MAWAZIRI WATATU WAZEMBE SERIKALI YA CCM KUWAJIBISHWA...

Mawaziri watatu wanatakiwa kuwajibishwa kutokana na kushindwa kutatua kero za wananchi, imeelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye  kwenye mkutano wa hadhara mjini hapa.
Nape alisema ni lazima wawajibishwe na chama kwa mujibu wa sheria kutokana na kulalamikiwa na wabunge na wananchi kwa alichosema ni kushindwa kusimamia wizara zao.

Alisema mawaziri hao watawekwa ‘kitimoto’ katika kikao kijacho cha Kamati Kuu (CC) ya CCM,   mwezi ujao ambapo watatakiwa kujieleza kwa nini wameshindwa kutatua kero za wananchi na muda mwingi wanautumia ofisini.
Nape alimtaja Waziri (jina linahifadhiwa)  ambaye kila wizara aliyopewa kusimamia ameshindwa kuonesha ufanisi katika kutatua kero za wananchi.
Nape alisema hakuna sababu ya kukaa kimya wakati mawaziri hao wanashindwa kufanya kazi ambayo wanastahili kuifanya, ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazohusu wananchi na ni lazima wawajibishwe ili kuokoa chama.
Alisema baadhi ya mawaziri tangu wateuliwe wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuongoza wizara zao, kwani hakuna siku waliyofika mkoani Ruvuma kushughulikia matatizo ya wananchi.  Mawaziri hao wameshindwa kutembelea mkoa huo na kutatua kero mbalimbali zikiwamo za pembejeo za kilimo na mbolea ya ruzuku ambayo wananchi walilalamika kwamba hazifiki kwa wakati.  
Hivi sasa kuna kero zinahusu wakulima mkoani hapa na nyingi kati zinahusu sekta ya kilimo huku viongozi wenye dhamana wakishindwa kuchukua hatua za kuwasaidia.
“Katibu Mkuu leo naomba unisamehe mzee wangu, sasa umefika wakati wa kufika mwisho, ni bora niseme haya mchana kweupe kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Nape na kuongeza kuwa wapo mawaziri wenye dhamana ya kutumikia Watanzania lakini hawafanyi hivyo. 
“Nimeuliza hapa walishawahi kufika mara ngapi kushughulikia matatizo ya wananchi hali ya kuwa hapa ndipo katika ghala la Taifa ambalo linalisha nchi nzima, lakini jibu lake hakuna hata siku moja wamefika,” alisema Nape. 
Viongozi hao wamekuwa hawafiki Ruvuma kutatua kero zinazowakabili wananchi zikiwamo za kukosa  pembejeo kwa wakati na wanapata kidogo wakati mahitaji yao ni makubwa.
Kutokana na hali hiyo, Nape alisema yuko tayari kupoteza nafasi yake lakini hawezi kuvumilia hali hiyo ikiendelea na alitumia nafasi hiyo kumwomba Kinana ahakikishe wanachukuliwa hatua na chama.
Alitoa mfano kuwa karibu Tanzania yote wakulima wana matatizo mengi na wamekuwa wakilalamikia wizara hiyo na yeye ni shahidi wa hayo yanayoendelea kutokea na ili kukinusuru chama ni lazima mawaziri walioshindwa kazi wawajibishwe.“Wananchi naomba mnilinde, lakini niseme ukweli…mawaziri ambao tumewapeleka jikoni wameshindwa kupika chakula, tunasubiri sebuleni lakini chakula hakiji sasa natamka wazi wanatukwamisha ni bora wakaondoka kama wameshindwa kazi.
“Katibu Mkuu siko tayari kuona CCM inakuwa chama cha upinzani bungeni kwa sababu ya hawa wenzetu wachache ambao wanafanya makusudi na uzembe katika kutekeleza wajibu wao,” alisema Nape.
Alisema mmoja wa mawaziri anatakiwa kuchukuliwa hatua kutokana na mkataba alioingia na wakandarasi wa ujenzi wa barabara ya Namtumbo-Tunduru mkoani Ruvuma yenye umbali wa kilometa 187.
Nape alisema Waziri huyo aliingia mkataba na kuipa kazi ya ujenzi kampuni ya Progressive ambayo imeshindwa kazi ya kujenga barabara hiyo.
Kutokana na hali hiyo alimshukuru  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kwa kumfukuza mkandarasi huyo ambaye alikimbilia mahakamani, lakini haki ilitendeka akashindwa kesi mara tatu.
Pamoja na kumfukuza mkandarasi huyo haitoshi, huku akitaka aliyehusika kumpa mkataba, naye anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Uchunguzi unaonesha kuwa mkandarasi huyo alishindwa kujenga barabara kwingine na alipewa mkataba mwingine na Waziri huyo.
“Amekuwa akitukwamisha CCM katika kutimiza wajibu wake. 
Hii barabara ya Namtumbo-Tunduru kushindwa kukamilika, imeleta aibu kubwa na kututia fedheha, hivyo lazima waliotoa mkataba huu akiwamo yeye wawajibishwe.
Alisema ikiwa mawaziri hao watashindwa kuwajibika kwa mujibu wa sheria, CCM itatumia wabunge wake kuandaa azimio la kuwafukuza kazi.
Akijibu hoja hizo Kinana, alisema katika kikao kijacho cha Kamati Kuu mwezi ujao chama kitamwandikia barua Rais Jakaya Kikwete ili mawaziri waje wajieleze kwa nini wasifukuzwe kwa kushindwa kazi.
“Hatuwezi kuwa na Serikali ya walalamikaji, Mkuu wa Wilaya analalamika, mbunge analalamika, hali hii imenishangaza sana sasa ni lazima tuchukue uamuzi mgumu wa kuwawajibishana,” alisema Kinana.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad