BAADA YA KUMFUKUZA ZITTO-DR SLAA AONYWA KUKANYAGA KIGOMA

*Uongozi wa mkoa wasema hali si nzuri
*Kisa Zitto kuvuliwa nyadhifa zote
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kigoma umemshauri Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.Wilbrod Slaa kufuta ziara ya kutembelea majimbo manane mkoani humo kutokana na hali ya siasa kuwa mbaya.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma jana, Alhaj Jafari Kasisiko ilisema hatua hiyo inatokana na hofu kubwa iliyotanda baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kuvuliwa nyadhifa zote na Kamati Kuu wiki iliyopita.

Kasisiko, alisema Dk. Slaa alitakiwa kuanza ziara hiyo keshokutwa lakini kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya, uongozi wa mkoa kwa pamoja umekubaliana na makao makuu kusogeza mbele ziara hiyo. “Kikao chetu kilikaaa na kutafakari kwa kina ziara ya Dk. Slaa lakini baada ya kubaini hali si nzuri, tumekubaliana kwa kauli moja kusogeza mbele ziara hii.

“Tulitegemea Dk. Slaa angetembelea majimbo yote manane ya Mkoa Kigoma na kufanya mikutano si chini ya miwili kwa kila jimbo na baadaye mkutano wa mwisho jioni ungefanyika makao makuu ya jimbo lengo likiwa kuangalia uhai wa chama,”alisema Kasisiko.

Alisema mambo makuu muhimu yaliyozingatiwa ni pamoja na usalama kwa kiongozi huyo kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto, Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Dk. Mkumbo Kitila na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha,Samson Mwingamba.

Jambo la pili lilozingatiwa ni kutoa taarifa rasmi kwa majimbo na kupokea hali ilivyo au inavyoonekana katika maeneo yao.

Alisema uongozi wa Mkoa wa Kigoma, kwa kauli moja ulipeleka taarifa makao makuu ya chama kusogeza mbele ziara hiyo kutoa fursa ya viongozi wa kanda na taifa kutembelea maeneo hayo kujionea hali halisi.

“Uongozi wa mkoa uliomba uongozi wa taifa usogeze mbele tarehe ya ziara hii muhimu kwa mkoa wetu ili mkoa kama ngazi ya chini ya kanda na taifa uende katika majimbo hayo na kuwaelimisha wanachama na wapenzi wetu kuheshimu na kuwa na nidhamu na uamuzi unaotolewa na ngazi ya juu ya chama chetu. 

“Hata kama uamuzi huu una maumivu …Katiba yetu ifuatwe katika kutatua tatizo… maoni ya wengi mkoani na viongozi wa chama ni kuudhiwa na uamuzi wa Kamati Kuu ambayo dhahiri yalilenga kuwavua nyadhifa viongozi,”alisema Kasisiko.

Alisema kutokana na hali hiyo, mkoa ulitishika na vitisho baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa majimbo kuwa hali si nzuri kwa ziara ya kiongozi mkubwa.

“Hali ya usalama ya mkoa wetu si nzuri kwa ziara ya kiongozi wetu Dk. Slaa kufika Kigoma kwa kipindi hiki wakati wanachama na wapenzi wakitafakari kwa kauli tofauti zisizolenga kuwapo usalama,”alisema Kasisiko.

Alisema kikao hicho kilijiridhisha kwa kupata maoni kutoka majimbo sita kuwa hali ni mbaya na kushauri ziara hiyo isigozwe mbele kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

“Kupitia kikao hiki, tunasema ni bora kuzuia kuliko kutibu tayari sintofahamu zimeonekana, viongozi na hasa wa majimbo kutofautiana mitazamo ni hatari katika hali hii. Mkoa umejiridhisha usalama hautakuwapo kwa ujumla hata kama baadhi ya majimbo yakisema wao wapo salama tu.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. mngemuacha aende wakamnyonyoe nywele zote amezidi

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad