GAVANA NDULA AKUMBWA NA KASHFA YA UTAPELI

ALIYEKUWA mfanyakazi wa ndani wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Benno Ndulu, amedai  kutolipwa haki zake na mwajiri wake huyo baada ya kukatisha mkataba wa kazi nchini Marekani.

Pia amedai bosi wake huyo ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi Benki ya Dunia, Marekani, ameendelea kuishikilia hati yake ya kusafiria tangu aliporudishwa nchini mwaka 2005.

Akizungumza na Tanzania Daima juzi, mfanyakazi huyo, Velena Melciady, alisema mwaka 2003 aliingia makubaliano ya miaka sita na Ndullu kuwa mfanyakazi wake wa ndani nchini Marekani.

“Nakala ya makubaliano hayo sina, lakini tuliandikishana. Nilipofika nilikuwa nalipwa dola 500 kwa mwezi, lakini baada ya mwaka mmoja na nusu nilitakiwa kulipwa dola 700, ndipo alipokataa na kunirudisha Tanzania kama mkimbizi.

“Alisema hawezi kulinipa mshahara huo kwa kuwa hata watoto wake hawapati mshahara huo,” alisema Velena akimnukuu Ndullu wakati huo.

Hata hivyo, alisema tangu wakati huo hajamlipa haki zake za kukatisha mkataba pamoja na hati yake ya kusafiria bado anayo.

Alipotafutwa Gavana Ndullu kuhusiana na madai hayo alikana kuwa na hati yake ya kusafiria. Mahojiano kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yalikuwa kama ifuatavyo:

Tanzania Daima: Habari za kazi, kuna malalamiko ya Velena kutompa haki zake baada ya kukatisha mkataba wa kazi za ndani huko Marekani, pia mpaka sasa umeendelea kushikilia hati yake ya kusafiria

Ndullu: Sina hati yake na haki zake zote alipata kisheria na kwa ushahidi wa kiserikali  Marekani (marejesho  ya kodi-tax returns kama employer ninazo).

Tanzania Daima: Je, ninaweza kupata hayo marejesho ya tax ya kisheria uliyosema unayo ili inisaidie katika habari yangu?

Ndullu: Njoo kisheria. Muulize pia alisafiri vipi kurudi bila hati ya kusafiria?

Tanzania Daima: Mimi nilikuwa nahitaji kwa ajili ya ‘ku-balance’  stori, si kufuata sheria kama  unavyotaka bali nia nikupe nafasi nawe uweze kuzungumza kwa upande wake kama ethics zinavyohitaji.

Ndullu: Eleza kikamili nitakujibu kikamili.

Ndullu: Nasema hivi kuwa swala hili linaweza likawa legal. Nielewe kwa maana hii.

Tanzania Daima: Nimeelewa, nayafanyia kazi haya uliyonijibu.

Alipopigiwa simu Velena kuhusu hati ya kusafiria ilichukuliwa vipi na Ndullu, alisema aliporejeshwa nchini akiwa amesindikizwa na mtoto wa Ndullu aitwaye Ndulika na kwamba baada ya kuwasili nchini mkewe Ndullu alimwamuru mtoto huyo arudi na hati hiyo ya kusafiria kwa kuwa wana kazi nayo.

“Kama anasema ana ushahidi nimelipwa autoe…sijalipwa kitu chochote nilirudishwa  Tanzania  kama mkimbizi. Aliniambia nitakuwa narudi likizo baada ya miaka miwili ama nikipata tatizo la kufiwa, lakini nilirudishwa bila kuwapo kwa tatizo lolote. Namuomba Rais Kikwete aingilie kati suala hili ili niweze kulipwa haki zangu,” alisema Velena.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. We muandishi gavana anaitwa Ndulu sio Ndula. Mxiiiuuu rudini shule kila spelling mnakosea.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad