Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Hamis Tambwe amefunga mabao manne akiiongoza Simba kuisambaratisha Mgambo Shooting kwa mabao 6-0, huku Yanga wakilazimishwa sare 1-1 na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Wapinzani wao katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Azam wameendelea kusuasua baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Ashanti United, kama ilivyokuwa kwa Coastal Union dhidi ya Rhino Rangers 1-1. Vinara JKT Ruvu wamepokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting na kuondolewa kileleni na Simba.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji Tambwe aliweka rekodi katika Ligi Kuu ya Tanzania kwa kufunga mabao manne katika mchezo mmoja.
Mrundi huyo aliwainua mashabiki wa Simba katika dakika ya 4, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Issa Rashidi, ambapo baadaye winga Haruna Chanongo aliifungia Simba bao la pili kwa shuti la mguu wa kushoto akimalizia mpira ulioshindwa kuokolewa vizuri na mabeki wa Mgambo.
Tambwe aliipatia Simba bao la tatu katika dakika ya 41, akimalizia mpira uliomshinda kipa wa Mgambo, Manzi. Mrundi huyo pia alifunga bao la nne kwa Simba katika dakika ya 44 akimalizia vizuri krosi ya Amri Kiemba.
Naye Chanongo aliipatia Simba bao la tano baada ya kuwazidi kasi mabeki wa Mgambo katika dakika ya 64. Kama hiyo haitoshi, Tambwe alipachika bao la sita kwa Simba kwa mkwaju wa penalti baada ya Bashiru Chanache kushika mpira kwenye eneo la hatari.
Kwenye Uwanja wa Chamazi, mfungaji bora wa msimu uliopita, Kipre Tchetche alifunga bao lake la kwanza msimu huu wakati alipoifungia Azam bao la kuongoza katika dakika ya 21 akiunganisha kwa shuti kali kona iliyopigwa na Waziri Salum na kushindwa kuokolewa vizuri na mabeki wa Ashanti United.
Katika mechi hiyo, Azam walipata pigo baada ya beki wao Aggrey Morris kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Oden Mbaga baada ya mchezaji huyo kumkwatua kwa makusudi Hussen Sued wa Ashanti.
Katika dakika ya 79, Antony Matanga’alu alisawazishia Ashanti kwa mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Huko Mbeya, Utulivu mkubwa ulitawala kwenye Uwanja wa Sokoine, tofauti na ilivyokuwa Jumamosi iliyopita dhidi ya Mbeya City, wakati Prisons walipoikabili Yanga mbele ya mashabiki wachache. Prisons walianza kwa kasi na kukosa bao dakika 2, baada ya shuti la Ibrahimu Isaka kutoka nje kidogo ya goli, Yanga walijibu mapigo dakika ya 8, kupitia Didier Kavumbagu.
Mshambuliaji Jerryson Tegete aliifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika 42, akiunganisha krosi ya Simon Msuva. Kabla ya Peter Michael kuisawazishia Prisons katika dakika ya 76 akimalizia krosi ya Omega Seme.