LEMA AMLIPUA BUNGENI NAIBU WAZIRI OLE MADEYE

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amemlipua bungeni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye kwa kumweleza kuwa sio mzigo tu, bali ni bomu hasa. Katika mchango wake kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuhusu utekelezaji wa shughuli zake kwa kuanzia Machi hadi Desemba 2013, Lema alimtuhumu Medeye kwa kuchochea ukabila mkoani Arusha.

“Taifa letu lipo katika mkanganyiko sana, chokochoko za udini na ukabila zinaletwa na wanasiasa wanapotafuta utawala…nashangaa kuona Ole Medeye aliwahi kushiriki mkutano wa ukabila uliokuwa na lengo la kuwatenga wakazi wa Arusha ambao sio wa kabila lake, ninayo DVD ya Medeye akitaka wenyeji wasiwauzie mashamba na mambo mengine wageni toka mikoa mingine.

Julai mwaka jana, viongozi  wa kimila wa kabila la Wamasai walitoa tamko wakiwataka wageni, wakazi na washirika wote kwa ujumla wao katika jiji la Arusha waonyeshe ushirikiano na kuwasaidia Malaigwanani kulinda na kuendeleza umoja, upendo, mshikamano, amani na siyo kuwa chanzo cha matatizo kwani hawatakubali kabisa.

Kabla ya tamko lao, baadhi ya viongozi hao walikuwa wakizungumzia mustakabali wa maisha ya Arusha mjini huku wakiwataka wageni (watu ambao sio Wamasai) kuacha kuleta vurugu katika eneo la Wamasai.

Akizungumzia kuhusu mlipuko wa bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti jijini Arusha, Lema alisema wapo watu katika serikali wanafanyakazi karibu na shetani.

Alishangaa kuona tukio la mlipuko wa bomu lililotokea katika mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni ya uchaguzi wa madiwani jijini humo halijaelezwa katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama.

“Tuna ushahidi wa video nani aliyerusha bomu Soweto na tukataka iundwe kamati huru na sisi tutoe ushahidi wetu lakini hakuna lolote lililotokea hadi sasa,” alisema na kuongeza, “tunashangaa wanaotueleza tulijilipua wenyewe bomu.”

Pia Lema alipinga mapendekezo ya Kamati hiyo kuitaka Serikali kupitia upya sheria zake ili hatimaye iandae muswada wa sheria itakayoweka utaratibu mahususi wa watu kuandamana utakaozingatia siku, muda na mahali ili kumwezesha mwananchi atumie haki yake ya kuandamana bila ya kuingilia uhuru wa mtu mwingine.
CHANZO: NIPASHE
Tags

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad