Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Shaka alisema kitendo cha kiongozi huyo kukataa kuachia madaraka ya kisiasa na kulipisha kundi la vijana ni udikteta usio na mipaka ndani na nje ya Bara la Afrika.
Alibainisha kuwa inasikitisha kusikia kiongozi huyo akitangaza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani ilhali alishindwa mara nne katika chaguzi zilizofanyika miaka iliyopita.
“
Shaka aliongeza kuwa laiti Maalim Seif angelikuwa anaheshimu misingi ya demokrasia na kutambua umri wake asingeendelea kushiriki siasa kama alivyoahidi hivi karibuni kuwa hataacha siasa hadi aishiwe nguvu.
Shaka aliwataka vijana wa CUF kujiondoa katika chama hicho na kujiunga CCM ili waweze kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wa kushikilia nafasi za uongozi ambao sasa unahodhiwa na Maalim Seif.
“Tazameni CCM ilivyo, vijana tunapewa nafasi ili kuonyesha uwezo na vipaji vyetu kisiasa, mkibaki huko hadi mtazeeka hamtapata nafasi ili kuisaidia nchi yetu kimaendeleo,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM inaonyesha kuheshimu misingi ya demokrasia tangu utawala wa TANU na ASP, ambapo kulikuwa na mabadiliko mbalimbali ya viongozi wa ngazi za kisiasa na kiserikali, tofauti na vyama vingine ikiwamo CUF.
Alitolea mfano kuwa kwa upande wa Jamhuri ya Muungnano aliondoka madarakani Rais Julius Nyerere akampisha Ali Hassan Mwinyi ambaye alimuachia kijiti Benjamin Mkapa na sasa taifa linaongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, Rais wa Kwanza ni Abeid Aman Karume, akafuatia Aboud Jumbe Mwinyi aliyempisha Idris Abdul Wakil, baadaye Dk. Salmin Amour, akafuatia Dk. Amani Karume na sasa nchi inaongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.
Shaka alilaumu utendaji aliouita ni legelege, usio wa uwajibikaji na uadilifu kwa wizara ambazo ziko chini ya upinzani na kusema waliopewa dhamana za madaraka hayo wameshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Aliitaja Wizara ya Afya chini ya Waziri Juma Duni Haji kwamba haiwatendei haki wananchi huku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mambo ya utawala na utoaji wa huduma yakiendeshwa shaghalabaghala.
“Duni umepewa dhamana na Rais Shein ila hutimizi wajibu wako, hakuna huduma za kuridhisha Mnazi Mmoja, wafanyakazi, wauguzi na waganga wanalalamika, kutana nao, acha kuwakimbia,” alisema.