Serikali ya Tanzania, imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuruhusu Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto kutohudhuria baadhi ya mashauri ya kesi yake ili kuweza kutimiza majukumu mengine ya kiserikali.
Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Fredrick Mwita aliandika barua kwenda ICC Jumatatu wiki hii akitetea hoja ya Ruto kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo.
Katika barua yake, Jaji Werema alisema kuruhusu Ruto kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi kutaimarisha ushirikiano baina ya ICC na washirika.
Hata hivyo, maombi hayo yanayotaka Ruto kuruhusiwa kutohudhuria kesi hiyo binafsi yamesimamishwa baada ya mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda kuyawekea pingamizi na sasa yanasubiri uamuzi wa majaji.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania, kuwasiliana na ICC kwani iliwahi kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo ya kina Ruto isikilizwe Tanzania au Kenya.
Hata hivyo, mpango huo ulikwama baada ya majaji kuupinga kwa kura za hapana.
Mwandishi Sang ajitetea
Mwandishi wa habari wa kituo cha KASS FM Joshua Arap Sang, amekamilisha ungwe ya kwanza ya utetezi wake kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kueleza kuwa hakuhusika kwa namna yoyote kuchochea machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi nchini Kenya.
Sang aliwasilisha utetezi wake katika hali ya kujiamini huku akionyesha sura yenye matumaini na kuiambia mahakama kuwa, kesi inayomkabili imetengenezwa ili kukatiza ndoto yake ya kuwa mtangazaji bora duniani .
Mwandishi huyo ambaye anatetewa na mawakili wanaoongozwa na Wakili Katwa Kigen, alipangua hoja zilizowasilisha na upande wa mashtaka kwa kutumia historia ya maisha yake aliyoyaelezea kuwa ni ya kumcha Mungu na uadilifu.
Kama ilivyo kwa washtakiwa wengine, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, Sang anadaiwa kuratibu na kupanga mashambulizi na kusababisha zaidi ya watu elfu moja kupoteza maisha.
Pia anadaiwa kuendesha kampeni ya uchochezi kupitia vipindi mbalimbali vya redio baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.