HUU NDIO MUAFAKA ULIOFIKIWA KATI YA RAIS KIKWETE NA KAMBI YA UPINZANI JUU YA VUGUVUGU LA KATIBA MPYA

Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Kikwete ili kuondoa sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge lilipokutana mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema. Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na wenyeviti wao ni Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John Mnyika wa Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete kukutana na viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha kurushiana maneno baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa wakivutana na viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri katika tukio lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu kutokana na ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa Septemba.
Rais Kikwete alionekana mwenye furaha tele wakati alipokutana na viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi ilikuwa pale alipokutana na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Viongozi hao walisalimiana huku wote wakitabasamu na kuashiria kuwa waliamua kuweka tofauti zao pembeni na kuangalia masilahi ya nchi.
Kumbuka katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Septemba, Rais Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa yeye hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alikaririwa akisema kauli hiyo ya Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu, huku akisisitiza kuwa mbunge huyo alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alipinga tuhuma hizo na kusisitiza Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) bila ya ridhaa yao.
Chikawe, Wassira na Lukuvi ndani
Mawaziri watatu, ambao walitetea kwa nguvu kupitishwa kwa muswada ule ndani na nje ya Bunge walihudhuria mazungumzo hayo.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira walikuwemo kwenye mazungumzo ya jana.
Mawaziri hawa kwa nyakati tofauti walitetea kuwa mchakato wa muswada ule haukuwa na matatizo yeyote na kushikilia kuwa lazima Rais lazima asaini muswada kwani ulikuwa umepitishwa kihalali na Bunge.
Pia walikuwa wameshikilia kuwa safari hii kulikuwa hakuna mambo ya mazungumzo kati ya Rais na upinzani.

Chanzo cha sintofahamu
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala wa muswada huo wakipinga matayarisho yake kutoshirikisha upande wa Zanzibar na pia walikuwa hawakubaliani na baadhi ya vipengele vya muswada huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Ikulu zilisema kwamba Rais Kikwete alisaini muswada huo tangu Oktoba 10 mwaka huu siku ambayo wapinzani walipanga kufanya maandamano nchi nzima.
Katika mahojiano na Mwananchi jana jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema muswada huo tayari ulikwishasainiwa na Rais na kama kuna marekebisho yatafanywa.
Mwananchi ilimtafuta Rweyemamu baada ya kusikia akithibitisha kusainiwa kwa muswada huo katika mahojiano na BBC Idhaa ya Kiswahili jana.
Akizungumza na Mwananchi Rweyemamu alisema, “Rais ameshasaini tangu Oktoba 10, unajua kulikuwa hakuna tatizo lolote kuhusu muswada huu kwa sababu ulifuata taratibu zote bungeni.”
Rweyemamu alisema kuwa awali Ikulu ilitoa taarifa kuwa Rais atakutana na wapinzani, pia atausaini muswada huo.

“Muswada umepitishwa bungeni na yeye amekamilisha kazi kwa kuusaini ili kuwa sheria. Alipokutana na wapinzani leo (jana) amewaeleza hilo na wameridhika” alisema Rweyemamu.



Udaku Specially Blog
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad