WATU SABA MBARONI KWA MAUAJI YA ALIYE KUWA MWENYEKITI WA CCM MWANZA

JESHI la Polisi mkoani Mwanza, linawashikilia watu saba kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), marehemu Clement Mabina (57). Akizungumza na RAI jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya msako mkali ili kubaini wahusika wengine.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za mashuhuda wa tukio hilo, wameeleza mauaji hayo yalifanywa na watu zaidi ya saba, hivyo jeshi hilo bado linaendelea kuwasaka wengine.

“Ni kweli tukio lilitokea jana (juzi) kati ya saa 6 na 7 mchana, ambapo marehemu alifika hapo kuweka mipaka katika eneo hilo, ambapo wananchi walitaharuki kuona mipaka ikiwekwa wakati bado kuna mgogoro wa muda mrefu.

“Baada ya hapo wananchi walivamia eneo hilo na kumhoji marehemu ndipo mvutano ulipoibuka ndipo marehemu alipojaribu kujihami kwa kutumia bastola yake na kupiga risasi juu.

“Lakini katika vurugu hizo, risasi moja ilimpata kijana mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Temeri Malimi (12) na kufariki papo hapo.

“Kutokana na kifo hicho, wananchi waliendelea kumshambulia marehemu kwa kutumia silaha za jadi hadi mauti yalipompata, ambapo miili yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Mlowola alikataa kutaja majina ya watuhumiwa kwa kile alichodai bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukulia.

Kwa upande wa msemaji wa familia ambaye ni kaka wa marehemu, Timoth Mabina alisema wamesikitishwa na kifo hicho.

Baadhi ya viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu ni pamoja na Meya wa Ilemela, Henry Matata (Chadema), Katibu wa CCM Wilaya ya Magu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Desdery Kiswaga na viongozi wengine.

Taarifa hii imeandaliwa na John Maduhu, Benjamin Masese na Peter Fabian, Mwanza
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad