Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) linakutana leo jini Dodoma huku hatma ya Mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Hamisi Juma ikiwa mashakani.
Mkutano huo wa baraza ulitanguliwa na kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM kilichokaa jana jioni mjini Dodoma kwenye Ukumbi wa White House ambako ni makao makuu ya CCM.
Sadifa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, analalamikiwa kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala, matumizi mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za chama hicho.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa vuguvugu la kumng’oa, Sadifa alijibu kwa kifupi tu; “Asante Nashukuru.” “Ninaambiwa nimekuwa mtu wa kutukana watu, nimemtukana nani? Asante Nashukuru.,”aliongeza Sadifa hata pale mwandishi alipomuuliza kwa zaidi ya mara tatu aliishia kutoa jibu: “Asante nashukuru.”
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alipoulizwa na Mwananchi jana, alisema kuwa hana taarifa za kuwapo mpango wa kumng’oa mwenyekiti wake kama inavyoelezwa.
“Sikiliza, mimi ndiye Mtendaji Mkuu wa UVCCM, ajenda za mkutano, sisi kama sekretarieti tumeshaziandaa na hakuna agenda kama hiyo. Umoja huu unaendeshwa kwa kanuni na taratibu,”alisema Mapunda.
Mapunda aliyechukua mikoba hiyo Agosti mwaka huu, alipoulizwa kuhusu mkutano huo kugharamiwa na CCM makao makuu badala ya Jumuiya yenyewe, alikanusha taarifa zilizozagaa akisema: “Mimi ndiye niliyeitisha mkutano huu, sasa chama kinatoka wapi?”
Mjumbe aanika madudu ya UVCCM
Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Ruvuma, Alex Nchimbi alifafanua hakuna njama za kumtoa ila mambo anayotakiwa kurekebisha ndio yanaweza kumtoa.
Nchimbi alisema kuwa UVCCM inakabiliwa na tatizo la matumizi mabaya ya fedha na kibaya zaidi hesabu za chama hicho hazijakaguliwa kwa muda mrefu.
Alisema jumuiiya hiyo hupata kiasi cha Sh80 milioni kutokana na miradi mbalimbali kama jengo lililoko makao makuu ya UVCCM, lakini fedha hizo zinafujwa.
“Ila utashangaa kaka yaani zile fedha zinavyofujwa. Hadi kwa mwezi jumuiya inabakiwa na Sh8 milioni au wakati mwingine hadi Sh6milioni,” aliongeza Nchimbi.
Nchimbi aliongeza tatizo jingine ni uteuzi wa viongozi bila kufuata taratibu.
Alisema kuwa Sadifa aliteua sekretarieti kabla ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ambapo ni kinyume na utaratibu.
Alitaja viongozi hao kuwa ni Mkuu wa Idara ya Uchumi na Fedha, Omar Suleimani, Mkuu wa Chipukizi na Uhamasishaji, Omar Justus na Tumaini Mwakasege, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Oganaizesheni.
“Umoja wetu una pikipiki 10, lakini kapeleka pikipiki mbili Morogoro na nane kazipeleka Zanzibar kwenye jimbo lake. Ukichunguza uandikishaji wake utagundua bado zinamilikiwa na UVCCM”, alisema Nchimbi.
Nchimbi pia alimtuhumu Sadifa kwa kuanzisha nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa bila ya baraka za Baraza Kuu.
“Hivi nani angewalipa watu hawa. Lazima tujiulize UVCCM ina fedha gani za kuwalipa makatibu wa mikoa na wasaidizi?,” alisema Nchimbi
Wanataka UVCCM izaliwe upya
Nchimbi alisema UVCCM wanakabiliwa na changamoto ya kusafisha uoza ndani ya jumuiya na hasa kwa kuzingatia kuwa Sadifa anatoka Zanzibar.
“Kwa hali ya kawaida, kama si kulindwa na wazee kwa hoja za kulinda Muungano na amani katika jumuiya na kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa basi tusingekuwa naye,” alisema Nchimbi.
Nchimbi, hata hivyo, alionya kuwa uongozi wa vijana uliopo usiporekebishwa hawawezi kumsaidia balozi wa nyumba 10 kushinda uchaguzi
Mpango huo wa kumtimua Sadifa ni wa pili ndani ya siku zisizozidi 60 baada ya awali kuibuka mvutano mkubwa ndani ya jumuiya hiyo, kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja huo kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti huyo.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu kilichokuwa kikifanyika Zanzibar, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Aking’olewa Sadifa, itakuwa mara ya pili kwa mwanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Zanzibar kung’olewa baada ya Masauni Yussuf Hamad kung’olewa mwaka 2010 kwa tuhuma za kughushi umri.
-Mwananchi
Udaku Specially Blog