Imeandikwa tarehe 29 Septemba 2013 By Eric Anthony, Kigoma
KAMPENI ya kitaifa ya kuondoa wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina la Operesheni Kimbunga, imefanikiwa kusambaratisha kijiji cha wahamiaji haramu wa Burundi waliokuwa wamejitengenezea dola yao nchini, kiasi cha
hata kutumia sarafu ya Burundi ilihali wakiwa Tanzania.
Aidha, watoto wao wanasoma shule kwa mitaala ya Burundi, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kwa lugha ya Kifaransa wakiwa kijijini Nyamugali, Mvugwe wilayani Kasulu, Kigoma.
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Issa Machibya katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wakazi wa mkoani Kigoma, wakiwemo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya za Kasulu na Buhigwe, wamepongeza hatua hiyo.
Wameitaka serikali kutorudi nyuma katika kuhakikisha inawaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wametajwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi kutokana na kujihusisha na matukio ya ujangili, biashara ya silaha zikiwemo za kivita, na matukio mengine.
Akizungumza mjini hapa, Machibya alisema mbali ya kutumia faranga (fedha za Burundi) kwa matumizi yao ya kawaida wakiwa nchini na kufundisha kwa mitaala ya nchi waliyotoka, wahamiaji hao walipeperusha pia bendera ya nchi yao katika sehemu mbalimbali za kijiji hicho.
“Lakini kwa sasa, wote wamekimbia na kuziacha nyumba zao. Huwezi kuamini kama ni nyumba za wahamiaji haramu, kwani walijijenga na kuishi watakavyo, tena bila ya hofu katika nchi ya kigeni.
“Hebu tafakari, ni dharau gani unaishi Tanzania, lakini hata pesa yao hutumii, badala yake unatumia faranga.Tunashukuru tumewasambaratisha, na tutaendelea na operesheni hii mpaka tuhakikishe Watanzania
wanaishi kwa amani katika ardhi yao,” alisema Machibya.
Inakadiriwa kuwa, idadi ya wahamiaji haramu waliokuwa wanaishi kijijini hapo, lakini sasa wakiwa wamekimbia mkono mrefu wa Operesheni Kimbunga, ni zaidi ya 600.
Mkoa wa Kigoma pekee umenasa wahamiaji haramu 4,365 wa Burundi katika awamu ya kwanza ya operesheni hiyo iliyosambaa katika mikoa mbalimbali nchini, lakini Machibya amewataka Wana-Kigoma kushiriki kikamilifu
katika vita dhidi ya wahamiaji haramu hasa katika awamu hii ya pili na nyinginezo.
“Tatizo lililopo ni usiri. Wengi wameshindwa kutoa ushirikiano, na kufanya wengi tuishi nao kana kwamba ni Watanzania wenzetu… Watanzania waelewe hawa si watu wema, wangekuwa wema wangefuata taratibu za kuishi nchini, lakini wamekuwa wakiishi kwa ujanja ujanja mno. Mshona nguo za RC “Miongoni mwao ndimo walimo mawakala wa silaha za kivita, mabomu ya kurusha kwa mkono na biashara nyingine haramu.
Hatuwezi kukubaliana na hali hii,” alisema Machibya na kutoa mfano unaoendelea kumshangaza hata yeye mwenyewe kuwa, fundi maarufu aliyekuwa anashona nguo za baadhi ya Wakuu wa Mkoa wa Kigoma, akiwemo
yeye mwenyewe na mtangulizi wake, John Simbakalia ni mtuhumiwa wa uhamiaji haramu.
“Ndiyo, hata kabla yangu ndiye aliyekuwa anashona nguo za baadhi ya ma-RC (Wakuu wa Mkoa) hapa Kigoma, Simbakalia ni miongoni mwao na mimi mwenyewe amenishonea suti mbili…nikanogewa na kutaka kushona suti
nyingine, sasa nikiwa na kitambaa changu, kila nikipita nakuta ofisi zimefungwa, zaidi ya mara nne nimepita... kuuliza naambiwa ni wale wale, wameamua kujisalimisha kabla ya kunaswa.
“Sasa mambo haya yanatokea hapa mjini, si huyo tu, kuna wengi wanaendelea kusombwa…lakini kama Serikali ya mkoa, tunasema wawe hapa mjini au mahali popote pale, operesheni hii itawanasa na tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuunga mkono,” alisema.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu, Frederick Nisajile, alipongeza kazi nzuri inayofanywa na serikali, huku akishauri mianya mingine ya kuzalisha wahamiaji haramu au hata kugawa uraia kiholela kwa wakimbizi ifungwe kwa sababu za kiusalama.
“Kwa idadi hii ya wahamiaji na wakimbizi, usalama wa nchi uko hatarini. Kuna mengi ya kufanyiwa kazi ili kuhakikisha nchi haiingiliwi,” alisema Nisajile ambaye amefanya kazi na wakimbizi kwa takribani miongo miwili.
Mkazi mwingine wa mjini Kigoma, eneo la Burega ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutajwa jina, alisema,” Kigoma imevamiwa.
Mbaya zaidi watu wanafichiana siri, lakini wahamiaji ni wengi, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa. Nao wanaita ndugu zao na kuzidi kuijaza nchi yetu, wakiishi bila kufuata taratibu.
Naipongeza serikali kwa kuanza kukabiliana na wimbi hili la wahamiaji haramu.” Naye Kiongozi wa Timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa, akizungumza kwa njia ya simu kutoka
Biharamulo, Kagera alisema anafarijika kuona operesheni inang’ata kila sehemu, huku akiahidi kutoa taarifa ya utekelezaji wa awamu ya pili ya operesheni inayoendelea kote nchini.
Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo ujambazi wa kutumia silaha, ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafugaji kutoka nchi jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho.
Ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa Julai 29, 2013 akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera, akitaka kufanyika kwa operesheni maalumu ya kuondoa uhalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na
Geita ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew Sukambi ilianza Septemba 6, 2013, baada ya kupita wiki mbili alizokuwa amezitoa Rais Kikwete kwa kuwataka wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari yao au kuhalalisha ukazi wao nchini.
source; HabariLeo
hii ya wahamiaji haramu isiwe tu kwa waafrika tu hata wazungu wachina na wengineo wengi wanafanya kazi hapa nchini bila vibali hasa wafanyi biashara ukienda mahotelini uakuta wahindi wengi hawana vibali nao pia fagio liwapitie
ReplyDeleteUmenena cha ajabu,wanawaogopa ngozi nyeupe kama nin wamekamata wamalawi,tu
DeleteMsiseme ivyo kuwa wafrica wanaonewa tatizo letu sisi wafrica atuheshimu fadhila ebu agalia watu wanaanzisha serikari yao nchi ambayo cio yakwao ,watu wanafanya biashara haramu siraha za kivita ,wanapola mali za watanzania kinguvu.
ReplyDeleteAsante,Tanzania ,mnaweza kutumia vijana wenu walioko nje wanaokuja nyumbani kila mwaka ,kutambua wageni haramu ,ni ngumu ,kwa vyombo au askari wetu kuwa jua wote ila watanzania ,wakishirikishwa walioko nje ,wanajua vichochoro vingi sana ,na msiogope wenye hela hata hizi nchi za watu tunafuata sheria ,na nikali sana,bado tunajeshi kubwa sana ,pia msiruhusu wageni katika majengo ya kijeshi ,hata km ni mainjinea au wajenzi ktk ,majeshi yetu,hata km wanaongea kiswahili ,na watafiti wanaoingia maporini na kwenye madini masaa 24 wawekwe kwenye ulinzi isije kuwa kama ile issue ya ya lake natron ya 1995-1997,,wananchi wawe wazalendo.
ReplyDeletewanafunzi hata washule za msingi wafundishwe kujihami,na kuipenda nchi yao,watu waelimishwe jinsi bongo ilivyo nzuri,na tuilinde,kwa ngarama zote,wengi wanaitamani sana bongo tuwe makini sana,na tumwombe Mungu atusaidie sana ,kufikia malengo ,ya kutoka kwenye ,mahitaji yetu ya kila siku,tuwe wazalendo.
ReplyDelete