Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, imevikataa viwango vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya sekondari vilivyotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu na kutaka utaratibu na alama zilizotumika mwaka jana, zitumike kupanga matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka huu.
Serikali ilitangaza utaratibu mpya wa alama za Mitihani ya Kidato cha Nne na Sita kwa kufuta Daraja la Sifuri na kuleta Daraja la Tano.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen Ngonyani alisema jana kuwa kamati hiyo ilichukua uamuzi huo kwa kuwa pamoja na udhaifu ulio kwenye alama hizo, kamati yao haikuhusishwa katika mchakato wa kuandaa alama hizo.
“Mwenyekiti wangu (Margaret Sitta) alisema kile hakiwezekani, kuna viwango ambavyo wameleta havipo kwenye nchi nyingine duniani, tumewaambia wakavifanyie kazi walete tena,” alisema mbunge huyo wa Korogwe Vijijini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Profesa Maji Marefu.
Ngonyani alisema waliagiza watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha wanaishirikisha kamati yao kwani imejaa walimu wanaoweza kushauri vizuri.
“Hatutaki watuletee mambo ambayo yamewashinda baada ya kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Ngonyani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome akitangaza uamuzi huo mapema mwezi huu, alisema uamuzi wa kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka 2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha Nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34 kwa upande wa Kidato cha Sita, A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho ulitarajiwa kuwa na alama 60 na alama 40 zitokane na alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni (Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya Serikali kufuta matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa mwisho ukiwa na alama 70.
Wadau wa elimu na wabunge walipinga vikali utaratibu mpya wa alama za mitihani hali iliyofanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuamuru wizara husika kupeleka bungeni taarifa yenye maelezo juu ya uamuzi huo.
Kabla ya Serikali kutoa kauli yake, watendaji na viongozi wa Wizara ya Elimu walikutana na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Mjini Dodoma mwezi huu ambapo wajumbe wa kamati hiyo walikataa viwango hivyo vipya na kuitaka wizara kuendelea kuvifanyia kazi viwango hivyo kwa kuishirikisha Bodi ya Necta.
Mjumbe mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho alisema hoja kuu zilizosababisha kukataliwa kwa alama hizo ni ile iliyosemwa kuwa ni kushusha sana viwango vya ufaulu, pia kutaka shughuli hiyo ifanywe kwa kushirikisha Bodi ya Necta ambayo kisheria ndiyo yenye jukumu la kutunga sera za mitihani.
“Tulichosema ni kuwa viwango vya ufaulu pamoja na utaratibu uliotumika mwaka jana, viendelee kutumika kwa mitihani ya kidato cha nne inayoendelea kwa sababu viwango vipya vimekosa uhalisia,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe hao walisema haiwezekani ufaulu wa A ukaanzia 75 wakati hakuna nchi duniani yenye A ya namna hiyo, pia haiwezekani 20 ikahesabika pia kama ufaulu.
“Pia ukiangalia, Kifungu cha Nne cha Sura ya 10 ya Sheria ya Necta kinasema kuwa taasisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kutengeneza sera ya mitihani,” alisema mjumbe huyo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema bungeni kuwa daraja sifuri litaendelea kuwapo lakini hakuzungumzia chochote kuhusu alama ambazo kamati ilishauri wizara hiyo izifanyie kazi.
Mulugo ambaye ndiye aliyehudhuria kikao hicho hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, iliita bila kupokewa.
Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyanzu alisema kwamba hana taarifa za maagizo hayo ya kamati hiyo.
Ufaulu wa chini
Kwa mujibu wa kitabu kinachoonyesha viwango vya ufaulu duniani kila mwaka cha International Qualification, baada ya Tanzania kutangaza alama hizo mpya, sasa inaongoza duniani kwa kuwa na alama za chini za ufaulu.
Nchi zinazofuatia kwa viwango vya chini baada ya Tanzania ni Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambazo hata hivyo, viwango vyake vipo juu kwa kiwango kikubwa vikilinganishwa na vile vya Tanzania.