SIKU moja baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya marekebisho katika upangaji wa viwango vya alama za matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne na sita kwa kufutwa daraja sifuri na kuwekwa daraja la tano, wadau na wasomi wameponda mfumo huo.
Wakizungumza na gazeti hili, wadau hao walisema kuwa tatizo si kushuka kwa kiwango cha ufaulu, bali uwepo wa elimu bora nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema kuna mifumo miwili ya elimu nchini inayotumika, ambayo ni ule wa watu masikini na wenye nafuu ya maisha.
Alisema hali hiyo inaanzia chekechea hadi vyuo vikuu, huku akihoji wizara husika mfumo wa aina hiyo unamlenga nani, kwamba tatizo lililopo ni ubora wa elimu hasa katika shule za umma.
Bashiru alisema kwenye mifumo hiyo inayotumika, ule wa masikini upo kwenye shule nyingi za umma ambako ndiko kwenye watoto wengi wanaofeli kutokana na kukosa vifaa vya kufundishia, maabara na walimu.
“Katika shule za umma watoto wengi hawasomi, hawana maabara, sasa wizara inawatahini nini? Mageuzi yoyote ambayo yatashindwa kuondoa matabaka hayawezi kuleta elimu tunayoitaka,” alisema.
Alisema ubora wa elimu utawahusu wanafunzi hao wanaosoma shule za michepuo ya Kiingereza, kwani ndio watakaokuwa wanafaulu kwa kuwa shule zao zina mfumo mzuri unaoeleweka na viwango walivyojiwekea kama mwanafunzi hatafikia atarudia darasa ama kuachishwa shule.
Naye mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Prof. Herme Mosha, alisema kama wizara inataka kuongeza idadi ya watu katika ufaulu waliofanya mtihani, inapaswa kuboresha elimu.
“Sio mara ya kwanza tumechezea vigezo, 2007 tulibadilisha viwango tulivyokuwa navyo tukaweka alama za chini, wanafunzi wengi wakachaguliwa, matokeo yake mtihani wa mwisho wa kidato cha nne kukawa na matokeo mabaya,” alisema.
Alisema lililofanyika sio utatuzi wa tatizo, bali wizara iangalie nini kinasababisha ubora wa elimu kushuka.
Kwa mujibu wa Prof. Mosha, wizara husika iangalie ni nini kinachowafanya wanafunzi wasisome badala ya kupandisha viwango kwa aina hiyo waliyoitumia.
Dk. Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tatizo lililopo ni mfumo mbaya wa ufundishaji, kwani kupanga madaraja kwa aina hiyo si suluhu ya kutatua changamoto iliyopo.
Alisisitiza kuwa kwa staili hiyo, serikali haitoi tatizo bali inajaribu kuficha tatizo, hivyo hakuna cha kushangilia kwa mfumo huo walioutangaza.
Mwalimu wa sekondari, Josephat Ammy, alieleza kuwa mfumo huo utamfanya mwanafunzi kubweteka na kutochukulia umuhimu suala la elimu kwa kudhani kuwa uwezo wa kufaulu anao.
“Wao walitakiwa waje na suluhisho la elimu na kujua kwanini wanafunzi wanafeli, sasa wanachofanya nini? Wanaondoa daraja ziro halafu hao wa daraja la tano wanakwenda wapi?” alihoji.
Naye mmiliki wa shule za Green Acres, Julian Bujugo, alisema kuwa mfumo huo sio mbaya kwani wanafunzi watafanya mtihani kwa kutumia mitaala.
“Mfumo huu ulikuwepo hapo awali kabla ya kutolewa, sioni kama una ubaya. Ni mzuri, utasaidia kwa wanafunzi tofauti na mwaka jana walitunga mitihani ambayo haikuwa kwenye mitaala,” alisema.
Naye Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gracian Mukoba, alisema kuwa kubadilisha alama itakayowasaidia watoto wengi kuonekana wamefaulu haisaidii kwani ndiyo kwanza kunaongeza zao la ujinga.
Alisema kama walikuwa wanatafuta kufurahiwa na wazazi na wanafunzi, basi wangeweka alama A, B, C plus bila kuwa na alama hizo za daraja hadi la tano.
Kwa mujibu wa Mkoba, kilichofanyika ni siasa tu na kucheza na saikolojia za wazazi, ambazo tayari zimeathiriwa na mfumo mbaya wa elimu ambapo idadi kubwa ya watoto wanaofeli inaongezeka kila kukicha.
“Yaani hapa ni kama bomba, unakuta linatoa maji machafu ya tope. Baada ya kuangalia nini chanzo chake wewe unaamua kubadilisha koki na kuweka nyingine wakati si suluhisho,” alisema.
Mukoba alisema njia sahihi za kuboresha elimu serikali inazijua kwa kuwa tayari walishatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuunda tume, kufanya utafiti, hivyo majibu tayari wanayo.
Naye mwalimu wa vituo vya elimu ya Taasisi ya Watu Wazima, Stanslaus Sekuru, alisema kuwa mfumo huo utaboresha elimu kwa sababu hapo awali wanafunzi walikuwa wakiumia sana.
Alitolea mfano daraja la nne akisema mwanafunzi anakuwa na alama 26, lakini akiwa na alama C tatu anashindwa kuendelea na kidato cha tano na mwenye daraja la tatu mwenye alama 25 na C tatu yeye anapewa nafasi ya kuendelea.
Mwalimu Charles Mkwidu ambaye ni mratibu wa Kituo cha Elimu ya Watu Wazima, alisema mpango huo ni mzuri ila uwekewe mkakati wa kuwasaidia wanafunzi kupenda kusoma, hasa masomo ya sayansi kwani wengi husoma wakati wa mitihani tu.
Naye mwanafunzi anayerudia mitihani, aliyeathiriwa na matokeo ya mwaka jana, Jesca Charles, alisema huenda ikawasaidia au la kwa kuwa mitaala ya elimu ndiyo iliyowaponza hadi wakafeli.