Dar es Salaam. Wakati Msemaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi), Jumaa Almasi akisema hali ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi imeanza kuimarika, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amedai kwamba bado hajapata fahamu.
“Hali yake inatia matumaini, ingawa bado hajapata fahamu lakini madaktari wanaomtibu wameeleza kuwa anaendelea vizuri. Nami nakubali kwa sababu hali aliyokuwa nayo juzi ilikuwa tofauti, kwa kuwa najua kusoma mashine za kupumulia, inaonyesha mapigo yake yanakwenda vizuri,” alisema Mbatia kauli ambayo inapingana na ile ya Almasi ambaye alisema jana kuwa:
“Hali yake imeanza kuimarika ingawa bado yupo ICU, ameanza kuzungumza ingawa kwa shida, lakini hamuwezi kumwona kwa kuwa madaktari wameshauri kwamba anatakiwa kupumzika.”
“Tunajua kwamba Mvungi ni mtaalamu wa masuala ya sheria, ni kiungo muhimu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tunashukuru masheikh na wanazuoni waliofika kumjulia hali. Mapadri pia wamefika na kumwombea, lakini bado tunahitaji kuendelea kumwombea zaidi,” alisema Mbatia.
Alisema pia wanaridhishwa na hatua za kuwasaka watuhumiwa ambazo zinafanywa na vyombo vya ulinzi, ahadi iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliofika kumjulia hali.
Dk Mvungi alijeruhiwa usiku wa kuamkia juzi, baada ya kukatwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Dar es Salaam.
Asimulia mkasa
Akisimulia mkasa huo, mjukuu wa Dk Mvungi, Doris alisema babu yake alikabiliana na watu waliovamia nyumbani kwake na kumwumiza mmoja wao kabla ya kuzidiwa na watu hao.
Alisema jana kuwa babu yake alimjeruhi mmoja wa watu hao usoni kwa kitu ambacho hakukitaja na kwamba hali hiyo ndiyo iliyochochea hasira zao na kumshambulia kwa mapanga mfululizo.
“Tulisikia mlipuko nje ya nyumba kwa mbele, tukapiga kelele na kuamka wote, ghafla mlango wetu ukavunjwa kwa tofali tukajaribu kutoka na kumkuta babu akiwa chini sebuleni,” alisema Doris na kuongeza kuwa watu hao waliwaamuru kulala chini.
Alisema akiwa amelala chini alisikia mmoja wa watu hao akidai kuwa ameumizwa usoni kauli ambayo ilifuatiwa na mashambulizi mfululizo kwa Dk Mvungi na kisha wakamvutia jikoni huku wakiendelea kumshambulia.
Doris alisema majambazi hao walikuwa watatu na hawakuwa wamejifunika nyuso huku mmoja akiwa amevaa kofia na kwamba laiti kungekuwa na mwanga chumbani wangewatambua. Alisema watu wengine wawili walibaki nje na walipiga baruti mbele ya nyumba.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Salome Emmanuel alisema Dk Mvungi alivamiwa nyumbani kwake na watu ambao anadhani walikuwa wakifuatilia nyendo za mmoja wa wafanyakazi wake.
“Unajua mfanyakazi wake mmoja alikuwa ndiyo kwanza amerudi kutoka matembezi na baada ya kuingia ndani haikuchukua muda mrefu mlango ulivunjwa,” alisema Salome ambaye ni mke wa dereva wa Dk Mvungi.
Salome ambaye wanaishi na mumewe jirani na Dk Mvungi, alisema baada ya milipuko inayodhaniwa kuwa ni baruti, alisikia kelele na kuona mwanga wa tochi kali ndani ya nyumba hiyo na ndipo alipomwamsha mumewe na kuanza kuhangaika kutafuta namba za simu za polisi.
Salome alisema wahalifu hao walionekana kuwa na ufahamu mkubwa wa jiografia ya eneo hilo kwani walipita uani ambako hakuna mwanga wa umeme na kuingia nyumbani kwa Dk Mvungi na hata walipoondoka walipita jirani na kwao na muda mfupi baadaye walisikia mngurumo wa pikipiki.
Polisi wakamata watano wakiwa na gongo
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema inawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhusika na tukio la kumshambulia kwa mapanga Dk Mvungi.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema watuhumiwa, ambao aligoma kutaja majina yao walikamatwa wakiwa na pombe aina ya gongo lita 17 na kete 15 bangi. Baada ya kuvamiwa, Dk Mvungi aliporwa bastola na kompyuta.
Kamanda Kova alisema baada ya msako mkali wa polisi kwa kushirikiana na raia wema waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa karibu na eneo la tukio.
Misa
Kutokana na tukio hilo Mbatia alisema leo saa 10 jioni kutakuwa na misa maalumu ya kumwombea Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi. Misa hiyo inatarajiwa kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.
Mwananchi