WAHAMIAJI HARAMU WAIKOROGA SEREKALI

*Taasisi zake mbili sasa zashikana uchawi
*Uhamiaji, RITA waingia katika malumbano
OPERESHENI ya kuwakamata na kuwaondoa wahamiaji haramu nchini, imechukua sura mpya baada ya taasisi mbili za Serikali kuingia katika malumbano. Hatua hiyo imekuja baada ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kukanusha madai yaliyotolewa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, kwamba inachangia uwepo wa wahamiaji haramu.

Hivi karibuni Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo, alisema RITA imekuwa ikitoa vyeti vya kuzaliwa bila kuchunguza taarifa sahihi zinazohusu uraia kwa waombaji.

Idara hiyo ilikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa, kitendo cha RITA kuondoa fomu za uhamiaji zilizokuwa zikitumika kuhakiki uhalali wa mwombaji, kimechangia ongezeko la wahamiaji haramu. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Phillip Saliboko alisema amesikitishwa na taarifa hizo, huku akiitaka Idara ya Uhamiaji kuthibitisha madai hayo.

Saliboko alisema idara hiyo haijaitendea haki RITA kwa kutoa taarifa bubu ambazo hazina uthibitisho juu ya namna wakala huo unavyohusika na tatizo la wahamiaji haramu.

“Hiki si kipindi cha kulaumiana, kila mtu afanye wajibu wake, hizo taarifa kama ni za ukweli busara itumike, Idara ya Uhamiaji ionyeshe uthibitisho juu ya hili badala ya kutoa taarifa za jumla,” alisema Saliboko.

Kuhusu RITA kuondoa fomu ya uhamiaji, Saliboko alikiri kuondolewa kwa fomu hizo na kusema kuwa zilikuwa zinasababisha ucheleweshaji wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa waombaji.

“Ni kweli tumeondoa hizo fomu, naomba nieleweke vizuri hizo fomu hazikuwa kwenye kanuni zetu.

“Tulifikia uamuzi wa kuziondoa baada ya kuona zinasababisha adha na usumbufu mkubwa wa kutoa vyeti vya kuzaliwa.

“Anapotokea mwombaji ambaye vielelezo vyake vinatiliwa shaka, tunashirikiana na idara hiyo na vyombo mbalimbali vya usalama ili kubaini uraia halisi wa mwombaji.

“Si kweli kwamba tunawapa vyeti wahamiaji, utaratibu wetu kabla hatujatoa cheti kwa mtu mzima huwa tunamuhoji, msajili kama hajaridhika anashirikiana na idara nyingine hadi kupata ukweli,” alifafanua.

Hata hivyo, Saliboko alisema utoaji wa vyeti hivi sasa unafanywa kwa umakini mkubwa kwa sababu baadhi ya wahamiaji haramu wanahaha kutafuta uhalali wa kuishi nchini.

“Tumejipanga vizuri watumishi wa RITA wameongeza umakini zaidi tangu ‘Operesheni Kimbunga’ ianze tofauti na siku zilizopita,” alieleza mtendaji huyo.

Utapeli waingia ndani yake

Wakati operesheni hiyo ikifanyika, kumeibuka wimbi la watu wasiokuwa waadilifu kutumia mwanya huo kwa ajili ya kutaka kujinufaisha kwa kufanya vitendo vya utapeli.

Habari za kuaminika ambazo MTANZANIA limezipata, baadhi ya Watanzania wamekuwa wakiwafuata wahamiaji haramu na kuwatishia kuwa ni watu wa usalama wa taifa. 

“Hawa wahamiaji haramu wanajulikana maeneo wanayoishi na hata wengine biashara zao zinajulikana, sasa kinachofanyika, baadhi ya watu (Watanzania), wanajifanya wao ni watu wa usalama.

“Wanavaa suti wanawafuata wanawatisha wanawauliza vyeti na kuwauliza maswali, wanawachukua katika magari na kwenda kuwatelekeza na kuwaambia hawatakiwi kurudi mjini, huku nyuma wengine wanachukua mali zao,” kilisema chanzo chetu.

Hivi karibuni wahamiaji haramu 465 kutoka mataifa mbalimbali, walikamatwa jijini Dar es Salaam.

Idadi kubwa ya wahamiaji hao ni vijana ambao walikuwa wanajishughulisha na biashara mbalimbali zikiwamo uuzaji kahawa, matunda na maji.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad