIKU wa kuamkia Juni 26, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa na kuteswa, kisha kutelekezwa katika Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Dk. Ulimboka alitekwa zikiwa ni siku tatu baada ya mgomo wa madaktari kuanza nchi nzima. Alikuwa na wenzake eneo la Leaders Club, Wilaya ya Kinondoni.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam liliunda kikosi kazi kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo ambalo Kamanda wake, Suleiman Kova, alijigamba kuwa halitajitokeza tena.
Hadi leo kikosi kazi hicho kilichoundwa na Kova hakikuwahi kutoa ripoti yake kwa umma kuwataja wahusika wa tukio hilo, badala yake jeshi hilo limekuwa na ndimi tofauti katika kulielezea.
Nani alimteka na kumtesa Dk. Ulimboka? Bila shaka majibu ya swali hili yanaweza kutolewa na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vyote vya dola kutokana na tukio hilo kulipaka matope taifa letu.
Kwa bahati mbaya hata vyombo vyetu vya dola vimeanza kutiliwa shaka. Wakati polisi wakitupiana mpira, Dk. Ulimboka alijitokeza kwenye vyombo vya habari na kumtaja mmoja wa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa akidai kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa.
Hakuna hatua zilizochukuliwa na polisi kuhusiana na madai hayo, ikiwa ni kumhoji mtuhumiwa wala Ofisi ya Rais Ikulu kumtaka mtajwa kukanusha tuhuma hizo.
Badala yake alikamatwa kijana mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi na kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa kuwa ndiye alimteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
Siku chache baadaye wakati polisi wakipigana danadana, serikali ililifungia gazeti la wiki la MwanaHalisi ambalo lilichapisha kwa undani taarifa za ofisa wa usalama aliyetajwa na Ulimboka, likidaiwa kuwa linachochea.
Ahadi ya Kova kuwasaka wahusika na kuwachukulia hatua ili kuhakikisha tukio hilo halijirudii tena imeshindikana kutekelezeka kwani usiku wa Machi 6, mwaka huu, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Absalom Kibanda, naye alitendewa unyama kama wa Dk. Ulimboka.
Kova aliunda kikosi kazi kingine kuchunguza tukio hilo lakini hadi leo hakuna ripoti iliyotolewa. Waliomteka na kumtesa Kibanda bado hawajulikani na siku zinazidi kwenda.
Katika kudhihirisha kuwa polisi walikurupuka na kumshtaki Mulundi ili kuwaziba wabunge midomo wasijadili suala hilo bungeni, juzi Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aliifuta kesi hiyo dhidi ya raia huyo wa Kenya.
Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likiwamo Jeshi la Polisi, wanalipwa mshahara kutokana na kodi za wananchi ili wafanye kazi zao kwa weledi na ufasaha, kwanini washindwe kuwabaini waliowateka na kuwatesa Dk. Ulimboka na Kibanda?
Kama wameshindwa kazi kuna haja gani ya wao kuendelea kuwapo kazini wakati wananchi wanaishi kwa hofu ya kutekwa, kunyofolewa kucha, meno, kutobolewa macho na kutupwa msituni?
Source:Tanzania Daima
Tags