Fundi huyo alisema Ufoo alifika katika eneo wanalofanyia kazi akiwa amejishika tumbo kama mtu mwenye maumivu na kumuomba amsaidie kupata usafiri utakaomfikisha Hospitali ya Tumbi.
Kibanda hicho kiko meta kama 100 kutoka nyumbani kwao na inadaiwa alikimbilia hapo kujiokoa.
“Alikuja na kunieleza huko nyumbani kumeshaharibika, akilalamika kuwa amepigwa risasi na hajui ndugu zake wapo katika hali gani kwa kuwa muuaji bado alikuwa akizungukazunguka ndani ya nyumba,” alisema fundi huyo.
Alisema ilikuwa ngumu kwao kuendelea kumhoji kutokana na hali aliyokuwa nayo Ufoo kwa wakati huo.
“Hata yeye baada ya kuona tunamuuliza sana maswali, aliingia katika moja ya chumba cha duka (anamuonesha mwandishi
hicho chumba) na kukaa katika kiti, huku akiugulia maumivu a nilichokifanya ni kusimamisha pikipiki na kumwagiza dereva ampeleke kwanza Kituo cha Polisi Mbezi Mwisho, ili apatiwe PF 3. Ufoo alitaka apelekwe hospitali moja kwa moja,” aliongeza.
Anasema ilibidi wakubaliane na matakwa ya Ufoo na pikipiki hiyo ilimbeba na kuondoka naye kwenda hospitali.
Baada ya Ufoo kuondoka, anasema alikwenda katika moja ya nyumba iliyopo jirani na nyumba ya akina Ufoo na kumuita mmoja wa jirani aliyemtaja kwa jina la Ustaadhi, na kumuuliza kama anajua suala lolote linaloendelea katika eneo hilo.
Jirani huyo alikiri kusikia milio ya risasi kutoka katika nyumba bila kujua ni ya nini. Ndipo alipomueleza kuhusu Ufoo kupigwa risasi ambapo wote kwa pamoja waliamua kusogea jirani kujua kinachojiri.
“Hatukuingia ndani kwa kuhofia usalama wetu, tulisimama kwa mbali na kuangaza huku na huko, lakini kwa mbali tulimuona mama yake Ufoo akiwa amelala chini. Polisi walipofika ndipo nasi tukapata ujasiri wa kuingia na kukuta mauaji hayo,” alisema.
Ufoo bado yuko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Huku akionyesha uchovu na kusikia maumivu baada ya kufanyiwa operesheni juzi, alizungumza kwa tabu na kusema; “Sijambo naendelea vizuri.”
Mwili wa marehemu mama Anastazia unatarajiwa kuagwa nyumbani kwake leo saa 5 asubuhi. Saa 7 mchana umepangwa kupelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kibwegere kwa ajili ya ibada kabla ya kuanza safari ya kwenda Moshi baadaye leo kwa ajili ya maziko yaliyopangwa kufanyika katika kijiji cha Shali, Machame mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati wa kikao cha ndugu wa marehemu kilichofanyika kwenye Ukumbi wa 92 jijini Dar es Salaam jana, Silver Mushi kaka wa marehemu alisema Anthery na Ufoo walikuwa wanapendana na jamaa zake wameshtushwa na taarifa za mauaji h ayo kwani hawakuwa na taarifa zozote za mzozo baina yao, “Siwezi kusema kuwa walikuwa wachumba kwani katika mazingira yetu ya Kiafrika kuwa na mwanamke kwa miaka 10 hadi kuzaa mtoto mwenye umri mkubwa kama huo ni wazi kuwa nyie mna zaidi ya uchumba,” alisema na kuongeza kuwa bado hawajaamua siku hasa ya kusafirisha mwili wa marehemu kwa ajili ya maziko huko Ongoma, Kata ya Uru, mkoani Kilimanjaro.
Mushi alisema pia kuwa marehemu alikuwa anakaribia kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Masuala ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu Huria nchini India.
Watu waliokuwa wakifanya kazi na Mushi kwenye Operesheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Kimataifa (UNAMID) huko Darfur, Sudan wameeleza kusitushwa na alichokifanya mfanyakazi mwenzao, Mushi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu jana, watu hao ambao waliwahi kuishi na Mushi wakiwa kwenye shughuli zao Darfur, walisema marehemu alikuwa na tabia ya upole, mcheshi na mchapa kazi.
Mfanyakazi mwenzake, ambaye ni raia wa Tanzania, ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa sio msemaji rasmi wa UNAMID, alisema hakuwahi kusikia Mushi akinung’unika kuhusu masuala ya maisha yake. Alisema pia mara nyingi, Mushi alikuwa akiwasiliana na mzazi mwenzake Ufoo nyakati za jioni. Walikuwa wakiwasiliana zaidi kwa njia ya mtandao wa intaneti.
“Kwa jinsi nilivyowaona kwa kweli walikuwa wanapendana sana. Kila mtu haamini kama kweli Mushi amefanya kitendo hiki cha kumpiga risasi Ufoo na kumuua mama mkwe wake,” alisema Mtanzania huyo kwa masikitiko makubwa.
Pia Mushi alikuwa anasifiwa kutokana na uwezo wake wa kufanya vitu vingi kiasi cha kupewa jina la utani la ‘multi talented’ (mwenye vipaji vingi).
“Mushi akiwa hapa UNAMID alikuwa kama mtaalamu wa mawasiliano lakini kumbuka huko nyuma aliwahi kuwa mpiga picha wa vituo vya televisheni vya ITV na TBC,” aliongeza raia huyo wa Tanzania, ambaye waliishi nyumba moja katika Mji wa El-Jeneina huko Darfur, Magharibi mwa nchi ya Chad.
Mushi pia alikuwa ana sifa ya kupenda kula vyakula aina ya mboga na alikuwa analima bustani. Mfanyakazi mwingine wa UNAMID, ambaye ni raia wa Nigeria mwenye cheo cha Kanali, alisema Mushi alikuwa akilima mchicha, kabichi, bamia na mboga za majani ya maboga kwenye eneo la nyumba yake huko Darfur.
Udaku Specially Blog