KINANA AZIDI KUWABANA MAWAZIRI WAZEMBE WA SEREKALI

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amezidi kuwaweka kitanzini mawaziri na watendaji wa Serikali, kwa kusema kuwa wataanzisha operesheni ya kupambana na kuufumua urasimu na umangimeza uliopo kwenye baadhi ya wizara, ili kurudisha uwajibikaji kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Kinana amesema kuwa hayuko tayari kuona wananchi wakilalamika kukosa huduma za jamii huku viongozi waliopewa dhamana wakikaa ofisini na kunyonga tai.

Kinana, alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lupando, wilayani hapa, ambapo alisema ili kukomesha hali hiyo, CCM haitatishwa na mtu yeyote katika kusimamia maslahi ya wananchi.

Alisema ili kuweza kukabiliana na hali hiyo, Kamati Kuu ya chama hicho, imedhamiria kufanya mageuzi kwa kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kero zao kupatiwa ufumbuzi.

Hatua hiyo ya Kinana imetokana na malalamiko yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupando, Wema Mwaipopo, ambaye alisema kuwa tangu ulipopatikana Uhuru mwaka 1961, hawajawahi kupata huduma ya maji hali inayowafanya wajihisi wanyonge kwenye nchi yao.

Kutokana na hilo, Kinana alisema kuwa CCM haiwezi kuwa na viongozi waliopewa dhamana ya kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, huku wakikaa ofisini na kuvuta makaratasi na kupulizwa na viyoyozi katika magari.

“Kuanzia sasa tunakwenda katika Kamati Kuu na tutaanzisha kampeni ya kupambana na kuufumua uendeshaji wa Serikali kwa urasimu na umangimeza. Hili hapana na halina nafasi ndani ya CCM.

“Watu wanalalamika kukosa huduma ya maji wanaoingia mikataba na wakandarasi wameishia kukaa ofisini badala ya kwenda kusikiliza kero za wananchi, sasa tunasema tunaendelea kuwa wakali kwa chama chetu pamoja na Serikali zetu,” alisema Kinana.

Hata hivyo katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crisipian Meela alijikuta katika wakati mgumu baada ya kutakiwa kutoa maelezo ya kwanini mradi wa ujenzi wa maji umesimama huku wananchi wakikosa maelezo ya kutosha.

Akitoa maelezo mbele ya wananchi hao, Meela, alisema kuwa mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga mradi wa maji alivunja mkataba kwa kutoukamilisha kwa muda uliotakiwa.

DC Meela, alisema ilimlazimu kuvunja mkataba huo na kulazimika kuzuia Sh milioni 200 zilizowekwa na mkandarasi huyo.

“Mradi huu ulitengewa Sh bilioni 4.7, lakini zilizotumika ni Sh bilioni moja, wakati mradi huu ulianza mwaka 2011, lakini bado umekuwa ukisuasua kwa kutokamilika kwa wakati,” alisema DC Meela katika majibu yake.

Hata hivyo majibu ya DC huyo, yalionyesha wazi kutomfurahisha Kinana, ambapo alisema kuwa wananchi hawataki kusikia maelezo ya kukwama kwa mradi ila wanataka kujua lini watapata maji.

“Muungwana ni vitendo kwa kuwa mradi huu pamoja na barabara uliahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, ninachotaka kuwaambia ni lazima utakamilika kabla hajaondoka madarakani,” alisema Kinana.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kwani Kinana ndo nani. Ifahamike kwamba kiongozi wa chama si kiongozi wa serikali. Hawa akina Kinana, mwigulu nchemba na nape nnauye wamezidi kujifanya wao ndo serikali na nchi. kama ni madaraka yao wayafanye kwenye ccm si serikalini. utendajui wa mawaziri hauwahusu viongozi wa ccm. mawaziri wanawajibika kwa rais ambaye ndo mkuu wa serikali

    ReplyDelete
  2. Naomba kama huelewi ni afadhari ukanyamaza.Serikali inaendeshwa na chama gani. Rais alisimama kwa chama gani.ni lazima alisimamishwa na chama fulani na alipopita ndion ikawa rais kupitia chama hicho.Ukinyamaza watu hawataelewa ujinga wako.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad