YANGA KILIO CHA MTU MZIMA..AZAM YAKATAA UTEJA

AZAM imekataa uteja wake kwa Yanga baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo mkali wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.

Azam imefungwa na Yanga kwenye mechi nne zilizopita na kutoa taswira ya kwamba timu hiyo inayomilikiwa na milionea Said Salim Bakhressa ni kibonde kwa miamba hiyo ya soka ya Tanzania Bara.

Yanga iliifunga Azam kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame msimu wa mwaka 2011/12, ikaifunga tena timu hiyo kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara msimu uliopita kabla Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii msimu huu.

Bao lililoizamisha Yanga kwenye mechi ya jana lilifungwa na chipukizi Joseph Kamwaga aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya chipukizi mwenzake Farid Musa. Kamwaga alifunga bao kwenye dakika ya 90 huku mwamuzi wa akiba Oden Mbaga akionesha dakika mbili za nyongeza.

Kwenye mechi hiyo, Azam walitangulia kufunga kupitia kwa mshambuliaji wake mahiri, John Bocco kwenye dakika ya kwanza aliyeunganisha kwa shuti mpira wa kichwa wa beki Kelvin Yondani aliyeokoa mpira wa krosi wa Brian Umony kutoka upande wa kulia.

Kuingia kwa bao hilo la mapema kuliiamsha Yanga usingizini na kufanya mashambulizi mfululizo, lakini washambuliaji wake Didier Kavumbagu, Simon Msuva na Jerry Tegete walipoteza nafasi nyingi za wazi walizopata kwenye dakika ya 5, 8 na 9.

Yanga ilitawala sehemu ya kiungo kwa wachezaji wake Athumani Idd, Haruna Niyonzima na Frank Domayo kwa kuwazidi ufundi viungo Humphrey Mieno, Kipre Balou na Himidi Mao.

Yanga walisawazisha bao kupitia kwa Didier Kavumbagu kwenye dakika ya 51 akitumia pasi nzuri ya Jerryson Tegete. Khamisi Kiiza 'Diego’ ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, aliifungia Yanga katika dakika 66 akiunganisha krosi ya winga Simon Msuva kutoka upande wa kulia. Kiiza aliingia kuchukua nafasi ya Tegete.

Azam walisawazisha kwa njia ya penalti iliyopigwa na Kipre Tchetche kwenye dakika ya 69 baada ya beki wa kushoto wa Yanga, David Luhende kuunawa mpira katika eneo la penalti na mwamuzi wa mechi hiyo Dominic Nyamisana kuamuru penalti hiyo kupigwa upande wa Yanga.

Ikiwa inaaminika kuwa mchezo huo ungemalizika kwa sare, Kamwaga aliwaamsha mashabiki wa Azam kwenye viti kwa kufunga bao zuri dakika ya 90 kwa shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la penalti.

Timu zote zilifanya mabadiliko kwa Azam kuwaingiza Said Moradi, Kamwaga na Kipre Tchetche na kuwapumzisha Jockins Atudo, Farid Musa na Umony na Yanga kumuingiza Kiiza badala ya Tegete.

Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, JKT Ruvu ilipoteza mechi dhidi ya JKT Oljoro baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex. Kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, Coastal Union iliifunga Ruvu Shooting bao 1-0.
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Azam walibahatisha hao hawana jipya kabisa ngoje mechi ijayo tukutane nao uone tutakavyowapa kichapo

    ReplyDelete
  2. Sio walibahatisha ww goli 3 unasema wamebaatisha, acha ushabiki wa kishamba, Puumbaafuuu!!

    ReplyDelete
  3. Funga mbwa hao wakaandamane jangwani, mwaka huu kazi wanayo ushindi wao suluu, mbwa wa kijani hao, wana nini.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad