SIMULIZI MBALI MBALI ZA KUTISHA KUTOKA MAUJI YA WESTGATE NAIROBI


MJAMZITO wa miezi nane na nusu ni miongoni mwa mateka waliouawa katika uvamizi wa kituo cha biashara cha Westgate jijini Nairobi Jumamosi, imefahamika.

Elif Yavuz ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Havard, Marekani aliuawa pamoja na mumewe Ross Langdon (33) ambaye ni msanifu majengo mwenye uraia pacha wa Uingereza na Australia.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka eneo la tukio zilisema Langdon ameshiriki miradi mbalimbali barani Afrika, ikiwamo inayohusika na ujenzi upya wa hospitali ya Ukimwi nchini Kenya bila malipo yoyote.

Elif ambaye alikuwa akitarajiwa kujifungua wiki mbili zijazo, aliuawa sambamba na mumewe huyo ambaye alipata kuwa mshindi wa tuzo ya ujenzi.

Langdon alipata mafunzo ya ujenzi katika Chuo Kikuu cha Tasmania kisha Chuo Kikuu cha Sydney, na kufanya kazi katika kampuni kadhaa kabla ya kuanzisha Kampuni yake ya Regional Associates Ltd, Mei 2008.

Akizaliwa na kukulia Kusini Mashariki mwa Tasmania, miongoni mwa miradi aliyoshiriki iko Uganda, Rwanda na Tanzania.

Alikuwa mtaalamu wa masuala ya malaria akifanya kazi Kenya katika Wakfu wa Bill, Hillary and Chelsea, ulioanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, Yafuz pia alipata kufanya kazi na Wakfu wa Bill and Melinda Gates unaoendeshwa na bilionea muasisi wa Microsoft, Bill Gates.

Akizaliwa Uholanzi, Yavuz ameishi Cambridge, Massachusetts, wakati akisoma Chuo Kikuu maarufu duniani cha Havard. Esther Waters-Crane, mtaalamu wa Uingereza ambaye anamfahamu vizuri Elif, alielezea masikitiko yake kwa kumpoteza mama huyo mtarajiwa na jinsi Kenya ilivyoshughulikia shambulizi hilo lisilo na sababu.

Alisema: “Namsikitikia sana Elif. Tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara juu ya kujifungua kwake akiwa Nairobi na nahisi kuugulia, hasira na mshituko kwa janga hili, janga la kupoteza wapendwa wetu. “Niko nyumbani na milipuko ya Westgate inarindima, inatoa sauti kama iko katika barabara yangu hapa nje. Tumesambaratishwa na hili – ni muda wa huzuni kubwa Nairobi na kwa nchi pendwa Kenya.”

Mama wa Langdon, Linden alisema hasara iliyosababishwa na kifo cha mwanawe huyo haipimiki. Familia yake imeomba faragha wakati huu ikiomboleza kifo chake, cha mwenza wake na mtoto wa tumboni - lakini mama yake aliamua kutoa maneno machache kupitia mitandao ya kijamii kuuambia ulimwengu kuhusu huzuni ambayo ndugu zake wanayo.

“Tumepoteza mwanangu mzuri Ross, mwenza wake mpendwa, Elif na mtoto wao mpendwa wiki mbili tu kabla ya kuzaliwa,” Linden aliandika katika ukurasa wake wa Facebook. “Hasara hii haipimiki, inaumiza.”

Machinjio

Katika hatua ya kusikitisha mmoja wa walinzi wa usalama dukani hapo alisema siku hiyo aliona ghafla duka linageuka machinjio katika kipindi cha nusu saa, kutokana na magaidi hao kuua watu ovyoovyo.

Wanamgambo hao walichoma moto nyuso za mateka wao na kuwanyofoa mikono kwa lengo la kupoteza utambulisho na miili yao kurundikwa katika lango kuu ili kupunguza kasi ya mchakato wa uokoaji.

Taarifa zilizotolewa juzi kupitia mitandao zilisema mwanamke majeruhi aliyekwama ndani ya duka hilo chini ya watekaji alidhalilishwa kijinsia mbele ya mtutu wa bunduki na mbele ya mateka vijana kwa kubakwa na magaidi hao. Inadaiwa mwanamnke huyo alipigwa risasi begani huku mwanawe akiuawa katika uvamizi huo.

Inasemekana mama huyo aliwasiliana na mumewe mara nyingi nje ya kituo hicho cha biashara – lakini usiku wa juzi mumewe hakupata tena mawasiliano ya mkewe.

Shindano

Shuhuda mwingine, Kamille Kaur, alikuwa na watoto wengi wakishiriki shindano la upishi katika duka hilo lililokuwa likifanyika katika ghorofa ya pili wakati shambulizi linatokea.

Mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 12 na bintiye wa miaka minane, walijeruhiwa kwa risasi. Alisema watu wazima “waligeuka kama wanyama, wakikanyaga watoto katika juhudi za kujiokoa.”

Twitter ya kikundi cha al Shabaab, ambacho kimedai kuhusika na shambulizi hilo, ilisema washiriki wanatoka mataifa saba, yakiwamo ya Uingereza, Marekani na Canada.

Kikundi hicho hivi karibuni kiligawanyika katika vikundi viwili kutokana na mapigano makali baina yao. Wasiohusika na uvamizi wa Nairobi wanadaiwa kueneza taarifa potofu zinazozua maswali juu ya ukweli wa taarifa za awali kwamba wakazi wa London, Ahmed Nasir Shirdoon (24) na Liban Adam (23) ni miongoni mwa magaidi hao.

Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi, alisema wapiganaji kutoka nchi mbalimbali wamehusika katika mashambulizi hayo, lakini hakutaka kuzitaja nchi hizo.

“Tuna fununu za ni akina nani, uraia wao na hata idadi yao pia,” alisema na kuongeza kwamba wanamgambo hao ni mkusanyiko wa raia wa mataifa mbalimbali duniani…tuna fununu pia kwamba hili si tukio la ndani,” alisema na kuongeza: “ Hapa tunapambana na ugaidi wa kimataifa na tuna uhakika na tunachokisema.”

Wakenya juzi usiku walikuwa wanahofia kutokea mashambulizi mengine ya kigaidi baada ya kutokea madai kuwa wengi wa wanamgambo hao wanatoka katika kikundi hicho cha al Shabaab ambao waliingia nchini baada ya kuhonga wahusika.

Msemaji wa al Shabaab alisema Waingereza wote walioko Kenya ni ‘walengwa’ wao kwa sababu Uingereza inasaidia nchi hiyo kuingilia kijeshi Somalia.

Juzi Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alirejea nyumbani mapema akitoka Balmoral, ambako alikuwa na Malkia, ili kuongoza kikao cha dharura cha ulinzi na Baraza la Mawaziri akiwamo Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg, Chansela George Osborne na Waziri wa Ulinzi, Philip Hammond.

Waislamu wauawa

Baba Mwingereza wa binti wa umri wa miaka minane juzi alisimulia kwa huzuni kubwa jinsi alivyopata taarifa za bintiye huyo Mwislamu na mkewe kuuawa na magaidi hao.

Louis Bawa (43), alisema bintiye huyo, Jennah na mkewe mzaliwa wa Kenya Zahira (41), waliuawa Jumamosi na ‘wanyama’ ambao walikuwa wakitumia “dini kama kisingizio cha kuua watu.”

Waziri Mkuu Cameron alisema inaonekana miongoni mwa waliouawa takribani sita ni raia wa Uingereza. Bawa, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni moja ya Masoko aliiambia The Daily Telegraph, kwamba: “Watu waliofanya haya, ni wanyama…mwisho wa siku wanatumia dini kama kisingizio cha kuua watu.

Wanasema wanalenga watu fulani, lakini wanalenga mtu yeyote. Zahira na Jennah walikuwa Waislamu! “Lakini wanyama hawa waliwaua kama walivyofanya kwa wengine.

Awali nilishawishika kwamba wangekuwa salama. Nilikuwa na matumaini…. Hivi sasa naomba haki itendeke kwa wanyama hawa waliotenda haya.” Bibi wa Jennah, Shakuntna Bawa (63) juzi alisema familia yake imesikitishwa na kukatishwa tamaa na janga la Nairobi, akiwambia waandishi wa habari :”Tulishajua kuwa wamepotea. “Lakini tukasikia baadaye kwamba kwa bahati mbaya wameuawa.

Nimeshituka sana – familia yote iko kwenye mshituko. Kwa sasa siwezi kusema lolote. Inasikitisha – lakini tutafanyaje?” Aliongeza: “Dada yangu alimwona Louis akizungumza kwenye televisheni na kunipigia simu.

Wakati huo tulikuwa bado tukiamini kuwapo fursa nyingine ya Jennah na Zahira kuwa salama, kwa sababu watu wengi walikuwa wamepotea. “Lakini polisi wamethibitisha kwa Louis kwamba mkewe na bintiye wameuawa.

Alijaribu kwenda mochari kutambua miili yao, lakini kulikuwa na walinzi pale. Hata hivyo, baada ya saa kadhaa aliruhusiwa kuingia na kuthibitisha wamekufa. Sijamwona Jennah kwa miaka mitano tangu familia hiyo ilipohamia Nairobi… alikuwa mrembo.”

Wanne wa familia moja

Wakati huo huo, mfanyabiashara wa Uingereza alitangaza kuuawa kwa watu wanne wa familia yake katika shambulizi hilo. Samir Bharma, wa Spinney Hills, Leicester, alikuwa juzi akikamilisha maandalizi ya safari ya kwenda Nairobi.

Ndugu zake hao walikuwa Nairobi kurekodi kipindi cha televisheni kinachojulikana kama Masterchef Junior. Alisema: “Walikuwa vijana wakishiriki shindano la mapishi ambalo lilikuwa linafanyika katika kituo hicho. Bahati mbaya wote wameaga dunia. “Shangazi naye yuko mahututi hospitalini. Nimezungumza na baba ambaye yuko huko, lakini mawasiliano ni magumu. Ni wakati mgumu sana na napanga safari sasa.”

Mkazi mwingine wa Leicester alielezea jinsi wazazi, kaka na dada yake walivyokuwa dukani hapo wakati magaidi wakishambulia. Mtu huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye hakutaka kutajwa jina baada ya mama yake kumwambia kwamba magaidi wameingilia mawasiliano ya Facebook yake na wakimwonya kuwa “tunakufuatilia”.

Alisema mama yake alimpigia simu: “Alikuwa ghorofani juu wakati mambo yote yakifanyika ghorofa ya chini ndipo alipoona magaidi hao wakizungukazunguka kila mahali na kufyatulia watu risasi. Aliona rafiki yake akipigwa risasi kichwani. “Dada yangu alichanganyikiwa. Kaka yangu alimvuta nje hadi eneo la maegesho ya magari…wakati huo eneo hilo lilikuwa salama na watu waliweza kuondoka.

Kaka yangu aliona mwili wa rafiki yake nje. Ulikuwa umepigwa risasi.” Mtu huyo alisema wazazi wake walikwenda hospitalini hapo kusaidia wafanyakazi kuhudunia majeruhi.

Mtoto jasiri

Mtoto wa miaka minne Mwingereza Elliot Prior kutoka Windsor, Berkshire, alionesha ujasiri wa aina yake kwa kumkabili gaidi ambaye aliishia kumwomba radhi.

Elliot alimwambia gaidi huyo kwamba ‘ni mtu mbaya sana’ wakati akimzuia kumshambulia mama yake, Amber, ambaye tayari alishajeruhiwa mguuni na dada yake Amelie.

Kama muujiza, gaidi huyo alijisikia huruma kwa familia hiyo na kuwapa watoto hao biskuti kabla ya kuwambia: “Tafadhali nisamehe, sisi si majinamizi.”

Askari shujaa

Askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza ambaye hakuwa zamu siku ya tukio la utekaji nyara wa kituo cha biashara cha Westgate, Nairobi Jumamosi iliyopita aliibuka shujaa kwa kuokoa maisha ya watu 100 siku ya tukio.

Mwanajeshi huyo siku hiyo alikuwa akipata kahawa katika moja ya migahawa ya Westgate wakati magaidi walipovamia. Shujaa huyo anadaiwa kurudi dukani humo mara 12, kuokoa watu licha ya mashambulizi ya bunduki yaliyokuwa yakiendelea.

Shuhuda mmoja alisema: “Alichokifanya ni cha kishujaa. Alikuwa akinywa kahawa na marafiki zake wakati tukio hilo linatokea. Alirudi ndani mara 12 na kuokoa watu 100. Fikiria kurudi ndani huku ukijua kilichokuwa kikiendelea humo.”

Vyanzo vya habari vilisema askari huyo wa SAS hawezi kutajwa kutokana na sababu za kiusalama. Vikosi maalumu vya Uingereza vimekuwa kwa kawaida vikitoa mafunzo na kuendesha shughuli zao nje ya Kenya, na vimekuwa vikishirikishwa katika kufuatilia raia wa Uingereza walio katika hatari ya kushambuliwa na Waislamu hao wenye misimamo mikali Somalia na Yemen.

Baadhi ya waliokuwa katika vikosi hivyo zamani, wamekuwa wakitumika katika serikali za Uingereza na Kenya kwenye kampuni mbalimbali za usalama na ulinzi katika Afrika Mashariki.

Mashuhuda walieleza jinsi magaidi hao walioficha sura zao kwa skafu zenye maandishi ya Korani walivyoingia jengoni humo, wakirusha mabomu na kumiminia risasi wateja kwa bunduki aina ya AK-47.

Juzi picha katika mitandao ziliwaonesha wakiingia kwenye duka hilo huku wakiwanyooshea silaha wateja waliokuwa wamejawa na hofu.

Wauaji hao ambao walivalia kimagharibi, walisikika wakiamuru Waislamu kuondoka, kabla ya kuwauliza maswali kibabe, kuona kama mateka hao wanaweza kukariri vifungu vya Korani na kutaja jina la Mama wa Mtume Muhammad.

Maarufu walioshambuliwa Uingereza/Australia

Ross Langdon alikuwa msanifu majengo aliyefanya kazi Uganda, Rwanda na Tanzania, akijenga majengo katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya utalii.

Uholanzi

Mwenza wa Langdon, Elif Yavuz (33), alikuwa akitarajia kupata mtoto wa kwanza mapema mwezi ujao. Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Havard Idara ya Afya mwaka huu, alifanya na kukamilisha tasnifu yale juu ya malaria katika Afrika Mashariki na alikuwa akifanya kazi na Mpango wa Afya Bora wa Clinton.

Peru

Juan Ortiz-Iruri alikuwa mtaalamu mstaafu wa magonjwa ya kitropiki katika UNICEF ambaye ameishi miaka 25 Afrika, kwa mujibu wa UNICEF na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Peru, Alejandro Neyra.

Mwanawe Ricardo Ortiz aliiambia Radio RPP kwamba aliingia dukani humo akifuatana na bintiye wa miaka 13 aliyezaliwa Marekani. “Maelezo kutoka kwa dada yangu ni kwamba baba alianguka sakafuni na hakujitikisa tena,” Ortiz alisema.

Alisema dada yake alijeruhiwa mkono, lakini hali yake si mbaya. Ortiz-Iruri amefanya kazi Kenya, Malawi, Zimbabwe na Liberia.

Ghana

Kofi Awoonor, mshairi wa Ghana, Profesa na Balozi wa zamani nchini Brazil, Cuba na Umoja wa Mataifa, alikufa kutokana na majeraha aliyopata, Ofisi ya Rais ya Ghana ilithibitisha.

Wizara ya Habari ya Ghana ilisema mwanawe wa kiume alijeruhiwa na anatibiwa. Kazi ya Awoonor ilivutia kutokana na vionjo vya utamaduni wa kabila lake la Ewe.

Kenya

Mpwa wa Rais Uhuru Kenyatta, Mbugua na mchumba wake, nao ni miongoni mwa waliouawa.

India

Raia wawili wa India, Parmashu Jain (8) na Sridhar Natarajan (40), waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema.

Canada

Wakanada wawili, akiwamo mwanadiplomasia, waliuawa kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Stephen Harper. Alituma salamu za pole kwa waathirika na kusema ni hasara kutokana na kifo cha Annemarie Desloges, ambaye alipata kutumika katika Ubalozi wa Canada nchini Kenya.

Mumewe, Robert Munk alijeruhiwa, lakini ameruhusiwa kutoka hospitalini, vyombo vya habari vya Canada vimeripoti.

Uswisi

Serikali ya Uswisi ilithibitisha kwamba mmoja wa raia wake alijeruhiwa. Ilisema ubalozi wake jijini Nairobi unawasiliana na familia ya majeruhi huyo na maofisa wa Serikali, lakini haukutaja jina lake.

Uingereza

Takribani raia wanne wa Uingereza waliuawa, kwa mujibu wa Ofisi ya Mambo ya Nje, ambayo ilionya kwamba idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

Ufaransa

Wanawake wawili wa Ufaransa waliuawa, Rais Francois Hollande alisema.

Afrika Kusini

Raia wa Afrika Kusini aliuawa, kwa mujibu wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa.

China

Mwanamke raia wa China mwenye umri wa miaka 38 mwenye jina la ubini la Zhou ambaye alikuwa akifanya kazi katika tasnia ya milki majengo aliuawa, Shirika la habari la Xinhua liliripoti.

Mwanawe wa kiume alijeruhiwa na anaendelea na matibabu hospitalini, kwa mujibu wa Ubalozi wa China nchini Kenya. Marekani Wamarekani watano walijeruhiwa kwa mujibu wa maofisa wa Serikali ya Marekani.

New Zealand

Raia wa New Zealand, Andrew McLeran (34) ambaye alikuwa akisimamia kiwanda cha kutengeneza mafuta ya avocado – Olivado nchini Kenya, alijeruhiwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya New Zealand ilithibitisha. Amelazwa na anaendelea vizuri.

Tanzania

Raia wa Tanzania Vedastus Nsanzugwanko alijeruhiwa miguu na amelazwa Aga Khan, Nairobi na hali yake inaendelea vizuri kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda Burian.

Korea Kusini

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini ilisema mwanamke raia wa nchi hiyo ni miongoni mwa waliouawa hata hivyo haikufafanua.

Wasiojulikana uraia

Ruhila Adatia-Sood, ambaye mumewe alikuwa mfanyakazi wa kigeni wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani akiishi Nairobi aliuawa, shirika hilo lilisema katika taarifa yake. Alikuwa mfanyakazi mashuhuri wa redio na televisheni nchini Kenya.

Hali halisi jana

Jana vikosi vya Kenya vilionekana vikitegua mabomu yaliyotegwa na wapiganaji hao wa Kiislamu ndani ya duka hilo ambapo watekaji nyara waliendelea kudai kushikilia mateka, Polisi ya Kenya ilisema jana.

“Tunaondoa milipuko ambayo imetegwa na magaidi,” Jeshi la Polisi lilisema kupitia mtandao wa Twitter. Hata hivyo, hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu ukubwa wa milipuko hiyo.

Jana asubuhi milio ya bunduki na milipuko mingine iliendelea kusikika, ambapo pia sehemu ya paa la duka hilo iliporomoka wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa ofisa wa Zimamoto.

Watu 68 ndiyo bado idadi ya watu waliopoteza maisha na 175 kujeruhiwa katika shambulio hilo kwa mujibu wa Serikali, ingawa kuna hofu ya idadi kuongezeka, huku al Shabaab ikitamba kuwapo “idadi kubwa ya miili ambayo bado haijaondolewa ndani ya duka hilo.”

Wanajeshi watatu wa Kenya nao wamepoteza maisha kutokana na majeraha waliyopata katika shambulizi hilo. Al Shabaab ilisema wapiganaji wake bado wanadhibiti kituo hicho na mateka wanaowashikilia bado wako hai.

“Kuna idadi isiyohesabika ya miili iliyotapakaa ndani ya duka hilo, na mujahidina (wapiganaji) wanadhibiti eneo lao (Westgate),” ilisema kupitia Twitter yake. “Mateka ambao wanashikiliwa na mujahidina ndani ya duka wako hai, wamechanganyikiwa sana, lakini wako hai.”

Baadaye ilidai kuwa mateka wote wamevishwa mabomu yanayoweza kulipuliwa kwa rimoti. Hadi jana jioni Serikali ilitangaza kuua magaidi saba, ingawa haikutoa ufafanuzi.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad