HATIMAYE Meya wa Bukoba, Dk. Anatory Amani (CCM), ameamua kufunguka na kuweka wazi ufisadi unaofanyika ndani ya Halmashauri ya Bukoba. Mbali ya ufisadi huo, ameainisha udhaifu na upendeleo wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), alioufanya wakati wa ukaguzi ndani ya halmashauri hiyo kwa lengo la kumuondoa katika nafasi yake ya umeya. (HM)
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania Dk. Amani alisema ameamua kuweka wazi mambo yaliyopo Bukoba jamii ifahamu kinachoendelea na kuchukua hatua.
Alisema kikao kilichofanyika Januari 17, mwaka huu kwa ajili ya ukamilishaji wa ukaguzi maalumu wa CAG katika Ofisi ya mkuu wa mkoa, ndicho kilichokuwa na ajenda ya kumchafua na kumng'oa nafasi ya umeya.
Alisema alishangazwa na taarifa nzima iliyosomwa na CAG, ikimlenga na kumdhalilisha huku ikikwepa kuwachukulia hatua watu wengine walioonekana kuhusika na ufisadi, ubadhirifu na udanganyifu na badala yake kumkaba koo yeye.
Aliainisha ufisadi uliogundulika katika ukaguzi wa CAG na kuonyesha udhaifu mkubwa wa kutochukua hatua dhidi ya wahusika.
Alisema kuna ufisadi uligundulika katika ukaguzi wa CAG wa Naibu Meya wa Bukoba, Alexander Ngalinda, kusaini mkataba wa mradi wa viwanja 5,000 kati ya Halmashauri hiyo na UTT bila ridhaa ya baraza la madiwani.
"Ni kosa kubwa mtu kusaini mradi mkubwa wa aina hiyo bila baraza la madiwani kuridhia au kujulishwa, lakini CAG hakusema ni hatua gani zichukuliwe juu ya ufisadi huo, pia kuna viwanja vingine 800 ambavyo wananchi walichangishwa fedha na halmashauri na kupatikana shilingi milioni 45.
"Katika ugawaji wananchi waliopata ni 313 na 487 hawakupewa licha ya kuchanga, sasa katika ukaguzi wa CAG haikuonekana fedha hizo zilivyotumika na hakukuwapo na nyaraka yoyote ya fedha hizo.
"Pia haikujulikana viwanja hivyo vililipiwa mwaka gani hilo ni kosa, ambapo hakupendekeza hatua zichukuliwe kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kabla haijawa Manispaa, Samweli Luangisha," alisema Dk. Amani.
Alizidi kuanisha ufisadi ulipo na kusema taarifa ya CAG ilibaini kuwapo na gari yenye namba za Serikali za Mitaa (SM) aina ya min bus, ambayo imeegeshwa kwa muda mrefu katika jengo la Kasibante FM radio, inayomilikiwa na Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Hamis Kagasheki.
Alisema ilipohojiwa gari hilo ni mali ya nani Mkurugenzi wa manispaa hiyo alikana si mali yao, lakini nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha ni mali ya manispaa hiyo.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za CAG, baada ya kumhoji, Kagasheki alikiri kuwa gari hilo alilinunua kwa fedha zake lakini hajalibadilisha namba za usajili.
Alisema anashangazwa na kitendo cha CAG kwa kupendelea na kutochukua hatua ya kumtaka, Kagasheki kutoa uthibitisho kama kweli alilinunua kwa ajili ya kujiridhisha na kuongeza kumekuwapo na watu kujimilikisha mali za umma.
Alisema ufisadi mwingine uliobainika katika halmashauri hiyo, ni baadhi ya madiwani kuchukua posho za safari ya kwenda ziara ya mafunzo mkoani Morogoro katika Shirika la Mizinga, lakini baadhi yao hawakwenda.
Alisema ilibainika madiwani wawili kati ya 19 hawakwenda ziara hiyo na mmoja wao ambaye ni Murungi Kichwabuta alichukua posho ya Sh 480,000 lakini hakwenda ambapo CAG hakupendekeza hatua zozote.
Alisema katika ukaguzi wa CAG, ulibaini kuwapo na uteuzi batili wa mjumbe wa bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Bukoba (BUWASA), uliofanywa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kwa kumteua Kichwabuta.
Alisema CAG alibainisha uteuzi wa mjumbe huyo ulivunja sheria na hautambuliki, lakini hakupendekeza ni hatua gani zichukuliwe.
Alisema akiwa kama meya walipendekeza vibanda vitozwe Sh 30,000 na kodi ya pango iwe Sh 15,000 lakini baadhi ya madiwani waligundulika kuwa madalali na kupangisha kwa Sh 45,000 hadi 90,000 lakini CAG hakuainisha hatua za kuchukuliwa.
Kuhusu tuhuma zake, alisema tuhuma anazotuhumiwa na kulazimishwa kujiuzulu kwa mujibu wa taarifa za CAG ni kupewa kituo cha kuoshea magari ambacho bodi ya zabuni ilishindanishwa na kampuni nyingine na kuonekana kutokuwapo na uhalali, huku akionekana kusaini mkataba huo.
Alisema anatuhumiwa kusaini mkataba wa UTT na nyongeza ya tathmini ya awali ya viwanja 5,000 ambavyo kwa mujibu wa CAG alidai kuwa tathimini hiyo haikuwa ya kisayansi kwa kuwa watendaji walialikwa ofisini na kukadiria fidia ya Sh bilioni 1.3.
"Tamko lililotolewa na Naibu Waziri wa Tamisemi, Agrey Mwanri ya madiwani na waandishi wa habari lililenga kunidhalilisha, tamko hilo lilitokana na amri ya baraza la madiwani kupiga kura ya kutokuwa na imani na mimi.
"Nasema hadi sasa mimi ni diwani kwa mujibu wa sheria, si kwamba nang'ang'ania umeya, la hasha bali napenda kutunza heshima yangu kama raia wa nchi hii, ninazo haki za kikatiba.
"Kama wanataka nijiuzulu kwa tuhuma zinazoelekezwa kwangu, twendeni katika vyombo vya sheria na ikibainika ndio nijiuzulu na kuchukuliwa hatua, lakini kwanza CAG atoe mapendekezo ya wale waliokutwa na makosa katika ripoti yake ya ukaguzi," alisema Dk. Amani.
Chanzo: mtanzania
KILA SIKU MSEMA KWELI NDIYE MUOVU NA WENGINE KUWENI WAWAZI KAMA HUYO MEYA WA BKB
ReplyDeleteKwa nn akusema hayo tangu mwanzo?baada ya kuambiwa ajiuzulu ndio anasema?hoja yake haina mshiko awajibike tu.
ReplyDeleteKweli kaka lazima awajibike
ReplyDeleteSiku zote alikuwa wapi au ndio mpaka kibarua kiote nyasi ndio unaanza kubweka tafuta kazi nyengine wewe si dokta?
ReplyDelete