MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutokubali vitisho vinavyotolewa na baadhi ya wabunge wa CCM, kwamba wako tayari Bunge livunjwe kuliko kupitisha mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema kuwa hakuna mwenye ubavu wa kurudi kwenye uchaguzi endapo Bunge litavunjwa, huku akiweka bayana kuwa mkutano wa Bunge ujao utakuwa na patashika endapo wabunge wa CCM watataka sheria ya mabadiliko ya katiba iendelee kubaki na kasoro bila kufanyiwa marekebisho ya msingi.
Angalizo hilo alilitoa jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa Baraza la Uongozi la CHADEMA Kanda ya Kaskazini, inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kuhudhuriwa na muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema wakati wa mazunguzo kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa, aliwataka wasitishe uamuzi wa kuingiza wananchi barabarani kufanya maandamano.
Alisema kuwa walimweleza rais kuwa hawapendi kufanya maandamano ila inabidi pale mambo yanapokuwa hayaendi sawa.
“Jumatatu tutakuwa na kikao cha Kamati ya Bunge ya Uongozi ambayo mimi pia ni mjumbe wake, hivyo kikao hicho kitaniwezesha kujua ni mambo gani yaliyo kwenye sheria ya mabadiliko ya katiba yatakayorudishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.
“Nimtake Rais Kikwete asikubali kutishwa na wabunge na mawaziri aliowateua mwenyewe, kwanza hakuna mbunge wa CCM mwenye ubavu wa kurudi kwenye uchaguzi kama rais atavunja Bunge. Nashangaa rais anatishwaje na watu aliowaajiri yeye?” alihoji.
Alisema CHADEMA wanaenda bungeni kwa roho safi ila kikao hicho kitakuwa na patashika endapo maslahi ya taifa yatawekwa kando na kutangulizwa ushabiki unaoendeshwa na baadhi ya wabunge wa CCM.
Mbowe alisema katiba ni mali ya Watanzania wote, huku akiweka wazi kuwa kwa sasa kuna hofu miongoni mwa wananchi kwani hawajui uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya katiba ipi.
Alifafanua kuwa chama chake kitakuwa kimekamilisha mchakato mzima wa kukiendesha kupitia mfumo wa dijitali ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Kwama wanatarajia taarifa zote, mawasiliano baina ya viongozi na wanachama pamoja na uwekaji wa kumbukumbu utafanyika kwa kupitia mfumo wa mawasiliano wa dijitali.
Naye Mtei alisema kuwa anapata faraja kuona namna chama hicho kinavyokubalika kwa wananchi jambo linaloufanya moyo wake kudunda akiamini kwenye uchaguzi mkuu ujao kitapata ridhaa ya wananchi kuongoza dola.
Chanzo - Tanzania daima
Udaku Specially Blog