Suala la Mrisho Ngasa kusajiliwa na timu mbili kutolewa uamuzi leo.
Dar es Salaam. Wakati leo Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikitarajia kulitolea uamuzi suala la Mrisho Ngasa, hofu imetawala kambi ya Yanga juu ya kitakachoamriwa na kamati hiyo.
Kwa zaidi ya wiki sasa, winga Ngasa ameviteka vyombo vya habari kutokana na jina lake kuonekana kwenye orodha ya usajili ya klabu za Simba na Yanga--kila upande ukidai kuwa ni mali yake.
Mabingwa Yanga wamemsajili Ngasa kutoka kwa wapinzani wao, Simba mara baada ya kumalizika msimu, ambapo kabla Wekundu hao wa Msimbazi walimsajili kwa mkopo winga huyo wa zamani Jangwani kutoka Azam FC.
Siku zote Ngasa amekuwa akisisitiza kuwa yeye ni mchezaji halali wa Yanga baada ya kumaliza kipindi chake cha kucheza kwa mkopo Simba, ambao wanaendele kubaki na msimamo kuwa ni mali yao.
Jana kwenye mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa Loyola, Dar es Salaam, suala la hatima ya Ngasa lilikuwa gumzo kubwa, huku pia viongozi wakikataa kusema lolote zaidi ya kusubiri uamuzi wa kamati.
Hofu hiyo ilikuja baada ya kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi wakati mazoezi yakiendelea kuwa, Kamati ya TFF imeamwidhinisha Ngasa kucheza Simba baada ya kuridhika na vielelezo vilivyoletwa na Wekundu hao wa Msimbazi.
Taarifa hizo ziliwashtua viongozi wa Yanga walikokuwa kwenye mazoezi ya timu hiyo na kuanza kupigiana simu ili kujua ukweli.
Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba wao wanachosubiri ni kile kitakachoamriwa na Kamati ya TFF.
“Sidhani kama kuna ukweli, lakini ngoja kwanza tusubiri hiyo kesho. Kwa sasa kila mtu anakuja na taarifa yake, sisi hatuwezi kuamini,” alisema Saleh. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusakao aliwataka viongozi wenzake kutulia na kuondokana na hofu kwa vile suala hilo bado halijatolewa uamuzi.