SIMBA YAJIBU MAPIGO YANGA-WASAJILI WAWILI FASTA FASTA

YANGA walicheka baada ya kumsainisha kiungo, Hassan Dilunga wa Ruvu Shooting aliyekuwa akinyatiwa pia na timu za Simba na Azam FC.

Mpaka sasa Yanga imewasajili wachezaji wawili katika dirisha dogo akiwamo kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja.

Lakini kama kawaida, Simba imesawazisha na kusajili wachezaji wawili wa haraka haraka.

Jana Jumapili, Simba ilianza usajili kwa kishindo cha aina yake baada ya kuiliza Mtibwa Sugar na kumuacha kocha, Mecky Maxime, akitokwa jasho na kufura hasira.

Simba ililipa tiketi ya ndege kutoka Zanzibar ili kuileta Dar es Salaam ‘injini’ na kiungo wa Mtibwa, Awadh Juma na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Kama hiyo haitoshi mchezaji huyo amesaini sambamba na straika Badru Ally aliyekuwa akiichezea Canal Suez ya Cairo, Misri.

Wachezaji hao wote wako kwenye timu ya Taifa ya Zanzibar iliyopiga kambi kwenye hoteli ya Bwawani mjini Unguja ikijiandaa kwa Kombe la Chalenji.

Awali, Badru ambaye yuko Dar es Salaam kwa miezi sita sasa, alikuwa akifanya mazoezi binafsi. Alifanya mazungumzo ya kujiunga na Azam FC lakini wakashindwana kwa kile kilichodaiwa kuwa mchezaji huyo alitaka dau kubwa.

Usajili wa Badru unamaanisha kwamba Zahoro Pazi na Sino Agustino ambao walishindwa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, sasa wana hali tete zaidi na watalazimika kukesha mazoezini ili kupata namba. Awadh ambaye ni kiungo mshambuliaji aliyeacha majonzi Mtibwa,  huenda akaingia kirahisi kwenye kikosi cha kwanza kwa vile kocha Abdallah Kibadeni ana shida ya mchezaji wa aina yake.

Badru alisema: “Nimesaini Simba kwa mkataba wa miaka miwili, nikiwa straika, lengo langu ni kuipigia Simba mabao hadi klabu ifurahi.

“Nimesajili Simba kwa sababu ni klabu ambayo nina mapenzi nayo kwa muda mrefu, hilo nitaridhihirisha kwa vitendo wenyewe wataona na hawatajutia kunisajili.”

Kuhusu Azam alisema: “Nilifanya mazungumzo nao, lakini tulishindwa kufikia makubaliano.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad