IKULU YAVUNJA UKIMYA KUHUSU MAWAZIRI MIZIGO

Dar es Salaam. Ikulu imetaka kufungwa kwa mjadala wa kuhusu kurudishwa kwa mawaziri wanaodaiwa kuwa ni mizigo kwenye Baraza la Mawaziri na badala imetaka waachwe wafanye kazi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema kuendeleza mjadala huo ni kupoteza muda, kwani Rais Jakaya Kikwete alishamaliza kazi yake.

Rweyemamu alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua mawaziri ambao wana wajibu wa kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo si sahihi wateule hao kuitwa ‘mizigo’ kwani yeye (Rais) ameona wanafaa.

“Rais anapoteua watu anaangalia wanaofaa kumsaidia na si vinginevyo. Kwani lengo lake ni kuona nchi ina `move forward’ (inasonga mbele) kimaendeleo,” alisema Rweyemamu. Alisema watu wanapaswa kukumbuka kuwa mtu anapoteuliwa kwenye uwaziri kuna suala la uwajibikaji: “Anatakiwa kutekeleza uwajibikaji wa pamoja. Sasa kumshambulia mtu binafsi na kumwita mzigo siyo sahihi.”

Rweyemamu alisema mjadala huo kwa sasa umepitwa na wakati na kuwataka wananchi na wachambuzi kuwaacha mawaziri hao kuchapa kazi.

“Ni vizuri wananchi wakawapa nafasi mawaziri hawa ya kufanya kazi na baadaye kuwapima na kuwachambua kutokana na utendaji wao,” alisema.

Chimbuko la majadala

Mjadala kuhusu suala hilo unatokana na Rais Kikwete kuwarejesha katika Baraza la Mawaziri baadhi ya mawaziri ambao walidaiwa kuwa ni mizigo kutokana na udhaifu katika utendaji wao.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ndiyo walioasisi mawaziri hao kuwa ni ‘mizigo’ walipokuwa na ziara ya kikazi mkoani Ruvuma, mwishoni mwa mwaka jana.

Mawaziri waliolalamikiwa kutokana na utendaji wao ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo, Waziri wa zamani wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa na aliyekuwa Naibu wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.

Baadaye baadhi ya wabunge nao walikoleza moto kwa kushinikiza mawaziri hao wang’oke, huku wakiongeza idadi yao kwa kuwataja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa katika kundi hilo.

Mawaziri hao waliitwa kujieleza mbele ya Kamati Kuu ya CCM kuhusu sababu za utendaji wao kuwa wenye matatizo.

Hata hivyo, kabla ya Rais Kikwete kuchukua hatua, alitengua uteuzi wa Mawaziri wanne, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii na Dk Mathayo kutokana na mjadala mkali bungeni kuhusu jinsi Serikali ilivyotekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili.

Kadhalika, Dk Mgimwa aliyefariki dunia Januari 5, mwaka huu alisababisha pengo la mawaziri kufikia watano.

Wakati Rais Kikwete alipofanya mabadiliko katika Baraza lake Januari 19, mwaka huu, karibu mawaziri wote waliolalamikiwa walirejeshwa.

Hali hiyo ilizusha mjadala mkali kutoka kwa watu na makundi mbalimbali, huku CCM kupitia kwa Nape Nnauye kilisema kitaendelea kupiga kulele pale utendaji wa mawaziri hao utakapokuwa mbovu.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Watanzania hawako serious na maisha yao,mmesikia mama wa Kimalawi anvyofanya kwa viongozi walioiba pesa za wananchi?Watu wenye msimamo na dhamira ya kuleta haki kama hawa ndio wanahitajika,lakini sisi mtu akifuturishwa na mbunge au waziri anaona ndio kasaidiwa kesho akiumwa hospitali hakuna dawa,mwenzake akiumwa anakwenda nje kutibiwa.Kwa hiyo hatureason tunapenda vitu rahisi vya kijinga kijinga.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad