CHADEMA WAMJIBU NAPE, WAMTAKA MSAJILI WA VYAMA AMPUUZE

Siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kushindwa kusimamia katiba yake na kutofanya uchaguzi wa ndani kwa zaidi ya miaka 10, chama hicho kimesema hakijawahi kwenda kinyume na katiba yake na kinachozungumzwa na Nnauye ni uzushi wa kisiasa unastahili kupuuzwa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema jana kuwa katika miaka 10 iliyopita chama chao kimefanya uchaguzi mara mbili kila baada ya miaka mitano kama katiba inavyoelekeza.

Chadema tumefanya uchaguzi mkuu wa ndani 2004 na 2009, mara baada ya kipindi cha miaka mitano kupita ya muda wa kawaida wa uongozi. Madai kwamba hatujafanya uchaguzi kipindi hicho hayana msingi,” alisema Mnyika.

“Msajili wa vyama vya siasa anapaswa kupuuza kauli hiyo ya Nape na CCM na kurejea Katiba ya Chadema ambayo ofisi yake inayo nakala yake.”Ni vyema msajili akaikemea CCM kwa kufanya siasa chafu za uongo na uzushi,” alisema.

Aliongeza: “Kauli ya Nape na CCM ni ishara ya chama hicho kutishwa na namna ambavyo Chadema kinajipanga kuanzia ngazi ya chini kujenga uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti mijini na vijijini kuanzia ngazi za chini kupitia Programu ya Chadema ni Msingi.”

Mnyika alisema Nape na CCM wanajaribu kupotosha umma unaounga mkono vuguvugu la mabadiliko (M4C) kupitia Operesheni za Kanda na kazi nyingine zinazoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kamati Kuu ya Chadema itafanya mkutano wake wa kawaida kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 20 mpaka 21.

Ajenda za mkutano ni kupokea, kujadili na kufanya uamuzi mihutasari ya mikutano iliyopita na yatokanayo na mikutano hiyo, taarifa ya hali ya siasa na ripoti ya fedha.

Ajenda nyingine ni pamoja na taarifa kuhusu mchakato na maudhui ya mabadiliko ya katiba, taarifa ya utekelezaji wa Programu ya Chadema Msingi na shughuli za Kanda na taarifa ya utekelezaji wa Mpango Mkakati kuhusu maboresho.
-Mwananchi
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Haya wapishi 2015 ndiyo hiyo inakuja sasa! vijembe,ngonjera na hadithi nyingi za kusadikika tutazisikia.suala ni moja tu kila mtu anataka kula na chakula chenyewe kidogo..kazi ipo........TAFAKARI CHUKUA HATUA

    ReplyDelete
  2. Nap asipo ongea chochote cjui anajisikiaje.? Kama huna lakuongea si ujaribu kufanya kazi zingine.? Maana unalopoka lopoka tu.

    ReplyDelete
  3. na kitajifuta chenyewe si unaona wanavyorumbana wenyewe kwa wenyewe

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad