SIMU YAKO YA MKONONI ISIWE KERO KWA WENZIO

SIMU za mkononi ni muhimu katika maisha yetu, kwa sababu ni kiunganishi cha mawasiliano ya wanadamu walio maeneo tofauti.

Matumizi ya simu yana faida nyingi katika maisha ya sasa, hasa upande wa kiuchumi na kuwaweka watu karibu duniani kote.

Lakini mbali na faida, lengo la kuandika mtazamo huu ni kuhusu wale watumiaji wa simu hizi za mkononi ambao hawajua matumizi yake sahihi.

Wako watu ambao hujisikia kama burudani au sifa wanapokuwa wanazungumza na simu, tena kwa muda mrefu. Wakati mwingine hujionesha kwa watu walioko karibu nao kwa namna wanavyojua kutumia simu.

Kwa mtazamo wangu, usiyafanye matumizi ya simu kuwa starehe au maonesho kwa watu, kumbuka bila kujijua maneno yako wakati mwingine yanaweza kuwa si mazuri kwenye masikio ya watu, jaribu kutumia simu yako kwa faida yako.

Usiwe kikwazo kwa namna yoyote, hasa sehemu za huduma za kijamii, kwa sababu siku hizi hata heshima kwa watu wanaotakiwa kuhudumiwa imepungua, kwani kuna baadhi ya wahudumu na hata wakurugenzi wa ofisi mbalimbali hujisahau kuhudumia wateja wao linapokuja suala la kuzungumza na simu.

Kwa mfano, katika zahanati au hospitali wahuduma wengi hujikuta wakizungumza na simu badala ya kuhudumia wagonjwa.

Hilo hutokea baada ya kupigiwa simu au kupiga simu na kuanza maongezi, tena ya muda mrefu, huku wakisubiriwa, ukiyasikiliza maongezi yao yanakuwa si ya heshima, hayafai hata kusikilizwa kwani hayana maadili mazuri, nyingine ni ahadi za mapenzi na ulevi.

Wanazungumza maneno yasiyofaa kwa jamii inayowazunguka, ila kwa kuwa una shida au mgonjwa, huna la kufanya, ni lazima kuyasikiliza, ukitoka utawahiwa na wenzako, hii ni kwa watu wa jinsia zote, iwe wanawake au wanaume, hasa vijana.

Hizi simu ndizo zinazovunja hata ndoa kwa wanandoa, kupoteza maadili mema na hata kuondoa ufanisi wa kazi maofisini, hivyo kufanya uchumi wa baadhi ya miradi kushuka na kuharibu uchumi wa taifa.

Mwandishi wa kitabu cha ‘Madhara na Faida ya Simu ya Mkononi’, Sweetbirth Bruno, anasema: “Licha ya kero kwa wengine imefahamika kwamba baadhi ya watoto wa shule za msingi na sekondari hushindwa kufanya vizuri wawapo shuleni, hilo ni pamoja na kukesha usiku kucha waki ‘chati’ na simu, tena wakizungumzia maneno ambayo hayana msingi na kusababisha kuvuruga ufahamu wao na kupoteza uwezo wa kusoma, hatimaye kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata alama za daraja la nne au sifuri na kuongeza idadi ya wajinga nchini.”

Rai yangu kwa idara na taasisi zinazojihusisha na masuala ya elimu, ni kuliangalia hilo, kwa sababu matumizi haya ya simu kwa wanafunzi yamezidi hadi kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho, hasa kidato cha nne na sita.

Nawashauri wanafunzi kuachana na matumizi ya simu na waweke bidii katika masomo yao kwa sababu wanaweza kujisababishia kushuka kimasomo na kulisababishia taifa kukosa wasomi, chanzo kikiwa ni matumizi mabaya ya simu kama kuingia kwenye mitandao mbalimbali ya anasa badala ya kusoma masomo ya darasani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad