WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amesema haogopi wala hazuiliwi na mtu kusema jambo la sheria juu ya utekelezaji wa shughuli zake. Amesema ataendelea kupambana na wasafirishaji na watumiaji wa barabara wanaozidisha uzito wa mizigo hadi atakapoingia kaburini.
“Siogopi kusema au kuzuiliwa nisiseme jambo ambalo lipo katika sheria. Nitaendelea kusema hadi naingizwa kaburini kuhusu watu wanaozidisha uzito barabarani… mchezo huu unaofanyika unaigharimu Serikali mabilioni ya fedha,” alisema.
Dk. Magufuli alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kusaini mikataba mitatu ya ujenzi wa barabara katika mikoa mine.
Alisisitiza kuwa siku zote atasimamia ukweli.
Waziri alisema hakuna kitu kinachomchukiza katika utendaji kazi wake kama wasafirishaji wanaozidisha uzito wa mizigo barabarani.
Alisema hapendi kuona kundi la watu wachache wakiharibu barabara kwa manufaa yao au kukiuka sheria huku Watanzania masikini wakitozwa kodi kulipa madeni ya Serikali.
Dk. Magufuli alisema anamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumpa nguvu ya kumtaka kusimamia sheria zilizopitishwa na Bunge.
“Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini zinahabirika muda mfupi kwa sababu ya maslahi ya kundi dogo, hatutaki kukarabati barabara kila mwaka.
“Ikiwa tutaendelea kuwachekea watu hao tujue wazi tunakitengenezea kizazi kijacho deni. Lazima walipe kwa sababu Serikali imeingia mikataba ya maandishi.
“Ni vema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wenye mamlaka ya kusimamia sheria wakatimiza wajibu wao na wakandarasi wahakikishe wanajenga barabara imara wanapopewa,”alisema.
Alisema kuanzia sasa, meneja yeyote wa TANROADS katika mkoa husika ambaye atashindwa kumsimamia mkandarasi wa ujenzi, ajiandae kuacha kazi.
“Kama unajua mkandarasi katika mkoa wako ameharibu kazi naomba usisubiri hadi hatua zichukuliwe kutoka ngazi za juu, tambua kazi hiyo imekushinda na jiandae kuwa mvuvi,”alisema.
Hata hivyo, Dk. Magufuli aligeuka mbogo kwa waandishi wa habari baada ya kuulizwa maswali na kuamua kuyajibu kwa mkato.
Dk. Magufuli alionekana kuchukia baada ya kuulizwa swali kuhusu timu iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutafuta suluhu ya mgogoro kati yake na wafanyabiashara wa malori.
Dk. Magufuli aliwahi kuondoa asilimia tano tozo ya uzito katika mzigo wa tani 56 unaostahili kwa lori kuruhusiwa kupita kwenye mizani za barabarani nchini.