TBS WAHAHA PAMOJA NA KUPIGA VITA CHUPI ZA MITUMBA ILA BADO ZINAUZWA KAMA NJUGU..NANI ANAZIINGIZA NCHINI?

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabishara wa nguo za ndani kutoa ushirikiano kwa shirika hilo mahali wanakozipata nguo hizo zilizopigwa marufuku kwa kuwa kila mara linapofanya ukaguzi bandarini hazionekani. TBS imetoa wito huo kutokana na malalamiko ya baadhi ya wafanyabishara wadogo ambao wamelitaka shirika hilo kuwabana waingizaji wakuu wa nguo hizo za ndani badala ya kuwabana wao.

Malalamiko hayo yametolewa baada ya TBS kuanza msako wa nguo hizo katika masoko ya Tandika na Temeke Stereo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na RAI Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema mara nyingi shirika hilo limekuwa likifanya ukaguzi bandarini lakini nguo hizo za ndani hazionekani.

Roida alieleza kushangazwa na kitendo cha nguo hizo kuonekana mitaani wakati ukaguzi unapofanyika bandarini hazionekani.

“Tumekuwa tukifanya ukaguzi mara kwa mara lakini hatuzioni hizo nguo… sasa kinachotushangaza ni kitendo cha nguo hizo kuonekana mitaani.

“Sasa hawa wafanyabiashara wanatakiwa watupe ushirikiano… watueleze wanakozipata hizi nguo ili sisi tufuatilie na tuwachukulie hatua wahusika,”alisema.

Awali baadhi ya wafanyabiashara wadogo walilitaka shirika hilo kuwazuia waingizaji wakuu wa nguo hizo nchini badala ya kuwaonea wao.

Mmoja wa wafanyabiashara wa nguo hizo za ndani, Ali Mohamed aliitaka TBS kuwadhibiti kwanza waingizaji wakuu wa bidhaa hizo na si wauzaji.

“Ingawa TBS wanasema nguo hizi hazina ubora na kututaka tusiziuze, lakini kwangu mimi naona wanatuonea kwa sababu hii ni moja kati ya biashara yangu na inaniingizia kipato kinachonifanya niendeshe. Nikiacha kuuza nitafanya biashara gain?” alihoji mfanyabiashara huyo.

Alilishauri shirika hilo kutumia busara kwa kuzungumza na kujadili nini kifanyike na si kuwadhalilisha kama vibaka.

Mfanyabiashara mwingine, Peter Msangija alisema haki ya kufanya biashara nchini haipo.

Alisema yeye na wenzake wamekuwa wakijaribu kila biashara kwa lengo la kujikwamua na umasikini lakini wanakatishwa tamaa na baadhi ya viongozi wa serikali.

Msangija alisema ni vema Serikali ikatumia njia mbadala ambayo inataka watu wa aina gani katika biashara na si kuacha biadhaa ziuzwe kwa miaka mingi ndiyo izipige marufuku.

“Biashara ya nguo za ndani za mitumba tumekuwa tukiifanya kwa muda mrefu. Serikali yenyewe ndiyo iliruhusu uingizwaji wa bidhaa hii.

“Leo hii wanapiga marufuku sisi wanyabiashara wadogo tusiuze wakati huohuo wauzaji wa jumla wanauza tufanye biashara gani? Tumechoka kuonewa!” alisema Msangija.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad