Bunge limeelezwa zaidi ya Dola za Marekani 1.25 bilioni sawa na Sh2 trilioni hutoroshwa na kupelekwa nje ya nchi kila mwaka kwa lengo la kukwepa kodi.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wingu zito likiwa limegubika uwasilishaji wa ripoti ya kikosi kazi cha Serikali kilichochunguza sakata la Sh315 bilioni zilizofichwa na Watanzania katika mabenki nchini Uswisi.
Takwimu hizo zilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Zitto alisema taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza kila mwaka mapato hayo ambayo ni sawa na asilimia tano ya Pato la Taifa kupitia uhamishaji huo haramu.
“Uhamishaji huu haramu wa fedha kupelekwa nje ya nchi hufanywa kwa lengo la kukwepa kulipa kodi au wahusika kuepuka kukamatwa na fedha walizopata kwa kupokea rushwa,” alisema Zitto.
Kamati hiyo imependekeza Bunge kutunga sheria itakayodhibiti uhamishaji haramu au ufichaji wa fedha nje ya kwa lengo la kuogopa kukamatwa na rushwa, kufanya ufisadi na kukwepa kodi.
Zitto alisema hayo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa 10 wa Jumuiya ya Kamati za Hesabu za Serikali za Mabunge (Sadcopac) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Alisema katika mkutano huo uliofanyika Septemba 2 hadi 7, mwaka huu Jijini Arusha, wajumbe waliazimia kuhamasisha mabunge ya nchi zao kutunga sheria kudhibiti uhamishaji huo wa fedha.
Wiki iliyopita, mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alikaririwa akisema bungeni ‘hapatatosha’ kama ripoti ya mabilioni ya Uswisi haitawasilishwa katika Bunge hili.
Mpina alisema yeye ni miongoni mwa wabunge waliohojiwa baada ya kutamka bungeni kuwa zaidi ya Sh11.9 trilioni zimetoroshwa kutoka Tanzania kati ya mwaka 1970 na mwaka 2008.
“Nilipolisema hilo jambo niliikabidhi Serikali kupitia Bunge taarifa za tafiti mbalimbali ili ifuatilie. Baadaye Zitto akaja na hoja ya bilioni 314… tunataka taarifa hatutanii,” alisema.
Ripoti hiyo ilikuwa iwasilishwe Bunge la Aprili lakini Serikali ikaomba muda zaidi na kuahidi kuiwasilisha katika Mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea Mjini Dodoma.
----Mwananchi