AFRIKA KUSINI YAGUSWA KUFUNGIWA KWA MAGAZETI YA MWANANCHI NA MTANZANIA

HATUA ya Serikali ya Tanzania kuyafungia magazeti mawili ya kila siku, Mtanzania (kwa siku 90) na Mwananchi (siku 14), imesababisha mjadala wa hali ya juu katika maeneo mbalimbali barani Afrika. Gazeti la Mail&Guardian la Afrika Kusini, liliandika kuwa hatua hiyo ni kusambaratisha uhuru wa vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari. 

Gazeti hilo liliendelea kudai kuwa hatua ya kufungia vyombo vya habari ni kuvunja maana ya upashanaji habari, ambayo inatakiwa kuwafikia wananchi. 

Chombo hicho cha habari kimeifananisha adhabu hiyo ya kuyafungia magazeti hayo mawili kama ile iliyochukuliwa na Serikali ya Uganda, mwanzoni mwa mwaka huu ya kulifungia gazeti jingine la NMG, la Daily Monitor, kwa madai lilichapisha habari ya uchochezi.

Tangazo la Serikali ya Tanzania kupitia Gazeti la Serikali namba 333 Septemba 27 mwaka huu lilitangaza magazeti ya Mwananchi na Mtanzania yamefungiwa.

Katika hatua nyingine, gazeti la Mail&Guardian lilimkariri Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akisema kuwa “Kufungia magazeti hakutazuia haki ya wananchi kutoa maoni yao na kupambana mpaka kupatikana utawala bora. 

“Kwanza kufungiwa kwa magazeti hayo kutawaimarisha waandishi kwa kiwango cha juu. Unalifungia gazeti kwa kutoa taarifa za mishahara? Tatizo liko wapi, je, watu hawatakiwi kujua mishahara ya watumishi wa umma?”

Ikitumia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, iliyafungia magazeti hayo kwa madai ya kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani. Serikali ilitangaza kulifungia Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90, kuaNzia Septemba 27, mwaka huu. 


Uamuzi huo ulichukuliwa na serikali kwa madai kwamba, magazeti hayo yaliandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola. Uamuzi huo, ambao ulikuwa ghafla, ulipokewa kwa mshituko mkubwa na wadau mbalimbali, huku wengi wakihoji mwelekeo wa demokrasia nchini. Wadau hao wa kada mbalimbali, wakiwamo wanasheria, wanataaluma, wanahabari, wanaharakati, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu, wote wamekuwa na kauli moja ya kufanana.

Source:Mtanzania

Udaku Specially Blog

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad