ABIRIA YOYOTE ATAKAYE KUTWA AMESIMAMA KWENYE DALADALA KUTOZWA FINE...KAMA KENYA VILEE

POLISI Kikosi cha Usalama Barabarani, inaandaa sheria itakayosaidia kudhibiti ujazaji wa watu kwenye magari ya abiria, ambayo abiria atakayekutwa amesimama, atatozwa faini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema kabla ya sheria hiyo kutungwa na kutekelezwa, watatafuta njia ya kutatua tatizo la usafiri kwanza.

“Ni kweli kuna maeneo ambayo kuna tatizo la usafiri, kwa maana hiyo kabla ya sheria hii kuanza kutekelezwa, ni lazima itafutwe dawa ya tatizo la usafiri na baada ya hapo ndiyo sheria ianze kutumika,” alisema Mpinga.

Akizungumzia usalama katika msimu wa siku kuu za mwishoni mwa mwaka, Kamanda Mpinga alisema matukio ya ajali ya kutisha yametokea ndani ya mwezi huu.

Alitaja ajali ya mkoani Tanga katika eneo la Kwalaguru katika barabara ya Chalinze – Segera, ambako basi la Kampuni ya Burudani lilipinduka na kusababisha vifo vya watu 12 na majeruhi 76.

Pia mkoani Arusha gari aina ya Noah ilisababisha vifo vya watu sita na majeruhi 12, Tanga katika eneo la Segera magari yaligongana na kusababisha vifo vya watu nane na majeruhi 17.

Alitaja pia ajali ya mkoani Dodoma, ambako basi la Kampuni ya Simiyu Express lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi 14.

“Haya ni baadhi ya matukio yaliyotokea kwa mwezi huu wa Desemba, mwaka huu katika mikoa mbalimbali nchini, ambayo yamesababisha majonzi miongoni mwetu na vyanzo vya ajali hizi ni mwendo kasi,” alisema.

>>Habari leo

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad