JAMAL MALINZI AWATOA KIFUNGONI VIGOGO WOTE WA TFF WALIOFUNGIWA NA RAIS WA ZAMANI LEONARD TENGA

Dar es Salaam. Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amemrudisha kundini Michael Wambura na Richard Rukambura baada ya kutoa msahama kwa wajumbe wote waliofungiwa kwa makosa ya ukosefu wa maadili.
Malinzi alitangaza msamaha kwa wahanga wote wa mpira ambao wamekuwa wakipata misukosuko kwa kufungiwa na kuenguliwa kwenye medali za soka kwa visingizio vya maadili.

“Tulikuwa vitani, na katika vita kuna watu ambao wamejeruhiwa, nawapa pole, mimi pia ni miongoni mwa majeruhi wa kamati ambazo zimekuwa zikiwahukumu watu kwa kisingizio cha maadili.
“Hata rais mpya wa nchi anapoingia madarakani anatoa msamaha, na mimi kama rais mpya wa TFF, natoa msamaha wa adhabu kwa watu wote waliofungiwa kuanzia ngazi za Wilaya, Mikoa na mpaka Taifa, kuna waamuzi kama wakina Martin Saanya maskini wamefungiwa mwaka mzima, ila msamaha huu hauwahusu waliofungiwa kwa masuala ya rushwa, iwe ametoa au kupokea.”alisema Malinzi na kushangiliwa na wajumbe wa mkutano mkuu.

Saanya alifungiwa na Kamati ya Ligi chini ya Wallace Karia kwa kipindi cha mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka kwa kile kilichoelezwa ni kuboronga uamuzi katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Coastal Union iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Malinzi pia,  ni mwiba mchungu kwa baadhi ya watu waliokamatwa juzi kwa rushwa na jana suala lao lilitarajiwa kupelekwa TAKUKURU.
Pia kauli hiyo inarudisha matumaini ya Katibu mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa TFF, Michael Wambura ambaye amekuwa mhanga namba moja kwenye kamati za TFF baada ya kuenguliwa mara kwa mara kila anapojitosa kuwania uongozi wa soka.

Wambura aliwahi kuenguliwa kwenye uchaguzi wa Simba na baadae uchaguzi wa Chama cha Soka cha Mara (FAM) kabla ya kuenguliwa kwenye mchakato wa awali wa TFF akiwania Makamu wa Rais.
Hata hivyo mchakato wa pili ulipoanza ambao uchaguzi wake umefanyika jana kwa Malinzi kushinda kwa kishindo, Wambura hakujitosa tena kuwania uongozi ndani ya shirikisho hilo kwa kile alichoeleza hawezi kujikosha kwa maji taka.
Mbali na Wambura, Richard Rukambura naye ni muhanga baada ya kufungiwa miaka 30 kwa kufungua kesi mahakamani kupinga kuenguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa awali uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu. Pia wapo baadhi ya waamuzi ambao wamefungiwa kwa sababu mbali mbali.
“Kwa mujibu wa katiba ya TFF, kifungo cha 44 (7) na 39 (7) uongozi uliopita na kamati zake zote zimemaliza muda wake tangu Desemba 13 mwaka jana, zipo kamati mpya ambazo zimeundwa juzi juzi, kuna kamati za kudumu na kamati ndogo ndogo za kisheria... “Kama rais mpya naomba kibali cha mkutano mkuu kwa sababu uamuzi wote ulioamuliwa na mkutano mkuu ni halali, naombeni kibali chenu nivunje kamati zote niunde kamati mpya, naombeni kibali chenu.” alimalizia kwa kusema.
Wajumbe walijibu “Umepata baba, sawa sawa vunja kabisa ruksaaaaaa”alisema wajumbe hao huku wakipiga makofi kwenye meza.
Baada ya kauli hiyo Malinzi aliwafurahisha zaidi wajumbe hao wa mkutano mkuu kwa kuwambia “Mlitakiwa muondoke leo Jumatatu, lakini mimi kama Rais mpya, naigiza sekretarieti ya TFF, iwalipe posho ya siku moja zaidi na kulala hotelini sasa basi badala ya kuondoka Jumatatu mtaondoka Jumanne.” Kauli hiyo ya Malinzi ilishangiliwa kwa nguvu zote na wajumbe wa mkutano mkuu.

 “Viongozi wa mikoani, jiandaeni kupokea ugeni wa Kamati ya utendaji ya TFF, sasa hivi vikao vitakuwa vinafanyika kwa mzunguko kila mkoa na sio kama ilivyozoeleka vikifanyika  Dar es Salaam pekee.”

Udaku Specially Blog
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad