MAAJABU YA MTOTO ALIYEFUFUKA MENGI YAJITOKEZA BAADA YA KABURI KUFUFULIWA

Stori:Victor Bariety, Geita 
TUKIO la mtoto Shaaban Maulid, 16, aliyefariki dunia miaka mwili iliyopita kabla ya mwaka huu kuonekana (kufufuka), limeendelea kutikisa baada ya maajabu mengine kujiri.
Shaaban, alifariki dunia na kuzikwa Januari, 2011 lakini Septemba 30, mwaka huu, alionekana akiwa hai, ingawa alikuwa akizungumza kwa taabu.
Kwa vile kufufuka kwa Shaaban ni jambo lililoacha wazi midomo ya wengi hususan waliohudhuria mazishi yake miaka miwili iliyopita, ilibidi kaburi alilozikwa lifukuliwe ili ndani yake ijulikane kuna nini.
Tamko la kufukua kaburi la Shaaban ni azimio la kifamilia, hasa baada ya ndugu na majirani kupendekeza, kwani kufufuka kwake, kulivuruga vichwa vingi, wapo walioamini inawezekana, ila wengine wakipinga kwamba mtoto huyo aliyeibuka sasa ni mzimu tu.

MAUZAUZA KABURINI
Shaaban alizikwa kwenye eneo la nyumba ya baba yake, Maulid Shaaban, kwa hiyo haikuwa shida kulipata kaburi, kwani familia nzima na hata majirani wanalijua kwa sababu walishiriki kumzika.
Jumatano iliyopita, shughuli ya kufukua kaburi la Shaaban ilifanyika. Kazi hiyo ilianza saa 2 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi, kabla ya kukamilika saa 4.30 asubuhi.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa kipindi chote ambacho ufukuaji ulifanyika, mauzauza mengi yalitokea, hivyo kusababisha taharuki na hata watu wengine kutimua mbio.
Wakati shughuli ya ufukuaji ikiwa mbichi kabisa, alitokea mbwa kutoka kusikojulikana ambaye alifika na kuanza  kujigalagaza juu ya kaburi hilo, huku akibweka. 
Hali hiyo, ilitafsiriwa na wengi kwamba mbwa huyo alikuwa hataki kaburi hilo lifukuliwe, ingawa baadaye aliondoka taratibu akibweka na kutokomea kusikojulikana.
Saa 2.30 asubuhi wakati ufukuaji ukiendelea, mwanamke jirani anayeitwa Sharifa Hitler, alianguka na kupoteza fahamu, kabla ya kuzinduka dakika 20 baadaye, kufuatia jitihada za kumuwekea kipande cha sabuni mkononi.
Baada ya kuzinduka, Sharifa alisema kuwa alisikia kichwa kinakuwa kizito, akapatwa na kizunguzungu kisha akapoteza fahamu.
Saa 3.05 asubuhi, tukio lingine litokea, kwani kipindi kaburi linafukuliwa, ukuta wa nyumba ya baba yake Shaaban, nao ulianguka na kutoa sauti yenye mshindo mkubwa.
Sauti hiyo iliwatisha wengi, kwa hiyo watu walikimbia kwa kutawanyika, kila mmoja akishika uelekeo wake.
Kuanguka kwa ukuta huo, kulifanya kazi ya kufukua kaburi isitishwe kwa muda ili kutawanya kifusi cha ukuta wa nyumba, kuhakiki kama kuna mtu aliangukiwa na kufunikwa.
Hata hivyo, baadaye iliamriwa mambo yote mawili yafanyike kwa wakati mmoja, baadhi wahusike na utawanyaji wa kifusi na wengine waendelee kufukua kaburi ili kwenda na muda.

MAAJABU NDANI YA KABURI
Kule kwenye kifusi, ilionekana hakukuwa na tatizo lolote lakini kwenye kaburi baada ya ufukuaji kukamilika, mambo yaliyoonekana ni haya;
Mosi; kwa mila za Kiislam, ndani ya kaburi, kuna sehemu ndogo ambayo huchimbwa kulingana na kimo cha marehemu, kisha kulazwa ndani yake.
Sehemu hiyo huitwa mwanandani, kwa hiyo baada ya kufukua, badala ya kukuta mwili, wafukuaji walikutana na chungu kikubwa.
Pili; kile chungu kilikuwa kimefunikwa na mifuko aina ya viroba. Tafsiri ya wengi walioshuhudia tukio hilo ni kwamba sanda aliyozikwa nayo Shaaban miaka miwili iliyopita, ndiyo iliyogeuka kiroba.
Tatu; nndani ya chungu kulikuwa na mifupa ya kiumbe cha ajabu, kwani kwa muonekano haifanani na ya binadamu wala mnyama yeyote anayefahamika, kwani ilikuwa ni midogomidogo mno.
Nne; kulikuwa na madawa yenye umbo la kimimika, rangi nyeusi.
Dunia Mrisho ambaye alikuwa shuhuda wa tukio hilo na alikuwepo miaka miwili iliyopita wakati Shaaban akizikwa, alisema kuwa yaliyoonekana ndani ya kaburi hilo, yamewashangaza wengi.
“Huyu mtoto tulimzika kwa heshima zote za Kiislam na mwili wake ulikuwa kwenye sanda, hii mifuko ndani ya kaburi imetoka wapi? Tunashangaa pia kukuta chungu ndani ya kaburi na kina mifupa na yule mbwa aliyetokea na kutokomea ni wa nani? Hapa kuna kitu,” alisema Dunia ambaye ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

KWANI SHAABAN ALIKUFAJE?
Januari Mosi, 2011, Shaaban akiwa na afya njema kabisa, aliondoka nyumbani kwao asubuhi kwenda kuchunga mbuzi kwenye malisho.
Tangu siku hiyo, Shaaban hakuonekana tena, ingawa jitihada za kumtafuta zilifanyika kwa nguvu sana kwa usimamizi wa jeshi la polisi.
Katika eneo la malisho, mbuzi alioondoka nao Shaaban walionekana wakiwa katika idadi kamili lakini mtoto huyo ndiye hakuonekana.
Siku nne baadaye, Shaaban alikutwa akiwa amefariki dunia na mwili wake ulikutwa ndani ya kisima katika Mtaa wa Mbugani, Geita.
Baada ya kujiridhisha kwamba amefariki dunia na wazazi wake kumtambua kwamba ni mtoto wao, alizikwa katika makaburi ya eneo la nyumbani kwao.

SHAABAN ALIFUFUKAJE?
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mama mzazi wa mtoto huyo, Aziza Ramadhani, 45, ambaye alisimulia jinsi alivyoweza kumuona mtoto wake huyo akiwa hai.
“Ilikuwa Septemba 30, mwaka huu, nilikuwa naelekea sokoni kwenye shughuli zangu za kuuza mbogamboga. Ilikuwa saa 1.30 asubuhi, nikiwa Mtaa wa Nyankumbu, nilikutana na mwanangu Shaaban.
“Nilishtuka na sikuamini haraka. Nilimwita kwa jina lake, mwanangu Shaaban ni wewe? Akaniitikia kwa kutikisa kichwa. Hakuweza kutoa sauti vizuri, alikuwa anazungumza kwa taabu.
“Nilikwenda kumshika mkono kuhakikisha kuwa ni binadamu au mzimu huku nikiwa siamini kabisa kuwa ni yeye. Nilipoona kuwa ni yeye nilimpigia simu mume wangu, akaja tukamchunguza vizuri na kubaini kuwa kweli ni mtoto wetu Shaaban.
“Ni maajabu kabisa, sisi tuliamini amekufa na tukamzika miaka miwili iliyopita. Kweli hii dunia ni ya maajabu,” alisema Aziza ‘Mama Shaaban’.
Aliendelea kusema kuwa mtoto huyo alikuwa na alama ya kinundu kwenye paji la uso na mguuni ambalo ni kovu iliyosababishwa na kuchomwa na mwiba. 
Aliongeza kuwa vilevile Shaaban alikuwa na mwanya uliofanana na wa baba yake ambapo huyu alama zote hizo anazo.
Alisema kuwa walikagua alama hizo kipindi cha kuutambua mwili wake pale alipofariki dunia na kujiridhisha ndipo walipomzika.
“Baba yake alipokuja eneo la tukio, tulimpeleka hospitali kwa sababu hali yake haikuwa nzuri, mpaka sasa bado yupo hospitali akitibiwa,” alisema Aziza.

SHULENI KWAKE NAKO
Mtoto huyo aliyevuta hisia za watu wengi mjini Geita, amethibitishwa na walimu wake katika shule aliyokuwa anasoma kwamba ndiye aliyezikwa.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mwatulole, Geita, Joseph Nungula, alisema kuwa amemwangalia Shaaban na kujiridhisha ni mwanafunzi wake yuleyule ambaye miaka miwili iliyopita zilitolewa taarifa za kifo chake na baadaye kuzikwa.
“Nimemtambua mtoto huyo kwa sura na alama, hasa ya usoni na alikuwa na mahudhurio mazuri shuleni. Pia maendeleo yake kitaaluma yalikuwa mazuri,” alisema mwalimu huyo huku akiungwa mkono na wanafunzi waliokuwa wanasoma na Shaaban.

BABA ANAZUNGUMZA
Maulid Shaaban ‘Baba Shaaban’, alisema kuwa ni kweli kabisa mtoto wao alitoweka na alipatikana akiwa ameshafariki dunia.
Aliongeza, mwili wa Shaaban ulikutwa ndani ya kisima cha maji, hivyo walitoa taarifa polisi kisha waliruhusiwa kuchukua mwili.
“Daktari alithibitisha alimkagua na kujiridhisha kwamba ameshakufa. Tukaamua kumzika kwenye kiwanja cha nyumbani kwangu, Kitongoji cha 14, Kambarage, hapa Geita.
“Shughuli zote za matanga tulifanya, baada ya hapo hatukuwa na wazo la Shaaban kurudi duniani. Leo hii kila kitu tunaona ni maajabu, Shaaban huyuhuyu ambaye tulimzika amerudi duniani,” alisema Maulid.

DAKTARI AELEZA
Shaaban amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, akifanyiwa uchunguzi zaidi na matibabu zaidi kwa sababu bado hajaweza kuzungumza vizuri.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Geita, Dk. Adamu Sijaona anayemtibu mtoto huyo, alisema kuwa tayari wazazi wake wameshachukuliwa sampuli na kuhifadhiwa kwenye maabara na mifupa iliyokutwa kaburini imechukuliwa kwa uchunguzi wa DNA.
“Hali yake inaendelea vizuri hasa katika kutamka maneno ikilinganishwa na wakati anafikishwa hospitalini kwa mara ya kwanza kwa sababu alikuwa hawezi kutamka neno hata moja,” alisema Dk. Sijaona.

OFISI YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI
Mchunguzi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Ziwa, Lukas Nduguru, aliliambia gazeti hili kuwa wamechukua vipimo vya wazazi na mtoto pamoja na baadhi ya mabaki ya mifupa iliyokuwa kwenye kaburi hilo kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili kubaini mwili wa nani ulizikwa kwenye kaburi hilo.
“Ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ilipata taarifa za huyo mtoto aliyezikwa mwaka 2011 kwamba ameonekana akiwa hai, kwa hiyo majibu ya vinasaba yatatoka ndani ya siku 14 au mwezi mmoja.
“Tuna changamoto za kukatika umeme mara kwa mara, kwa hiyo ndani ya kipindi hicho tutakuwa tumekamilisha,” alisema Dk. Ndunguru.

NENO LA KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo, mbali na kuthibitisha kufukuliwa kwa kaburi hilo kwa kibali maalumu cha mahakama, alisema mtu hawezi kufa kisha kufufuka kwa hiyo jeshi la polisi haliamini kama mtoto aliyezikwa ni yeye.
“Unajua hatuna imani na hili isipokuwa tunasubiri majibu ya uchunguzi wa watalaamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali,” alisema Paulo.

NI TUKIO LA PILI GEITA
Tukio kama hilo ni la pili kutokea katika Wilaya ya Geita katika kipindi kisichozidi miezi mitano ambapo Aprili 12, mwaka huu, mwanamke aliyetambulika kwa jina la Flora Onesmo, 45, aliyefariki dunia Februari 28, 2008 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kisha kuzikwa katika Kijiji cha Nakasenya, Kata ya Butundwe, alionekana akiwa hai.
Flora, alikutwa hai Aprili 12, mwaka huu, akiwa ameketi nje ya nyumba ya dada yake aitwaye Monica James, anayeishi Kijiji cha Kasamwa, Geita.

UWAZI LIPO KAZINI

Uwazi bado lina kazi ya kufanya kuhusiana na Shaaban na Flora, yapo maswali mengi hayajajibiwa, kwa hiyo lipo kazini likiibuka litakuwa na mengine mengi ambayo pengine yatakuwa mazito zaidi. MHARIRI

Source:Global publishers

Udaku Specially Blog

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. shigongo kwa uongo namuaminia? kuna siku aliniandika eti nimefumaniwa na mume wa mtu wakati hata sikuwepo dar.

    ReplyDelete
  2. This is true uckalili wewe!

    ReplyDelete
  3. yaan nikishaona source gpl ccomi hata hyo habari yenyeww

    ReplyDelete
  4. Haya ndiyo Watz yanatupotezea muda, haiwezekani mtu kufufuka

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad