Nairobi. Picha zilizonaswa kupitia kamera za CCTV zilizofungwa kwenye jengo la kibiashara la Westgate Mall mjini Nairobi zinaonyesha kwamba magaidi waliovamia jengo hilo walikuwa wanne, hivyo kuanza kuibua mtizamo mpya kuhusu magaidi waliovamia jengo hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, taarifa hizo ambazo bado si rasmi kutoka kwa mmoja wa maofisa wa juu wa Serikali ya Kenya juzi, zilieleza kwamba watu wanne wakiwa na silaha za kisasa ndio walioonekana kupitia kamera hizo za siri, hivyo kuanza kuwepo kwa uwezekano wa kupungua kwa idadi ya awali ya watuhumiwa hao wa ugaidi waliovamia jengo hilo.
Awali, Serikali ya Kenya ilieleza kwamba wavamizi hao ambao walijitambulisha kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab la Somalia waliotekeleza uvamizi huo Septemba 21, walikuwa kati ya 10 hadi 15 na kusababisha vifo vya watu 67, idadi ambayo imeanza kutiliwa walakini.
Kati ya waliouawa, kwa mujibu wa taarifa za Serikali, walikuwemo wanausalama sita, watatu wakiwa maofisa usalama wa jeshi na watatu wakiwa maofisa usalama wa polisi ambao waliuawa kwati wa kujibizana risasi walipokuwa wakijaribu kuwadhibiti wavamizi hao.
Taarifa hizi zimeanza kuvuja wakati wataalamu wa masalia ya miili ya binadamu wakiendelea kufanya uchunguzi kwenye mabaki ya miili ya watu waliokuwa wamenasa kwenye vifusi vya jengo hilo.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, tayari vijana kadhaa wameshakamatwa kwenye eneo la watu wa makazi duni la majengo mjini Nairobi, kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano kama sehemu ya polisi kujaribu kuwanasa wavamizi hao ambao kwa mujibu wa taarifa za awali, walifanikiwa kutoroka kupitia mtaro wa maji machafu unaotoka kwenye jengo hilo.
Udaku Specially Blog
MAPYA YAANZA KUIBUKA UVAMIZI WA WESTAGATE MALL NAIROBI
0
October 06, 2013