JAKAYA KIKWETE ATEUWA MAJINA YA WABUNGE WA BUNGE LA KATIBA

Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amekamilisha uteuzi wa majina ya Wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, litakaloanza vikao vyake Februari 18 mjini Dodoma.

Kupitia uteuzi huo amewarejesha bungeni wanasiasa wakongwe akiwamo Kingunge Ngombale Mwiru na Paul Kimiti na kuwakumbuka pia wanasiasa wakongwe ambao hawakuwahi kuwa wabunge.

Baadhi ya wanasiasa hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha (NLD) Dk Emmanuel Makaidi na Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi Tanzania (Chausta) James Mapalala.

Pia wamo Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila na John Chipaka ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Tadea.

Bunge hilo litajumuisha wabunge wote 357 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe 82 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na 201 waliotangazwa jana na kufanya idadi yao kuwa 640.

Akitaja majina hayo jana Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Florens Turuka alisema wajumbe hao wameteuliwa kutoka katika makundi 10 ya kijamii.

Aliyataja makundi hayo na idadi ya walioteuliwa katika mabano kuwa ni Taasisi zisizo za Kiserikali (20), Taasisi za Dini (20), Vyama vya Siasa (42), Taasisi za Elimu (20), Makundi ya Walemavu (20), Vyama vya Wafanyakazi (19), Vyama vya Wafugaji (10), Vyama vya Wavuvi (10), Vyama vya Wakulima (20) na Makundi yenye Malengo yanayofanana (20).

“Taasisi 554 kutoka Tanzania Bara na 178 kutoka Zanzibar ziliwasilisha mapendekezo yao yaliyojumuisha majina 2,762 kwa upande wa Bara na upande wa Zanzibar yalihusisha watu 874,” alisema na kuongeza:

“Majina yote yalikuwa 3,636, lakini kinyume na sheria watu 118 walipendekeza wenyewe na kufanya idadi ya majina yaliyopendekezwa kuwa 3,754. Taasisi hizo zilileta majina mengi na kazi ya kuyachuja mpaka kubaki 201 ilikuwa ngumu,” alisema Turuka.

Alisema uteuzi huo umezingatia umri wa waombaji na kwamba wenye umri kuanzia miaka 22 hadi 35 wapo 35, wenye umri wa miaka 36 hadi 60 ni 145 na kuanzia miaka 65 na kuendelea wapo 21.

“Wameteuliwa kwa kuangalia umri, jinsi, uzoefu, sifa na mahali anapotoka mjumbe husika. Wanawake wapo 100 na wanaume wapo 101, wajumbe waliotokea Zanzibar ni 67 na waliotokea Tanzania Bara ni 134,” alisema.

Alisema katika kila kundi wajumbe kutoka Tanzania Bara wapo theluthi mbili na wale kutoka Zanzibar theluthi moja.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sasa tusubiri tusikie ujinga wa tundu lisu na wenzake coz wao ni Kulalamika tu na kuona hawatendewi Haki

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad