KIOJA MUHIMBILI:MWANDISHI WA GLOBAL AJIFANYA DAKTARI NA KUFANYA KAZI SIKU TATU BILA KUSHTUKIWA

Stori: Waandishi Wetu

KUNA madai ya ulinzi dhaifu unaoikabili Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam na ndiyo maana kila kukicha madaktari feki wananaswa wakiwa katika harakati za kujipatia kipato cha rushwa kutoka kwa wagonjwa wanaopigania afya zao, Ijumaa limebaini kioja cha aina yake.

Kikosi cha makachero cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kutoka Global Publishers kiliamua kuyafanyia kazi madai hayo ili kujiridhisha.
Kikosi cha OFM chenye makachero wanne kilipangwa, kikajiweka tayari kwa kuingia kwenye hospitali hiyo kufanya uchunguzi wa awali ambapo walibaini kwamba ni kweli kuna udhaifu wa ulinzi.
Baada ya uchunguzi huo, OFM walirudi makao makuu ya Global, Mwenge, Dar es Salaam na kuweka mikakati ya kuanza kazi siku iliyofuata.

Vazi la kidaktari aina ya joho jeupe lenye kumfika dokta magotini lilipatikana sanjari na kipimo cha kitabibu ambacho huvaliwa shingoni kama daktari hampimi mgonjwa.

MPANGO ZA OPARESHENI
Mpango wa zoezi hilo ulikuwa ni kufanya kazi kwa siku tatu, kuanzia Septemba 24-27, mwaka huu ambapo maeneo mbalimbali ya kutembelewa na daktari huyo feki yalianishwa ikiwa ni pamoja na mapokezi, kwenye korido, wodini, theatre na mwisho kabisa ni kwenda kuonana na Afisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha kwa lengo la kusalimiana naye ili kuona kama ataweza kumbaini mwandishi huyo aliyejifanya daktari.
Kuanzia aya zinazofuata, mwadishi aliyejifanya daktari anasimulia mwenyewe hali ilivyokuwa siku ya kwanza ya oparesheni:

SEPTEMBA 24, SAA 5:00 ASUBUHI
Ni Septemba 24, mwaka huuu, siku ya Jumanne, saa 5:00 asubuhi nikiwa na watenda kazi wenzangu tunaingia Hospitali ya Muhimbili, kabla ya kushuka kwenye gari, navaa joho jeupe na kujipachika kwenye shingo kifaa cha kupimia wagonjwa.
Ilibidi nivae na miwani ya kawaida ili nifanane na daktari japokuwa haikuwa lazima sana.

Niliamua kujiita Dokta Ruta endapo ningekutana na ugumu wenye kulazimisha kuulizwa jina langu.

MAPOKEZI
Mbele yangu walinitangulia watenda kazi wenzangu ambao kazi yao ilikuwa kuendelea kufanya uchunguzi zaidi kama kuna madaktari wengine feki mbele yangu ili wasiharibu zoezi.
Nilifika mapokezi bila kukaguliwa na walinzi ambapo niliwakuta vijana wawili wakiwa na vielelezo vya hospitali hiyo vikionesha ugonjwa wa mama yao. Walinionesha vielelezo hivyo huku wakiulalamikia uongozi mbovu katika kushughulikia matatizo yao.
Walidai kwamba, siku hiyo ilikuwa ya nne wanazungushwa kupata huduma hospitalini hapo. Wakasema imefika hatua wamekata tamaa na hawajui waende wapi kulalamikia hali hiyo.

MALALAMIKO YAO
“Daktari tunaomba msaada wako, tuna siku nne bila kupata huduma hospitalini hapa. Tumeanza kuchoka na mama yetu ni mgonjwa sana, tusaidie,” walisema vijana hao ambao hawakutaja majina.
“Mimi nawaomba muendelee kuwa wavumilivu mtahudumiwa kama wengine, si mnajua hii ni hospitali ya taifa, ina wagonjwa wengi sana,” niliwajibu.

SAA 6: 30 MCHANA, MZEE ASAKA HUDUMA
Saa 6 na nusu mchana bado nikiwa na sare ya kazi, nilipishana na daktari mmoja akiwa amekiweka kipimo kwenye mfuko wa upande wa kulia wa joho, ilibidi na mimi nikitoe shingoni kipimo changu na kukiweka mfukoni kama yeye. Nilihisi huenda ni staili ya utambulisho ya madaktari wa hospitali hiyo.
Nilikwenda hadi kwenye dirisha la kutolea risiti za malipo ambapo nilikutana na mzee mmoja aliyeniomba msaada wa kuandikiwa kibali cha kuchukua dawa nje ya hospitali.
“Daktari naomba unisaidie nina siku mbili nahitaji kupewa kibali tu cha kuchukua dawa nje ya hospitali lakini kila ninayemwendea ananiambia yuko bize,” alisema mzee huyo.
Mwandishi ‘daktari’: Mzee fuata utaratibu wa kuandikiwa kibali na si kupita njia za panya.
Mzee: Siwezi kupata msaada kwa wakati endapo nitafuata utaratibu. Lakini sawa ngoja nifuate utaratibu wenu.

MZEE MWENYE TATIZO LA KANSA
Nikiwa maeneo hayo, mzee mmoja naye alinifuata na kusema ana tatizo la kansa ya koo, akaniomba nifanye jitihada zozote ili kunusuru maisha yake kwani alikuwa na mwezi mmoja tangu apewe ahadi ya kufanyiwa upasuaji.
Mwandishi ‘daktari’: Mzee fuata utaratibu, utafanyiwa upasuaji wala usiwe na shaka.

MZEE MLEMAVU WA MGUU
Saa saba na robo nilitoka mapokezi na kushika mwelekeo wa Wodi za Sewa Haji, Kibasila na Mwaisela. Njiani nilikutana na mzee mmoja mlemavu wa mguu uliokatwa, alinionesha X-ray. Bila kusita nilisimama na kuipokea nikaikagua hadharani kwa kuiweka hewani kinyume na taratibu za udaktari lakini hakuna mtu yeyote aliyekuwa tayari kunikamata kwa kitendo hicho.

MTOTO MWENYE TATIZO LA SHINGO
Nikiwa bado naelekea upande wenye wodi hizo nilikutana na mama mmoja ambaye alinisimamisha na kuniambia anatoa shukrani zake za dhati kwa madaktari wa Muhimbili kwani mtoto wake alikuwa na tatizo la shingo na alifanikiwa kupata matibabu, lakini akaongeza kuwa kilichomuokoa mwanaye akapata tiba nzuri ni pesa zake.
Mwandishi ‘daktari’: Una uhakika mama?
Mama: (huku akiondoka) Khaa! Kwani siri, sijui mkoje hapa!
Nilipita kwenye wodi hizo kwa nje na kukutana na wagonjwa mbalimbali, wengi walionesha kutaka kusaidiwa zaidi kuliko kushukuru kwamba wameshapata tiba.

OFM WARUDI OFISINI NA USHINDI
Saa 8:55 mchana tulirejea kwenye gari na makachero wenzangu na kurudi ofisini huku nikiwa bado nimevaa gwanda la kitabibu.

SIKU YA PILI WODINI
Jumatano ya Septemba 25, mwaka huu, saa 9:23 alasiri, OFM iliingia mzigoni tena.
Oparesheni ya safari hii ilipangwa kufanywa ndani ya wodi ambazo jana yake hazikufikwa kutokana na muda, kwani mbali na mwandishi huyo kujifanya daktari Muhimbili pia alikuwa na majukumu mengine ya habari za kawaida.
Aya zinazofuata paparazi huyo aliyefanya kazi nzuri ya kuhakikisha hagunduliki kama si daktari anasimulia mwenyewe:

SAA 9:23 WODI YA KIBASILA
Saa 9:23 alasiri siku ya pili ya zoezi letu, baada ya kuvalia gwanda langu kwenye gari nilishuka kwenye gari na kuanza kutembea kuelekea Wodi ya Kibasila.
Niliwapita walinzi ambao walisimama kwa heshima zote wakiamini mimi ni daktari halali kabisa, niliwasalimia wakaitikia, nikawapita wauguzi, nikaenda ndani ya wodi ambapo wagonjwa walikuwa wamelala katika hali ya kupoteza matumaini.
Nilimfuata mama mmoja aliyelala kwa huzuni, nilimuuliza tatizo lake ambapo aliniambia ana uvimbe sehemu za siri. Alinishukuru kwa kufanyiwa upasuaji na akasema anaendelea vizuri.
Mwandishi ‘daktari’: Pole sana mama.
Mama: Asante dokta, namshukuru Mungu nimefanyiwa upasuaji. Sasa naendelee vizuri dokta. Nawashukuru sana nyinyi.

AINGIA WODI YA MWAISELA
Nilitoka kwenye wodi hiyo kwa kutamba na kwenda Wodi ya Mwaisela, ghorofa ya kwanza ambapo pia muda wa watu kuona wagonjwa ulifika, wakaingia. Mimi niliingia kwa kuheshimiwa na wauguzi waliokuwa wamekaa kwenye ofisi yao.
Niliongea na wagonjwa mbalimbali na kuwapa pole, wengi walishukuru ujio wangu kama daktari na waliniambia maendeleo yao kwa wakati huo.
Saa kumi na moja na nusu kikosi kizima kilirejea kwenye gari, safari ya kurudi ofisini ikaanza. Ilikuwa siku ya pili ya oparesheni hiyo.

CHUMBA CHA UPASUAJI ‘O THEATRE/ICU/X RAY/CT SCAN’
Siku iliyofuata, yaani Alhamisi ya Septemba 26, saa 7 mchana nikiwa na wenzangu tulirejea tena Muhimbili, safari hii maeneo yaliyotakiwa kufanyiwa kazi ni chumba cha upasuaji na kwa afisa uhusiano wa hospitali hiyo.
Kwanza kwenye chumba cha upasuaji nilibaini kwamba kila mtu anaweza kuingia. Niliingia kwenye chumba hicho na kuwasalimia madaktari waliokuwa tayari wamevaa zana za kazi. Salamu yangu ilijibiwa bila maswali wala kutazamwa kwa mshangao kwamba mimi ni mgeni.
Wakati natoka katika chumba hicho cha upasuaji, nje nilikutana na mzee mmoja ambaye aliniomba msaada wa kupangiwa siku ya kufanyiwa operesheni kwa ndugu yake wa karibu.
Mwandishi ‘daktari’: Mzee fuata taratibu, lakini pole sana.
Mzee: Asante sana.
Nilipoachana tu na mzee huyo, muuguzi mmoja alitokea na kuniuliza:
“Hivi dokta incharge (mkubwa) wa leo ni nani hapa?”
Mwandishi ‘daktari’: Ratiba si inajulikana!

AINGIA OFISI YA AFISA UHUSIANO
Niliachana na muuguzi huyo, sasa nikafunga kazi kwa kwenda kwenye ofisi ya uhusiano. Nilikutana na bosi wa hapo, Aminiel. Nilisalimiana naye.
Mwandishi ‘daktari’: Habari za leo kiongozi?
Afisa Uhusiano: Salama, za leo dokta?
Mwandishi ‘daktari’: Safi tu, samahani mkuu nina ndugu yangu ameletwa jana kutoka mkoani una taarifa yoyote?
Afisa Uhusiano: Pole sana dokta, nakuomba uende pale emergence room kwenye mapokezi, pale watakuwa na takwimu zote dokta, nakutakia kazi njema.
Mwandishi ’daktari’: Asante kiongozi kwa maelekezo naomba nirudi mapokezi kupata ufafanuzi.
Afisa Uhusiano: Oke, kazi njema.
Mwandishi ‘daktari’: Oke, asante.
Nilitoka hapo kuelekea chini, nikampita mlinzi, mbele nikakutana na nesi wa kiume akiwa anaingia kwa bosi huyo, tulisalimiana kwa kusimama na kushikana mikono kisha tukaambiana poapoa baadaye.
Zoezi letu liliishia hapo na kurudi ofisini. Kifupi niliweza kutembea maeneo mbalimbali ya Muhimbili huku nikiwa napishana na wauguzi kwa madaktari bila kunishtukia. Sikuona hata mmoja mwenye dalili ya kunitilia shaka zaidi ya kunichangamkia kuwa ni mwenzao.

OKTOBA 2, 2013 AFISA UHUSIANO ABANWA NA IJUMAA
Juzi asubuhi, Ijumaa lilimpigia simu Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha na kumuuliza maswali haya:
Mwandishi: Kuna madai kwamba hapo Muhimbili mna madaktari feki wengi sana, inakuwaje kuhusu hilo?
Afisa Uhusiano: Kwanza kabisa sisi hatuajiri madaktari feki, kuna utaratibu wa kuajiri. Hao makanjanja kila fani wapo lakini hapa Muhimbili akijipenyeza tunamgundua na kumkamata.
Mwandishi: Je, kama akitokea daktari feki akaingia mpaka wodini mtajuaje?
Afisa Uhusiano: Mara nyingi manesi wanaokuwa wodini ni rahisi kuwagundua na kutoa taarifa.
Mwandishi: Sasa mbona kuna mwandishi wetu alijifanya daktari akawa anafanya shughuli za kuwaona wagonjwa hapo kwa siku tatu?
Afisa Uhusiano: Hakuna kitu kama hicho, si rahisi kuingia na kufanya kazi kwa siku tatu bila kugundulika.
Mwandishi: Mbona huyo mwandishi alishakuja hadi ofisini kwako tena mkaongea akisema ana mgonjwa wake katoka mkoa?
Afisa Uhusiano: (mshangao) Hakuna kitu kama hicho bwana.

TAHADHARI
Kikubwa kilichobainika Muhimbili ni ukosefu wa ulinzi makini kwani kama mtu anaweza kuvaa vazi la kidaktari na kukatiza maeneo yote hadi kuingia wodini iko siku ataingia mtu mbaya na kufanya mambo ya ajabu, hata kuiba wagonjwa na kuondoka nao, achilia mbali masuala ya ugaidi.


Chanzo.KIOJA MUHIMBILI - Global Publishers

Udaku Specially Blog

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sio kweli ofisi ipi atafanyia?kila dr.lazma ana nesi wa zamu wa kumsaidia labda kama alikua akizunguka zunguka tu

    ReplyDelete
  2. Ni hatari sana udhaifu km huu unavyojulikana duniani,sawa na viwanja vya ndege vya afrika,na hongo inavyo tawala ,ni hatari sana kwa usalama wa nchi,jambo la kwanza bongo nikuimarisha vyombo vya ulinzi na kujiamini,nasio kuacha wageni wanapita airport bila kukaguliwa km wenyeji ,mbona huku ,tunachekiwa hivyo,kuna safu ya ulinzi haipo nyumbani tuko nyuma bado ila tuna vijana wanao weza hiyo kazi ,bila uwoga wa wageni ,kutoka hapa maryland.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad