AZAM YATOKA SARE NA WAGOSI COASTAL UNION - MECHI YATAWALIWA NA VURUGU

SULUHU ya bila kufungana kati ya Coastal Union na Azam FC katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga imezidi kuwaongezea idadi ya suluhu Wagosi wa kaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Mchezo huo uliokuwa na presha kubwa kwa mashabiki na wachezaji ulimuweka katika wakati mgumu mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani, kutokana na kushutumiwa kuwapendelea Azam FC.

Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa nguvu zikihakikisha zinapata mabao ya mapema na kujihakikishia ushindi lakini hakuna hata timu moja iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kushambulia kwa kasi huku wakimiliki mpira hali iliyowachanganya wachezaji wa Coastal Union wakaanza kupoteana na kucheza bila kufuata mfumo. Hali hiyo ilizidi kuwachanganya Wagosi wa Kaya hasa baada ya mwamuzi kuanza kutoa maamuzi ya utata, kwani katika dakika ya sabini alitoa kona kwa Azam wakati ilikuwa ni goal kick.

Mashabiki wakaanza kuhamaki na kutaka kuvuruga mchezo baada ya mwamuzi kuzidisha kutoa maamuzi ya utata kama faulo zisizoeleweka na kona za utata. Hali hiyo ilimtisha mwamuzi na kusimamisha mchezo mara kwa mara ili kuwataka wasimamizi wa mchezo huo kuwatuliza mashabiki.

Tukio lililotokea kipindi cha kwanza ambapo mwamuzi wa pembeni alipigwa na kitu kisichojulikana kutoka jukwaa la 'Rasha' lilitaka kujirudia kipindi cha pili baada ya chupa na mawe kutupwa uwanjani baada ya mwamuzi kutoa faulo nje kidogo ya 18 upande wa Coastal Union.

Dakika ya 65 mwalimu Hemed Moroco alifanya mabadiliko na kumtoa Pius Kisambale akaingia Suleiman Kassim 'Selembe'. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Wagosi hasa kutokana na aina ya uchezaji wa Selembe kutumia mipira ya kasi.

Azam FC walianza kuelemewa kutokana na Mganda, Yayo Kato kutumia vema mwili wake mfupi na wenye nguvu kuwashambulia mabeki wa Azam, hali hiyo iliwafanya Azam kubadilika na kucheza mpira wa hovyo uliowapa nafasi Coastal Union kupiga mipira mirefu ambapo ilipofika dakika ya 75 kipindi cha pili katika jukwaa la African Sports, Wagosi walikosa bao la wazi baada ya Selembe kupiga krosi iliyopenya ngome ya Azam akiwemo mlinda mlango Mwadini Ally na kugonga mwamba.

Kutokana na piga nikupige ya lala salama kufika dakika ya 74 mwamuzi alimnyooshea mlinzi wa kulia wa Coastal Union, kinda Hamadi Juma 'Basmat', kadi nyekundu baada ya kubadilishiana maneno na mchezaji wa Azam, Kipre Tchetche.

Tukio hilo lilianzia kwa Kipre kumpiga Hamadi kiwiko cha shingo hali iliyomfanya kinda huyo kumfuata kwa jazaba huku akimuuliza kwanini amemfanyia hivyo. Mwamuzi baada ya kuona Hamadi amemuelekezea kichwa Kipre akadhani kinda huyo anapigana ndipo akatoa kadi ya moja kwa moja.

Baada ya kadi hiyo hali ya uwanja ilichafuka ambapo mashabiki walikuwa wakipiga kelele huku wachezaji wakitaka kupigana, ndipo mchezaji mwingine wa Coastal Union beki wa kushoto Othman Tamim akapewa kadi ya njano papo hapo.

Baadaye mchezo ulirudi katika hali yake lakini ngome ya Coastal Union ilikuwa imepwaya hali iliyomfanya Juma Said 'Nyoso' kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha ngome yao inakuwa imara.

Ilipofika dakika ya 84 mwlimu Moroco alifanya mabadiliko kwa kumtoa Uhuru Suleiman na kumuingiza Yusuf Chuma. Ambapo kinda huyo alionyesha uwezo mkubwa na kurudisha uhai wa safu ya ulinzi.

Mpaka mwamuzi wa leo anapuliza kipyenga cha mwisho matokeo yaliendelea kusomeka hivyo hivyohivyo 0-0, na kuendelea kuibakisha Coastal Union katika nafasi ya nne ikiwa na point 11 nyuma ya Azam iliyo nafasi ya tatu yenye point 11 lakini ikiwa na mabao mengi ya kufunga.

Baada ya mechi ya leo Coastal Union itashuka dimbani wiki ijayo katika uwanja wa Chamazi dhidi ya Ashanti United wanaoshika mkia katika ligi.


HABARI NA PICHA KWA HISANI YA COASTAL UNION BLOG


Udaku Specially Blog
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad