Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyabiashara walio katika maeneo ya Kariakoo wamegoma kushiriki semina ya uelimishaji iliyokuwa itolewe na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) katika kile walichokiita kupuuza madai yao na kutaka kufanya vile wanavyotaka wao kuhusiana na sakata la mashine za kielektroniki za kukusanyia mapato.
Mamlaka hiyo iliitisha mkutano katika Hoteli ya Starlight ikilenga kuwaelimisha wafanyabiashara hao juu ya matumizi ya mashine za kielektroniki, jambo ambalo lilizua zogo miongoni mwa wafanyabiashara waliokuwepo katika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wafanyabiashara wa nguo eneo la Kariakoo aliyekuwepo hotelini hapo, akijitambulisha kwa jina moja tu la Mwanahamisi alisema siku ya Jumatano gari la matangazo lilipita baadhi ya mitaa ya Kariakoo likiwataka wafanyabiashara hao wafike kwenye mkutano uliopangwa kufanyika.
“Kutokana na taarifa hiyo kuletwa kienyeji, baadhi ya wafanyabiashara wachache tumefika tukijua tutapata ufumbuzi juu ya kilio cha muda mrefu kuhusiana na malalamiko waliyopeleka kwenye mamlaka hiyo, a alisema.
Matokeo yake watu kutoka mamlaka hiyo waliofika kwenye mkutano, walianza kutoa utambulisho juu ya kile walichotarajia kukifanya ikiwa ni kutoa elimu juu ya matumizi ya mashine hizo.
Gazeti la Mwananchi