TEAM YA TAIFA STARS KUFA NA KUPONA LEO-LAZIMA WAGANDA WAKAE

Kilimanjaro Stars yenye mastraika gumzo, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta inashuka mjini Mombasa leo kuikabili timu ngumu ya Uganda ambayo haijaruhusu hata bao moja kwenye Chalenji msimu huu.

Mechi hiyo ni gumzo zaidi kwa Wakenya ambao timu yao inacheza na Rwanda jioni kwenye Uwanja huohuo wa Manispaa ya Mombasa. Mshindi wa mechi ya Stars atacheza na mshindi wa Kenya na Rwanda kwenye nusu fainali mjini Kisumu.

Robo fainali zingine zitapigwa kesho kwa Zambia kuivaa Burundi mchana na Ethiopia kucheza na Sudan jioni. Mechi ya Stars na Uganda inatazamiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na umahiri wa wachezaji wanaounda vikosi hivyo ambao ni maarufu zaidi kwenye ukanda wa Cecafa.

Uganda chini ya Kocha Mserbia, Sredejovic Milutin ‘Micho’ imeishinda Stars katika mechi mbili za mwisho ilizocheza nao kuwania kufuzu Chan lakini kikosi cha Kim Poulsen hakikuwa na mastraika Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe wa kipa mahiri Ivo Mapunda wa Gor Mahia ya Kenya.

Mechi hiyo itakuwa na utamu wa aina yake kwani Stars itakuwa chini ya ukuta mahiri ulioruhusu goli moja wa Said Morad na Kelvin Yondani huku pembeni wakisimama Erasto Nyoni na Himid Mao.

Kwenye kiungo huenda akasimama Frank Domayo na Aboubakary Salum ‘Sureboy’ ambao watakuwa wakigawa mipira kwa Mrisho Ngassa, Ulimwengu, Samatta na Amri Kiemba.

Kikosi hicho kilicheza mechi ya mwisho dhidi ya Burundi na kutengeneza nafasi nyingi za mabao ambapo Poulsen alisema “Timu iliyocheza na Burundi ilitengeneza nafasi nyingi sana za kufunga na ilikuwa ya kushambulia zaidi, ilicheza mpira wa hali ya juu sana sioni sababu ya kuibadilisha ila tunaweza kuiboresha zaidi.”

“Tunaingia kwa nguvu kwenye robo fainali, tunakutana na timu ngumu lakini tutapambana na kuonyesha uwezo wetu tuna imani tutashinda na lengo ni kwenda nusu fainali, mashindano ndio yanaanza sasa,” alisisitiza Poulsen huku mastraika wake Samatta na Ngassa wakiahidi makubwa.

Ngassa: “Sisi tuko sawa na tumefika hapa tulipo kutokana na umahiri wetu, tutafanya kazi nzuri kwa vile tunataka kufika mbali na tunachukua hadhari kubwa.”

Uganda inaingia na ukuta imara ambayo katika mechi tatu haujaruhusu bao hata moja lakini fowadi yake imefunga mabao matano huku Stars ikiwa imefunga mawili.

Fowadi yake itakuwa na Emmanuel Okwi, Danny Serunkuma na Hamis Kiiza ambaye huenda asiwe kwenye fomu kutokana na kufiwa na baba yake mdogo juzi lakini uongozi ukamwomba abaki.

Kocha Micho alilalamika kwamba Stars imekuwa na muda mwingi wa kupumzika kuliko kikosi chake ambako kilicheza juzi Alhamisi wakati stars ilicheza Jumatano.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad