Brandts ashangaa
______________________________ ___________________
KOCHA wa Simba Abdallah Kibadeni amelaumu
kuwa kuna hujuma imefanyika kwa wachezaji
wake, wakati Mholanzi wa Yanga, Ernest Brandts
amesema wachezaji wake hawako kiprofesheno. Kibadeni aliweka wazi kuwa Yanga isingeweza
kuwafunga mechi hiyo lakini kwa sababu kuna
watu wamevamia kambi yake na kuwadanganya
wachezaji wakacheza chini ya kiwango. “Nawajua wachezaji wangu, kiwango kile si chao,
hawakutaka kucheza ndiyo maana tulifungwa
mabao yale matatu kipindi cha kwanza. Kuna watu
wanakuja kambini na kuwapandikiza maneno
wachezaji na hao waliopandikizwa maneno
hawakucheza vile inavyopaswa kipindi cha kwanza wakaruhusu mabao matatu ya haraka
haraka,”alisema Kibadeni katika Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam jana Jumapili. “Tulivyokwenda mapumziko, nilizungumza nao na
nikawaambia, mmeshawapa mabao matatu
yanatosha, sasa chezeni mpira,”alisema Kibadeni
ambaye alienda mbali na kuwazungumzia kiungo,
Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’ na winga, Haruni
Chanongo ambao aliwatoa na kuwaingia, Said Ndemla na William ‘Gallas’. “Siwezi kuwataja kwa majina, watajijua na
kujichuja wenyewe. Yule Humoud nilimpanga kwa
makusudi kama mlivyoona ndiyo maana
nilimtoa,”alisema Kibadeni ambaye wiki iliyopita
alikuwa akilalamika kwamba kuna wachezaji ndani
ya Simba ambao wanamtengenezea majungu kwavile anawaambia ukweli na hawataki kufuata
utaratibu wa kambi yake.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernest Brandts alisema:
“Tulistahili kushinda na ninachowalaumu
wachezaji wangu hawako kiprofesheno kwa
sababu baada ya kushinda mabao 3-0 kwenye
mapumziko waliingia wanashangilia wakati mechi
inaendelea. Nilishangaa sana. “Wakati wa mapumziko walivyoingia kwenye
vyumbani walikuwa wanashangilia kama
wameshinda mchezo, mpaka nikashangaa, sare
wameitaka wenyewe, tulipata nafasi nyingi na
tukashindwa kuzitumia. Timu nzima ilikuwa na
upungufu, Luhende na Chuji walifanya makosa mawili yakatugharimu,”alisisitiza Brandts. Na alipoulizwa kama kuna hujuma, Brandts alisema
inawezekana. “Haiwezekani tuongoze mabao
matatu na baadaye warudishe yote, haiwezekani
wachezaji wametuhujumu na kinachotakiwa
tuwachomoe baadhi yao,”alisikika shabiki mmoja
maarufu.
Udaku Specially Blog