BARAZA FEKI LA MAWAZIRI LAZUA MTAFARUKU...IKULU YAWAKA

Joto la uteuzi wa Baraza la Mawaziri limeendelea kupanda hadi kufikia baadhi ya watu kuunda na kutangaza baraza ‘feki’ lililoibua mtafaruku kwenye jamii, kiasi cha kuwafanya wananchi kupiga simu chumba cha habari kutaka kujua ukweli wa taarifa hizo.

Hii ni kufuatia mitandao ya kijamii kuchapisha taarifa za kutangazwa kwa Baraza hilo huku baadhi ya wananchi wakitumiana ujumbe mfupi wa simu kuhusu taarifa hizo.

Taarifa ya mtandao wa Matukio UK, iliyosema tayari Rais Jakaya Kikwete, ametangaza Baraza la Mawaziri juzi usiku na kuingiza sura mpya na baadhi za waliomo sasa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, ameteuliwa kuongoza Wizara ya Uchukuzi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alikanusha taarifa hizo akieleza kwamba Baraza la Mawaziri haliwezi kutangazwa kwenye mtandao.

Balozi Sefue alisema hana habari kuwa Rais Kikwete ametangaza Baraza la Mawaziri.

Alipoambiwa kuwa habari hizo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Balozi Sefue alisema: “Hiyo (mitandao ya kijamii) wala sihusiki nayo. Hayo mambo ya mtandao siwezi kuyajibia. Baraza la Mawaziri halitangazwi kwenye mitandao. Vuteni subira tu.”

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limeahidi kufuatilia taarifa hizo kwa kuwa ni sawa na uhalifu wa mtandao (cyber crime).

Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alisema  jana kwa ufupi kwamba: “Ngoja tufuatilie.”

Aidha, Baraza hilo feki halikutaja Naibu Mawaziri na hata baadhi ya sura mpya zilizodaiwa kuteuliwa na Rais siyo wabunge kama Katiba inavyotaka, huku ikiacha kutaja Mawaziri walioteuliwa kuongoza baadhi ya wizara kama ile ya Uwezeshaji na Uwekezaji, ambayo imeachwa wazi kwa madai kuwa waziri wa sasa amehamishiwa wizara nyingine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya mtandao, sura mpya ni pamoja na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Baramagamba Kabudi na Profesa Paul Mbawala, ambao hawana sifa za kuteuliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa siyo wabunge kwa mujibu wa Katiba.

Katika taarifa hiyo, Kabudi ameteuliwa kuongoza Wizara ya Elimu wakati Profesa Mbawala amepelekwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Sura nyingine mpya ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, ameteuliwa kuongoza Wizara ya Afrika Mashariki na Samuel Sitta, amehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Wengine walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo na Wizara zao kwenye mabano ni Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), January Makamba (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk. Harrison Mwakyembe (Tamisemi), Dk. Abdallah Kigoda (Fedha), Profesa Mark Mwandosya (Utumishi), Aggrey Mwanri (Ujenzi), Dk. John Magufuli (Maliasili na Utalii), Charles Kitwanga (Mifugo na Uvuvi na Dk. Charles Tizeba (Mambo ya Ndani).

Wengine ni Dk. Mary Nagu (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe (Maji) na Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi). 

CHANZO: NIPASHE
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. jinsi magazeti yanavyoendelea kuandika, inabidi ikulu waendelee kubadilisha majina, kazi kweli kweli

    ReplyDelete
  2. huyu muongo halisi kazi kwake!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad