MAKALA:TUKUBALI TU KUWA SOKA LETU BONGO LIMEKWAMA MAHALI-LAHITAJI MAOMBI

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, juzi ilimaliza kwa machungu kampeni ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil, baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Gambia.

Ingawa Stars ilishakosa tiketi ya kucheza hatua ya kumi bora tangu ilipofungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Morocco na Ivory Coast, iliwafuata Gambia wakihitaji ushindi ili kumaliza kampeni hizo wakiwa nafasi ya pili.

Wakati Stars inaondoka nchini, Kocha wake Kim Poulsen, alisema wazi wanahitaji pointi tatu ili kushika nafasi ya pili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya viwango vya timu katika upangaji wa timu kampeni za kimataifa zikiwemo fainali za Kombe la Mataifa Afrika za mwaka 2015.

Hata hivyo, Stars imeshindwa kupata ushindi kwa vibonde hao wa kundi la C, waliomaliza na pointi nne wakitanguliwa na vinara Ivory Coast (14) waliotinga raundi ya 10 bora, Morocco (9) na Tanzania (6).

Kwetu Tanzania Daima tumepokea matokeo hayo yasiyotarajiwa kwa masikitiko makubwa kiasi cha kuzua maswali mengi juu ya nini kifanyike ili Stars iweze kuwa na uwezo halisi kisoka badala ya kuwa na kiwango kinachopanda na kushuka kama homa ya vipindi.

Tunapaswa kujiuliza hivyo kwa kuzingatia kuwa kama matunzo na mahitaji muhimu, wachezaji hao chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tazania (TBL), wamekuwa wakipata matunzo mazuri pengine kuliko wakati wowote katika historia ya timu hiyo.

Tunajiuliza kama Stars inayopata matunzo ya kiwango hiki inapata matokeo mabaya hivi, nini kifanyike ili timu hiyo iweze kufanya vizuri kwenye kampeni mbalimbali za kimataifa kama fainali za Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia?

Inasikitisha kuona timu yetu ikizidi kupotea ikifungwa mechi tatu mfululizo za kimataifa wakianza kufunga na Morocco 2-1, Ivory Coast (4-2) kisha kufungwa 2-0 na Gambia iliyo nafasi ya 163 kwa ubora wa soka ulimwenguni.

Kama Stars inashindwa hata mbele ya timu dhaifu kama Gambia, tusitarajie miujiza ya kucheza fainali za Afrika chini ya mazingira haya kama hakutakuwa na hatua madhubuti za kuleta mabadiliko ya kusonga mbele.

Matokeo haya yanaonyesha wazi kumbe tatizo la Stars ni zaidi ya udhamini kwa maana uwekezaji kwenye programu za vijana mbinu ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa siri ya mafanikio ya mchezo huo kote duniani.

Tunasema bila kufanya uwezekezaji huo muhimu, hata udhamini wa mamilioni ambao umekuwa ukimwagwa kwa timu hiyo, utakuwa ni sawa na kazi bure kwa sababu mafanikio ya kweli ya mchezo huo yatabaki kuwa ndoto isiyotimia.

Uwekezaji tunaosema hapa ni kuanzia klabu za Ligi Kuu kuwa na timu hai za vijana tofauti na ilivyo sasa ambapo huwatafuta wa msimu pale wanapotakiwa kushiriki michuano ya Kombe la Uhai ambayo hushindanisha vikosi vya vijana wa chini ya miaka 20.

Kama klabu zote za Ligi Kuu zitakuwa na vikosi vya vijana na msisitizo ukiwekwa kwenye michuano mingine ya vijana kama Copa Coca Cola, mashindano ya shule za msingi kuanzia shule za msingi (Umitashumta) na sekondari (Umiseta) na Kombe la Taifa na mingineyo, mageuzi yataonekana.

Tunasema umefika wakati sasa wa kuchukua hatua stahiki ya kuondoka hapa tulipo kama kweli tunataka kuyafikia mafanikio ya kweli ya soka tofauti na ilivyo sasa ambapo kila kukicha ni heri ya jana, tuzinduke, tuchukue hatua kwa sababu jahazi linazidi kuzama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad