Rais Jakaya Kikwete amewataka wajumbe watakaopata fursa ya kuingia kwenye Bunge la Katiba kuweka mbele masilahi ya Taifa badala ya makundi yao.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ripoti na Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba jana, Rais Kikwete alisema kuingiza hulka binafsi katika mchakato huo ni kuchelewesha upatikanaji wa Katiba Mpya kwa muda uliopangwa.
Alisema alipofanya mazungumzo na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, aliwataka kuweka kando masilahi ya vyama vyao na kutanguliza utaifa ili kupata Katiba yenye sura ya taifa.
“Niliwaambia na leo (jana) narudia kuwa watakapokuwa wakiijadili rasimu, watambue kuweka mbele masilahi ya taifa, malengo ya vyama na asasi zao yawe ya pili. Kama hawatafanya hivyo hatutapata Katiba,” alisema na kuongeza:
“Kama itashindikana kupata Katiba Mpya, hakutakuwa na katiba ya mpito… hii tuliyonayo sasa itaendelea kutumika, nawaelezeni na ikihitajika tena mchakato utatakiwa kuanza mwanzo na mimi nitakuwa nimesshastaafu nipo kijijini Msoga (Chalinze, Pwani).”
Alisema Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walitoka maeneo tofauti hivyo kutofautiana malengo, lakini kutokana na uzito wa uundwaji wa Katiba, waliweka kando tofauti zao na ndiyo maana rasimu waliyoiandaa ina sura ya kitaifa.
“Wajumbe wanatakiwa kuiga mfano wa Wajumbe wa Tume ambao waliweka kando tofauti zao na leo hii wamekuja na rasimu iliyo na sura ya kitaifa. Nanyi mnatakiwa kufanya vivyo hivyo,” alisema na kuongeza:
“Mtambue pia kuwa hatima ya katiba iko mikononi mwa wananchi, hivyo msifanye mnavyojua, isomeni rasimu kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho ili muweze kutoa maoni na mapendekezo kwa ufasaha zaidi kuliko kuchagua maeneo ya kuchangia.”
Rais Kikwete alisema kukamilika kwa rasimu hiyo kunatoa nafasi kwa mchakato wa kuwapata Wajumbe wa Bunge la Katiba ili ifikapo Februari 11, mwakani Bunge hilo liwe limeanza.