CUF NAO WAIGOMEA KAMATI YA ZITTO KABWE

*Wasema hata ikiwaita hawatakwenda kuhojiwa
*Chadema, NCCR-Mageuzi wapigilia msumari 
HOJA ya ukaguzi wa ruzuku za vyama vya siasa iliyoibuliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, imeendelea kuvivuruga vyama vya siasa.

Baadhi ya vyama vilivyotajwa na kamati hiyo vikidaiwa kushindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, vimetoa misimamo yao inayoonyesha kutokukubaliana na kauli ya Zitto.

CUF kwa upande wake, kimetishia kwenda mahakamani endapo msajili ataamua kusimamisha ruzuku kama alivyoagizwa na Zitto kwa kile walichosema kuwa hakuna sababu za msingi chama chao kutopewa fedha hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema hawana wasiwasi na hesabu zao na kama msajili ataamua kuisimamisha, watakwenda mahakamani.

Alisema msajili wa vyama vya siasa hawezi kufuta ruzuku ya chama chao wakati wanao ushahidi wa nyaraka zinazothibitisha ofisi yake ilipokea hesabu zao zilizokaguliwa.

Mtatiro alisema kuwa, hesabu ambazo wao hawajapeleka kwa msajili ni za mwaka 2012/2013 na si miaka minne kama Zitto alivyosema. Kutokana na hali hiyo, alisema kuna uwezekano msajili aliyemaliza muda wake hawakukabidhiana baadhi ya nyaraka ndiyo maana inasemekana ukaguzi wa hesabu zao hauko vizuri.

“Sisi hatufanyi kazi na Kamati ya Zitto isipokuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye anapaswa kuhojiwa kama kuna upungufu katika jambo lolote,” alisema Mtatiro.

Kiongozi huyo wa CUF alisema kwamba, awali walikuwa wakifanya ukaguzi wao wa ndani na kupeleka hesabu kwa msajili, lakini mabadiliko yaliyowataka kumlipa mkaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ndiyo yaliyowatia shaka.

Pamoja na hayo, alisema chama chake hakitakwenda mbele ya Kamati ya Zitto kujieleza, kwani hakiwajibiki kwao.

“CUF si Serikali, si utaratibu wala sheria kwa vyama vya siasa kutafuta mkaguzi wake binafsi, mtu hawezi kujikagua mwenyewe badala yake tutasababisha mgongano wa kimaslahi, hii ni aibu kwa Serikali kutokuwa na wakaguzi.


“Ingawa tunatambua Kamati ya Bunge ina uwezo wa kumwita mtu yeyote, tunasema hatutakwenda kwenye kamati hiyo japokuwa hatujapata wito rasmi na tunamtaka Zitto aache kutuchafua kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Mtatiro.

Udaku Specially Blog
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Nikweli ukotayari kunyongwa? acha utani toa hoja

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad