SADC YAMUONYA KAGAME KUHUSU PLAN ZAKE ZA KUIVAMIA TANZANIA

MZOZO wa kidiplomasia alioibua Rais wa Rwanda, Paul Kagame kwa Rais Jakaya Kikwete, sasa unaonekana kuchukua mwelekeo mpya, baada ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kumuonya kiongozi huyo kuacha mara moja fikra zozote mbaya dhidi ya Tanzania, MTANZANIA Jumatano limedokezwa. 


Habari za uhakika na za kuaminika kutoka miongoni mwa viongozi wa juu wa SADC na maofisa wa Serikali, waliokuwa katika ujumbe wa Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa akihudhuria Mkutano wa viongozi wa Maziwa Makuu huko Uganda hivi karibuni, zinaeleza kuwa tayari Jumuiya hiyo imekwisha mpatia ujumbe huo mmoja wa mawaziri aliyekuwa ameandamana na Kagame muda mfupi baada ya kikao chake na Kikwete.

Taarifa ambazo MTANZANIA Jumatano imezinasa, zinaeleza kuwa, kiongozi mmoja wa juu wa Msumbiji ambaye alikuwa pia Uganda, alikaririwa akimueleza Waziri huyo wa Kagame kuacha kabisa fikra za kuishambulia Tanzania, kwa sababu ya uamuzi wake wa kupeleka vikosi vyake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC. 

“Uamuzi wa Tanzania na Afrika Kusini kupeleka majeshi DRC, ni msimamo wa pamoja wa SADC. Vitisho vyovyote dhidi ya Tanzania au uvamizi wa kijeshi, utachukuliwa ni uvamizi dhidi ya SADC, hivyo tutakuwa tayari kuingia vitani kupigana upande wa Tanzania,” alikaririwa akisema ofisa huyo wa juu wa Msumbiji.

Inaelezwa kuwa, SADC imetoa msimamo huo baada ya kubaini kuwa hasira ya sasa ya Kagame dhidi ya Rais Kikwete, msingi wake unatokana na hatua ya Tanzania kupeleka vikosi vyake nchini Kongo kwenda kupambana na vikundi vya waasi vikiwemo vile vinavyodaiwa kuwa na ushirika na majeshi ya Rwanda.

Taarifa hizi zinathibitishwa na habari ambazo gazeti hili ilizinasa jana kupitia gazeti la The Namibian la nchini Namibia, ambalo liliandika kuwa Jeshi la nchi hiyo (NDF), ambalo linaunda kikosi maalumu cha SADC, lilikuwa limeanza kushiriki mazoezi huko Jangwani karibu na Walvis Bay. Mazoezi hayo yatadumu hadi Oktoba 15 mwaka huu.

Inaelezwa kuwa wakati mazoezi hayo yakiendelea, Mkuu wa majeshi ya Namibia (NDF), Luteni Jenerali, Epafras Ndaitwah aliwakumbusha washiriki hao kuwa kwa sasa wanachama wenzao kama Wanajeshi wa Tanzania na Namibia, wanapambana na maadui wa amani Kongo na kwamba lazima wajiandae kwa hali yoyote ambayo haitabiriki.

Hatua hiyo ya sasa ya SADC, na sifa ambazo imepata kummwagia Rais Kikwete kwa namna alivyosimamia mizozo wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, inaonyesha wazi jinsi Jumuiya hiyo ilivyotayari kuwa upande wa kiongozi huyo.

Kutokana na hilo, baadhi ya wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wanasema kuwa si ajabu basi Kagame na Serikali yake wakawa wanafahamu msimamo huo wa SADC, ambao haujawekwa hadharani hasa kwa kuzingatia uamuzi wake wa kuungana na Uganda na Kenya katika usharika wao wa hivi karibuni.

Pia hatua ya nchi yake kusaini mkataba wa kiusalama na nchi nyingine tano wa kusaidiana kijeshi endapo mmoja wao atavamiwa na nchi nyingine, imeelezwa kuwa na mwelekeo huo huo wa Kagame kuanza kujihami.

Nchi ambazo zimeingia mkataba huo na Rwanda ni pamoja na Ethiopia, Kenya, Uganda na Sudan Kusini. 

Hata hivyo wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo, wamekosoa muungano huo wa kusaidiana kijeshi na Rwanda, wakidai kuwa ni wa mashaka ukilinganisha na ule unaounda SADC ambao unajengwa na matendo ya kihistoria.

Wameitolea mfano Ethiopia, kwamba ni rahisi kuasi kutokana na mfumo wake wa kijeshi unaoongozwa kwa mkono wa chuma, huku wanajeshi wake wakiwa katika hali mbaya ya kiuchumi.

Wameulinganisha mfano huo na nchi moja tu ya Zimbambwe ambayo inaunda SADC kwamba, pamoja na matatizo yote ya migogoro ya kisiasa na kidiplomasia inayoyakabili, lakini jeshi lake lipo imara na linatunzwa vizuri.

Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo huo, hatua ya sasa ya SADC imekuja wakati ambapo tayari Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliwahi kuionya Rwanda akisema kuwa endapo nchi hiyo itajaribu kuigusa Tanzania, atakuwa tayari hata peke yake kupeleka jeshi lake kupambana nchini humo.

Nje ya SADC, nchi zinazounda Jumuiya hiyo kama Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na Angola zinaguswa moja kwa moja na hisia za Tanzania, kutokana na historia yake ya kushiriki kwenye ukombozi na uhuru wa nchi hizo.

Kutokana na hilo, wachambuzi hao wanasema kuwa si rahisi kwa wao kukaa kando pale watakapoona maslahi ya Tanzania yanachezewa, hasa linapokuja suala la kuichokoza.

Taarifa hizo za SADC zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kuinyooshea kidole cha lawama Rwanda, kitendo hicho kinaonekana kuungwa mkono kwa kasi na makundi mengine ya kimataifa.

Kagame ambaye kwa miaka mingi amekuwa kiongozi kipenzi cha mataifa mengi tangu alipofanikiwa kumaliza mapigano yaliyosababisha mauaji ya halaiki nchini kwake mwaka 1994, katika siku za hivi karibuni taswira yake inaonekana kubadilika na kuchukua mwelekeo wa uadui zaidi kuliko urafiki.

Hilo linatokana na kile kinachodaiwa kuwa Serikali yake imekuwa ikihusika kuwasaidia waasi wa kundi la M23, wanaoendesha mapambano dhidi ya majeshi ya Serikali ya Kongo, jambo linalopingwa na Jumuiya ya Kimataifa pia wanatuhumiwa kwa ubakaji na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Tuhuma hizo ndizo ambazo zinamuweka Rais Kagame katika hatari na wingu la mashaka kwa sasa, hasa baada ya uhusiano wake na Tanzania kupita katika wakati mgumu kutokana na kuingia kwenye mgogoro na Rais Kikwete ambaye alimshauri kukaa meza moja ya mazungumzo na waasi wa FDLR.

-Mtanzania
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hizi ni habari za kupika kwa nini hazipo BBC?, yaani nyie waandishi wa habari mchwara ni wachonganishi sana.Mnachochea mambo tu ili kueneza ugomvi,vita ikitokea hata familia zenu zitaathirika pia. shame on you

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad