Dodoma.Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alipigilia msumari sakata la wabunge kuchukua posho bila kuzifanyia kazi stahiki kwa kuwaamuru wazirudishe.
Spika alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati akitoa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde akitaka ufafanuzi wa hatua ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Erasto Zambi kutumia Bunge kujitetea kuhusu tuhuma za kuchukua posho za safari bila kusafiri.
Alisema Zambi ni mbunge ,pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya na Kamishna wa Bunge anayefahamu taratibu za safari zinazoeleza kuwa kuchukua fedha bila kwenda safari ni makosa.
Silinde wakati akiomba mwongozo huo alimtuhumu Zambi kuwa alichukua kiasi cha Sh13 milioni za posho ya safari ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na nyingine kwa ajili ya safari ya shughuli za michezo lakini hakusafiri.
“Mtu anapozungumza kwa kutumia Bunge lako kujitetea kwa kukiuka taratibu, inaruhusiwa?” alihoji Silinde, ambaye pia ni Waziri kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
Kabla ya Silinde kusimama na kuomba mwongozo, Zambi alikuwa amepewa fursa na Spika ya kuchangia taarifa za Kamati za Bunge za Nishati na Madini na Miundombinu zilizowasilishwa juzi.
“Jana (juzi) kulitokea maneno maneno fulani hapa bungeni. Alisimama ndugu Silinde akasema Zambi kala hela hakusafiri,” alisema lakini kabla hajamalizia kuzungumza Spika alimkatiza... “Naomba hilo uliache unapoteza muda na haliwasaidii wananchi, changia mambo mengine muhimu,” alisema Spika Makinda huku wabunge wengi ndani ya Ukumbi wa Bunge wakipiga makofi.
Hata hivyo, Zambi aliendelea kusisitiza kuwa taswira inayokwenda kwa wananchi ni mbaya na wameanza kumpigia simu kuwa ameiba fedha na kusema hilo ni jambo baya analostahili kulisemea.
Alisema utaratibu uko wazi kama hujasafiri unarudisha fedha na kusema... “Ningekuwa kiongozi wa ajabu sana kama ningekwenda Dubai na Uingereza na kutokwenda ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutoka chama kinachotawala.”
Baada ya kueleza hayo, Spika alisimama na kusema: “Waheshimiwa wabunge nimesema kama mlichukua pesa bila safari, mnarudisha si basi…. Wote kabisa ninawajua na ninalifanyia kazi. Wote waliochukua pesa warudishe ndiyo utaratibu wa Serikali na ndivyo inavyotakiwa. Wote watarudisha.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao aliwataka wabunge kutumia kikao cha kupeana taarifa cha wabunge wote kuzungumza kama kuna tatizo lolote badala ya kuumbuana ndani ya Bunge.
Moto wa posho hizo ulikolea juzi pale Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alipoomba mwongozo wa Spika akitaka kujua hatua ya mbunge aliyechukua fedha na kwenda safari binafsi. Nchemba alisoma ujumbe wa simu uliokuwa ukionyesha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alikatisha safari ya Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Joyce Mukya.